Prime
Siri ya mamilioni! Mjadala mzito Yanga kumtumia Fabrizio Romano
BAADA ya Yanga kumtumia mwandishi nguli wa habari za mpira wa miguu, hususan usajili wa wachezaji, Fabrizio Romano kutangaza jezi itakazozitumia katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika, kumezuka mijadala inayolenga kusifu hatua hiyo ama kukosoa.
Wanaosifu wanasema hatua ya kumtumia mwandishi huyo raia wa Italia imeongeza wigo wa kujulikana kwa klabu, soko na kuongeza thamani ya jezi hizo, ikiwa ni siku mbili kabla ya Yanga kuivaa Gaborone United katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa itakayofanyika Botswana.
Wanaokosoa wanasema, ingawa wanakubali kuwa ni hatua kubwa, kitendo cha Romano kutoweka video hiyo ya kutangaza jezi za Yanga kwenye akaunti yake ya Instagram, yenye wafuasi milioni 50 kote duniani, kinapunguza uzito wa mkakati wa masoko wa klabu hiyo. Na baadhi wanadai mwandishi huyo maarufu kwa kuibua habari sahihi za uhamisho wa wachezaji anatoza fedha nyingi kwa kila taarifa anayotuma kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii na hivyo Yanga kushindwa kumudu.
Harakati zake za kuwa wa kwanza kuibua habari sahihi za uhamisho zimesababisha awe maarufu duniani na baadhi ya vyombo vya habari humkariri kama chanzo vinapozungumzia uhamisho wa wachezaji nyota.
Ukichanganya akaunti yake ya Instagram yenye zaidi ya wafuasi milioni 50, Romano anakadiriwa kuwa na wafuasi zaidi ya milioni 80 kwenye akaunti zake zote za mitandao ya kijamii, yaani Facebook, X (zamani Twitter), YouTube na TikTok. Wingi huo wa wafuasi ndio unamfanya awe maarufu na hivyo wadau wengi kupenda kutumia akaunti zake kwa ajili ya kukuza soko la bidhaa zao, ama kuongeza thamani, kupongeza, kupongezwa, kusifiwa na mambo mengine.
Mchezaji anapotajwa kwenye akaunti za Romano kwamba anasemekana kugoma kusaini mkataba mpya, au anasakwa na klabu kubwa, ghafla thamani yake huongezeka na kuingia kwenye mgogoro na klabu yake na pengine kununuliwa na klabu iliyokuwa ikimmezea mate.
Hadi sasa bado hakuna takwimu za mauzo ya jezi za Yanga yamekuwaje baada ya Romano kuzitambulisha kwa msemo maarufu wa “Here We Go” ambao Mtaliano huyo anasema huutumia pale mambo yanapokuwa yana uhakika.
Hata hivyo, video zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha mashabiki na wanachama wakimiminika makao makuu ya Yanga yaliyopo katika makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani, kwenda kununua jezi hizo na wengi wakilitaja jina la Romano kuwa ndilo limewavuta kuzifuata.
Umaarufu wake mitandaoni na bei anazoweka kwa wateja wake umemfanya awe mmoja wa mabilionea duniani na mwaka 2023 jarida la Forbes lilimuorodhesha katika mabilionea 30 duniani waliokuwa na umri chini ya miaka 30.
Wakati Romano hana viwango vya aina moja vya tozo zake na ambavyo vimewekwa hadharani kwa ajili ya kutangaza biashara yake, habari zinazovuja na kurasa za watu maarufu duniani hutoa picha halisi ya kiasi gani kinalipwa kupata nafasi ya sifa au pongezi katika majukwaa yake.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Norway na Denmark vilivyofanya utafiti wa mapato ya nguli huyo wa habari, kutajwa au salamu kwenye kurasa za Romano kunagharimu kati ya dola 200 za Kimarekani hadi 1,100 (sawa na takriban Sh500,000 za Kitanzania hadi Sh2.6 milioni). Yaani salamu ndogo ya pongezi ni kuanzia Sh500,000, wakati posti ya kawaida ya viwango hugharimu Sh2.6 milioni.
