Kiakala anukia Namungo FC
Muktasari:
- Nyota huyo ameihakikishia Polisi Tanzania kucheza Ligi Kuu Bara baada ya msimu wa 2025-2026 katika Ligi ya Championship kumaliza ikiwa nafasi ya tatu na pointi 66, jambo lililoiwezesha kupata fursa hiyo kupitia kucheza mechi za Play-Off.
BAADA ya kuchangia Polisi Tanzania kurejea Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Tariq Seif Kiakala yuko katika hatua za mwisho za kujiunga na kikosi cha Namungo FC.
Nyota huyo ameihakikishia Polisi Tanzania kucheza Ligi Kuu Bara baada ya msimu wa 2025-2026 katika Ligi ya Championship kumaliza ikiwa nafasi ya tatu na pointi 66, jambo lililoiwezesha kupata fursa hiyo kupitia kucheza mechi za Play-Off.
Msimu wa 2025-2026, timu hiyo ilimaliza nafasi ya tatu na pointi 66, baada ya kushinda mechi 20, sare sita na kupoteza nne na kucheza Play-Off ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya Kwanza iliyomaliza ikishika nafasi ya nne na pointi 61.
Katika mechi za Play-Off, Polisi Tanzania ilianza kwa kishindo kwa kuitoa Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 7-1, baada ya kushinda kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora mabao 4-0, kisha kushinda kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi mabao 3-1.
Baada ya hapo, Polisi ikacheza mechi nyingine ya Play-Off dhidi ya Tanzania Prisons iliyoshika nafasi ya 13 na pointi 32, katika Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, ambapo kikosi hicho kilishinda kwa jumla ya mabao 4-1.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika, Polisi iliifunga Prisons mabao 4-0, Julai 12, 2026, kisha marudiano kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ikachapwa bao 1-0, Julai 16, 2026 na kurejea Ligi Kuu kwa jumla ya mabao 4-1.
Baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na kikosi hicho kilichorejea tena Ligi Kuu Bara tangu kiliposhuka msimu wa 2022-2023, Kiakala yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na Namungo FC, kutokana na kiwango chake kizuri alichokionyesha.
Kwa msimu wa 2025-2026, Kiakala aliifungia Polisi Tanzania mabao tisa katika Ligi ya Championship, huku akicheza timu za Stand United, Biashara United, Yanga, Mbeya City, Geita Gold, Kagera Sugar na sasa Namungo FC inaitaka pia saini yake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo FC, Ally Suleiman amesema licha ya kutangaza baadhi ya wachezaji, ila bado kuna wengine wanaoendelea kufanya nao mazungumzo kwa ajili ya kuongeza nguvu na watakapokamilisha watatangaza kikosini.