Kiungo Twiga Stars afariki dunia, kuzikwa kesho
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mwanafamilia aliyejitambulisha kwa jina la Khadija Yahya, Madaba alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya muda mrefu ambapo alilala kitandani kwa takribani miaka mitano. Mazishi yake yamepangwa kufanyika kesho Julai 18, 2025 saa 7 mchana katika makaburi ya Yombo.
KIUNGO wa zamani wa timu ya taifa ya Wanawake Tanzania, Twiga Stars, Arafa Yahya 'Madaba' amefariki dunia leo Julai 17, 2025 nyumbani kwao Yombo Kilakala jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mwanafamilia aliyejitambulisha kwa jina la Khadija Yahya, Madaba alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya muda mrefu ambapo alilala kitandani kwa takribani miaka mitano. Mazishi yake yamepangwa kufanyika kesho Julai 18, 2025 saa 7 mchana katika makaburi ya Yombo.
Wakati wa uhai wake, Madaba aliacha ujumbe kwa wachezaji wenzake akisema: "Najua mnapambana sana lakini nawashukuru sana kwa kuwa na mimi tangu naanza kuugua hadi nilipo, na hata nikifa kesho sitasahau wema wenu ndugu zangu."
Kwenye maisha yake ya soka, Madaba alizichezea timu za Evergreen, Uzuri Queens, TMK Sisters na Mlandizi Queens.
Kutokana na msiba huo, kipa wa zamani wa Twiga Stars na Uzuri Queens, Hanifa Iddy, amesema: "Nimehuzunika sana, ni mtu niliyecheza naye wakati ule, soka la wanawake halilipi, kuna wakati mchezaji anaumwa lakini anakosa hata mahitaji ya kujitibua."
Naye kiungo wa Tausi Queens itakayoshiriki Ligi Kuu Wanawake msimu ujao, Zuwena Aziz, amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha Arafa ambaye pia aliwahi kucheza naye.
"Ndio hivyo mwenzetu ametangulia, aliugua sana, ni mtu ambaye tumeishi vizuri, mara kadhaa nimewahi kumjulia hali alikuwa anasema hata akifa leo hatasahau umoja wetu," amesema Zuwena.