Romano pia hutoza hadi Dola 6,000 (takriban Sh18.5 milioni) kwa tangazo la video lililopangwa vizuri likionyesha uhamisho au kutangaza bidhaa.
Lakini kwa matangazo ya video ya bidhaa za mashirika makubwa (corporate) yanayojishughulisha na mambo ya teknolojia, programu na ubashiri, menejimenti yake ndio huyashughulikia. Na kwa sababu anavuta wafuasi zaidi ya milioni 50, bei yake ni lazima iwe maelfu ya dola.
Na kwa sababu Yanga imo katika kipengele hicho cha mwisho, ni lazima ilikadiriwa maelfu ya dola kuweza kumtumia Romano kutangaza jezi zao.
Lakini huwezi kutarajia mavuno makubwa bila ya kupanda mbegu bora. Yanga imefanya uamuzi sahihi kumtumia nguli huyo wa Transfer Rumours kupanda ngazi nyingine kimataifa.
MAKANDOKANDO YAKE
Hata hivyo, Romano amekumbana na kashkash katika kazi yake, akituhumiwa kujaribu kufanya mbinu na baadhi ya klabu au wachezaji ili avumishe habari za usajili na hivyo kuongeza thamani ya mchezaji.
Ni kweli habari za usajili na uhamisho huvuta masikio ya wengi duniani na kuongeza thamani ya mchezaji na pia kuongeza faida kwa mawakala. Lakini taarifa hizo ndio malipo pekee kwa huduma za Romano? Hili ni swali lililosababisha waandishi wa Denmark na Norway kumchunguza 2024. Gazeti la Tipsbladet lililokaririwa na mtandao wa dynamo.kiev.ua linasema si taarifa pekee. Ilitumia habari ya uchunguzi dhidi ya Romano kuhusu winga chipukizi wa Copenhagen, Roney Bargie.
Romano aliandika katika akaunti yake ya Twitter wakati huo kuwa winga huyo mwenye miaka 18 na aliyefunga bao katika mechi dhidi ya Manchester United katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, alipoteza nafasi kwenye kikosi hicho kwa sababu hakutaka kusaini mkataba mpya na klabu yake ya Copenhagen.
Copenhagen ilikanusha habari hizo na mchambuzi wa gazeti la Tipsbladet, Troels Togersen akaandika kuwa suala hilo linaonyesha ni kwa jinsi gani mawakala, kwa msaada wa Romano, huziwekea shinikizo klabu.
“Nafahamu Fabrizio Romano anapendwa na wengi. Lakini pia kwamba mara kadhaa anapewa maelekezo na mawakala na hupata taarifa kutoka kwao. Tuna nyaraka zinazoonyesha ni kwa jinsi gani kampuni inayowakilisha huduma za Romano inavyowasiliana na klabu za Denmark na nyingine na kutoa fedha kwa ajili ya kutangazwa. Klabu inaweza kutoa fedha kidogo na Romano ataandika kitu kuhusu klabu au mchezaji kwenda kwa wafuasi wake milioni 20 wa Twitter (sasa X) na milioni 27 (sasa milioni 50) wa Instagram,” anaandika Togersen akikaririwa na dynamo.kiev.ua.
“Hilo linasema mengi kwamba kampuni inayomuwakilisha Romano hujaribu kutengeneza mahusiano na klabu. Kinachoandikwa na Romano ni lazima kiangaliwe kwa makini kwa kuwa kinafanywa kwa sababu za kibiashara. Huu si uandishi wa habari, hii ni biashara.”
Kwa mujibu wa mtandao huo, gazeti la Tipsbladet liliwasiliana na Romano lakini hakujibu ujumbe wao.
Gazeti la Norway la idrettspolitikk liliripoti kuhusu pendekezo la kampuni na bei za Romano. Kwa mujibu wa mkurugenzi wa zamani wa masoko wa gazeti hilo, Meran Amundsen-Ansari, mwaka 2022 klabu ya Norway ya Vålerenga ilipokea barua ya pendekezo la kusambaza uvumi kuhusu wachezaji wake kwenye majukwaa ya Romano.
