Prime
Kutoka ‘kids’ hadi sokoni kwa mabilioni
HISTORIA inakumbusha enzi zile ambapo mitaa ya Dar es Salaam ilikuwa chujio kuu la kuibua vipaji vya soka nchini.
Hapakuwa na viwanja vya kisasa vya nyasi bandia wala mabweni yenye viyoyozi, lakini kulikuwa na kitu kimoja cha thamani ya kipekee ambacho ni mifumo thabiti ya uzalishaji wa vipaji vya ndani kupitia timu za watoto za Simba Kids, Yanga Kids, na vile vikosi vya pili vilivyojulikana kama Simba B na Yanga B.
Mifumo hii haikuwa tu chemchemi ya burudani, bali ilikuwa ni kiwanda rasmi kilichosokota na kusuka majina makubwa ya wachezaji wazawa nchini.
Walikuwa wachezaji waliokulia ndani ya utamaduni wa klabu hizo, wakijua uzito wa jezi, thamani ya dabi, na kuwa na uzalendo uliotukuka.
Hata hivyo, miaka imeenda na upepo wa mabadiliko ya soka la kisasa umevunja mifumo hiyo ya asili. Leo hii, soka halichezwi tena kwa hisia pekee bali kwa sayansi, mifumo ya kisheria, na mikataba rasmi.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepiga hatua kubwa kwa kuweka kanuni madhubuti zinazolazimisha kila klabu inayoshiriki Ligi Kuu kuwa na timu za vijana za umri wa chini ya miaka 17 (U17) na chini ya miaka 20 (U20).
Azam FC midfielder Feisal “Fei Toto” Salum. PHOTO | COURTESY
Ushindani sasa hivi ni mkubwa na unatia moyo; kwa mfano, hivi karibuni kwenye Ligi ya Vijana ya TFF U17, timu ya Yanga U17 iliibuka mbabe na kutwaa ubingwa, huku mahasimu wao Simba U17 wakifuata kwa karibu katika nafasi za juu.
Mabadiliko haya ya TFF yana faida kimkakati. Mfumo huu unajenga muendelezo ambapo kijana anayecheza klabuni anapata nafasi ya kuchaguliwa katika timu za taifa za vijana kama Serengeti Boys na Ngorongoro Heroes, kabla ya kupanda na kuwa nguzo imara ya timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars.
Kitaalamu na kisayansi, vijana wa sasa wanajengwa vizuri kuliko wa zamani. Wanajua misingi ya mbinu za uwanjani, wanapimwa afya mara kwa mara, na wanalelewa kwa kufuata misingi inayotambuliwa duniani kote na mashirikisho makubwa kama CAF na FIFA.
Lakini, hapa ndipo gari linapomwaga mboga. Licha ya uzuri wa mfumo huu wa kisayansi, kuna ugonjwa sugu unaotafuna vilabu kama vile ukosefu wa subira na ustahimilivu.
Vilabu vingi vya Ligi Kuu bado vinazitazama timu hizi za vijana kama “mzigo wa kisheria” au jambo la kufanya ili tu kukidhi vigezo vya kupata leseni ya klabu.
Viongozi na makocha wengi hawana ujasiri wa kuwaamini na kuwapandisha vijana wanaomaliza muda wao katika kikosi cha U20 kwenda kikosi cha kwanza.
Matokeo yake, vipaji vingi vyenye uwezo mkubwa vinaishia kuachwa huru au kuuzwa kwenye timu ndogo ambazo nazo hazina miundo mbinu ya kuwaendeleza, huku klabu kubwa zikibaki yatima wa vipaji vyao wenyewe.
Kufa kwa ule utamaduni wa kulea na kukosekana kwa imani kwa vijana wa ndani kumesababisha Simba na Yanga kuingia kwenye mtego mkubwa wa kiuchumi.
Ili kukidhi kiu ya mashabiki inayochochewa na shinikizo kubwa la kutaka matokeo ya haraka, vikombe vya ndani, na mafanikio kwenye michuano ya kimataifa ya CAF, vilabu hivi sasa vinalazimika kuingia sokoni kwa nguvu kubwa ya kifedha.
Taarifa na ripoti mbalimbali za kifedha zinaonyesha kuwa miamba hii miwili sasa inatenga kati ya Sh4 bilioni hadi Sh6 bilioni kila msimu kwa ajili ya usajili na uendeshaji wa vikosi vya kwanza.
Kiasi hiki kikubwa cha fedha kinatumika kulipia ada za usajili na mishahara minono ya wachezaji wa kigeni ambao tayari wameiva kutoka nchi kama DR Congo, Ivory Coast, Ghana, na kwingineko.
Athari za kiuchumi haziiishii kwenye ada za usajili pekee, mchezaji wa kigeni anakuja na mzigo mkubwa wa ziada.
Klabu inalazimika kutoa tiketi za ndege za daraja la kwanza, kuwapatia nyumba za kifahari za kuishi, magari ya kutembelea, na kulipia vibali vya kazi na makazi nchini ambavyo kwa taratibu za kisheria zinazohusisha TFF na Idara ya Uhamiaji, vinagharimu mamilioni ya shilingi kwa kila mchezaji, takriban Sh11 milioni.
Tukipiga hesabu za haraka za kiuchumi, mabilioni haya yanayoteketea kila msimu kununua wachezaji waliokomaa kutoka nje, yangeweza kufanya mapinduzi kama yangewekezwa nyumbani.
Fedha hizo zingetosha kujenga akademi za kisasa zenye viwanja vya kiwango cha juu, vifaa vya kisasa vya mazoezi, na kuajiri makocha wabobezi wa makuzi ya vijana.
Hili lingewezesha vilabu vyetu sio tu kujitegemea kwa wachezaji wazawa wenye viwango vya juu, bali pia kugeuza soka kuwa biashara kwa kuuza wachezaji hao kwenda ligi kubwa za Ulaya na uarabuni.
Kimsingi soka la Tanzania lipo kwenye njia panda. Leo hii, tuna mfumo mzuri wa TFF wa U17 na U20 unaofuata misingi ya kisayansi, lakini unakwazwa na tamaa ya matokeo ya haraka na uwekezaji mkubwa wa fedha kwenye majina ya kigeni.
Ili soka letu liendelee kwa usalama kiuchumi na kiufundi, ni lazima viongozi wa vilabu wabadili mtazamo: timu za vijana zisiwe sehemu ya kukamilisha sheria, bali ziwe mradi mkuu wa kimkakati wa uwekezaji wa baadaye.