Kiungo Fei Toto anavyorejea Azam FC
Muktasari:
- Fei Toto amekosa michezo hiyo mitatu ya mwanzo kutokana na adhabu ya kufungiwa kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Simba SC, iliyomalizika kwa Simba kushinda 1-0, Julai 4, 2026.
MSIMU wa Ligi Kuu Bara 2026-2027 umeanza kwa Azam FC kuonyesha inaweza kupata matokeo bila kiungo wake Feisal Salum ‘Fei Toto’, huku takwimu za michezo yake mitatu ya kwanza zikitoa picha tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita alipokuwepo nyota huyo.
Fei Toto amekosa michezo hiyo mitatu ya mwanzo kutokana na adhabu ya kufungiwa kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Simba SC, iliyomalizika kwa Simba kushinda 1-0, Julai 4, 2026.
Katika mchezo huo, Fei Toto alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea vibaya kiungo mshambuliaji wa Simba, Libasse Gueye.
Katika kipindi ambacho Fei Toto hayupo, Azam ilianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania, kabla ya kuifunga TRA United 2-1 na kupata matokeo kama hayo dhidi ya Pamba Jiji.
Kwa ujumla, Azam bila Fei Toto imefunga mabao matano na kuruhusu matatu, ikiwa na wastani wa bao 1.67 kwa mchezo na kuruhusu bao moja kwa kila mchezo.
Abdul Suleiman ‘Sopu’ amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika mwanzo huo, akifunga dhidi ya Polisi Tanzania, TRA United na Pamba Jiji, huku Iddy Seleman ‘Nado’ akifunga bao dhidi ya TRA United, akitengeneza pia dhidi ya Pamba Jiji.
Hata hivyo, picha inabadilika ukirudi nyuma kwenye michezo mitatu ya mwanzo msimu wa 2025-2026, wakati Fei Toto akiwa sehemu ya kikosi, Azam ilianza kwa kuifunga Mbeya City 2-0, kisha ikatoka 1-1 na JKT Tanzania, kabla ya kupata sare nyingine ya 1-1 dhidi ya Namungo.
Hivyo, katika michezo hiyo mitatu, Azam ikiwa na Fei Toto ilikusanya pointi tano, ikifunga mabao manne na kuruhusu mawili.
Kinachompa uzito Fei Toto ni mchango wake wa moja kwa moja kwenye mabao, katika mechi tatu za msimu uliopita, Fei Toto alihusika moja kwa moja kwenye mabao matatu kati ya manne ya Azam sawa na asilimia 75 ya mabao ya timu katika kipindi hicho.
Kwa sasa, Azam bila Fei Toto imeonyesha inaweza kupata matokeo mazuri kupitia mchango wa kikosi kizima, huku kurejea kwa kiungo huyo baada ya kumaliza adhabu yake, safu ya ushambuliaji ya timu hiyo itaongeza nguvu na ubunifu katika kusaka mabao.
Fei Toto amemaliza adhabu yake na leo Ijumaa anaweza kuitumikia timu hiyo wakati Azam ikiwa ugenini kukabiliana na Geita Gold kuanzia saa 12:30 jioni kwenye Uwanja wa Bukombe mkoani Geita.
Kiungo huyo anakwenda kuongeza nguvu kwa kushirikiana na Sopu ambaye tayari ana mabao matatu katika michezo mitatu ya mwanzo.
Pia Nado na Henoc Molia aliyetua msimu huu akiwa tayari ana bao moja, ushirikiano wao unaweza kuifanya safu ya ushambuliaji ya Azam kuwa hatari zaidi wakati huu ambao kocha Florent Ibenge anajaribu kuiweka timu katika hali nzuri ya kuisaka ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu baada ya zaidi ya miaka 10 kupita.