Idrettspolitikk liliripoti wakati huo kuwa klabu kadhaa za Norway na Denmark zilipokea ujumbe wenye ofa kama hizo. Ofa hizo huwa haziandikwi na Fabrizio Romano mwenyewe bali kampuni inayoitwa Memmo, ambayo huwezesha mtu kupata moja kwa moja mawasiliano ya simu ya mtoaji habari wa ndani.
Idrettspolitikk iliwasiliana na Romano na kampuni ya Memmo lakini hakukuwa na majibu. Hata hivyo, Meran Amundsen-Ansari anasema hakutumia huduma hiyo. “Haikuwa na maana kwetu. Nimekuwa nikifanya kazi kwa miaka saba katika soka la juu, nimepokea ujumbe kutoka sehemu nyingi, lakini si kama huu. Kinadharia huyu anaweza kuwa mmoja wa waandishi maarufu duniani,” anasema Amundsen-Ansari.
“Nakumbuka niliacha kumfuatilia baada ya habari hii.”
ALIANZA KIJANA MDOGO
Romano alianza kazi ya uandishi wa habari akiwa na miaka 18, alipokuwa TuttoMercatoWeb, kabla ya kujiunga na Sky Sport Italia ambako alifanya kazi kwa karibu na mwandishi nguli Gianluca Di Marzio.
Akiwa amepania kujenga himaya yake, Romano alianza mradi wake ambao baada ya muda ukawa na mafanikio makubwa, kiasi cha kumwezesha kutambuliwa kuwa mmoja wa mabilionea walio na umri mdogo.
Anashirikiana na vyombo vya habari maarufu duniani vya CBS Sports Golazo, Sky Sports, The Guardian pamoja na vingine vingi vya kimataifa, wakati amejijengea jina mitandaoni linalompa fedha nyingi.
Mtandao wa Reporteri, ukikariri jukwaa la “Hafi” ambalo huchakata mapato kwa kutumia wafuasi, views na ushirikishaji (engagement), Romano alipata kati ya Dola 298,826 na 416,158 kwa mwezi Juni pekee 2025, kupitia Instagram, TikTok na YouTube.
Zaidi ya nusu ya mapato yake (kati ya Dola 232,000 na 318,000) hutokana na akaunti yake ya Instagram.
Mapato yake kwa mwaka yanakisiwa kufikia Dola 3.5 milioni na milioni 4.9, mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko kubwa kunganisha na mwaka 2023, wakati mtandao wa “Wtfoot” ulipokadiria thamani ya utajiri wake kuwa ni Dola 2.1 milioni. Wakati usajili ukiwa umepamba moto, Reporteri linaripoti, Romano hulala masaa matano tu kwa siku kutokana na kuwasiliana na mawakala, wachezaji na klabu kote duniani.
Licha ya kasi hiyo kubwa, Romano anasema hakuwahi kuhisi kuwa angepata mafanikio hayo.
“Nimekuwa nikipenda mitandao ya kijamii, lakini sikuwahi kufikiria kuwa nitaanzisha chapa kama hii,” aliuambia mtandao wa TransferMarket.
Anasema msemo wake maarufu wa “Here We Go” ulikuja kwa bahati.
“Niliandika mwishoni mwa ujumbe wangu (mtandaoni) na watu wakaanza kuulizia kama kulikuwa na lolote katika ujumbe huo. Baada ya kuona wasomaji wengi wamefurahishwa, niliamua kuuendeleza na kuupa uzito unaostahili – kuutumia wakati kila kitu kinapokuwa sawa na dili ni la kweli,” anasema Romano.
Romano anaendelea kuwa nguli wa habari za uhamisho kote duniani na hakuna shaka kwamba kitendo cha Yanga kumtumia bilionea huyo kuzindua jezi zao kitakuwa na maana kubwa kwa biashara yao msimu huu katika soko ambalo linazidi kuwa na ushindani, huku likikabiliwa na tatizo kubwa la bidhaa bandia.