Kisa Simba, Nabi atimua Haruna, Lamine
MWANASPOTI linajua kwamba Kocha Nabi Mohammed wa Yanga, amewaambia viongozi jana kwamba Haruna Niyonzima na Lamine Moro hataki kuwaona kambini kuelekea mechi ya Jumamosi dhidi ya Simba.
Nabi amefanya maamuzi hayo magumu baada ya wachezaji hao kuchelewa kuripoti kambini huku kiufundi wakiwa wamepoteza pia namba kwenye kikosi cha kwanza hivikaribuni.
Mbali na hao pia Mwanaspoti linajua kwamba Nabi amewaondoa Michael Sarpong kwa sababu za kinidhamu na Balama Mapinduzi, Yassin Mustafa ambao ni majeruhi.
Habari za uhakika zinasema kwamba Yanga walirejea kambini Jumatatu lakini Haruna na Lamine hawakurejea na hakukuwa na sababu mpaka jana alipowaambia viongozi kwamba hataki kuwasikia watu hao wala sababu zao zozote walizonazo.
Licha ya viongozi wa Yanga kukwepa kulitolea ufafanuzi sakata hilo, Mwanaspoti limejiridhisha pia amewaambia hata wakiweza wafanye uamuzi wa zaidi ya mechi hiyo kwani hawapo tena kwenye programu yake. Mwanaspoti linajua kwamba Nabi atawatema mastaa wa kigeni kwenye usajili ujao akiwemo Haruna, Lamine, Sarpong, Fiston Abdulrazak,Carlihnos ambaye ameshasepa na kipa Mkenya, Faroukh Shikalo.
Katika hatua nyingine, jana kulikuwa na kikao kizito cha viongozi wa matawi kwenye makao makuu ya Yanga Jangwani ili kuweka sawa ishu ya mechi ya watani.
Mwanaspoti lilishuhudia viongozi hao wakiingia Jangwani na kukaa hadi usiku wakijadiliana jinsi ya kuushinda mchezo huo muhimu huku wengi wao wakionekana kuwa na sura za furaha na walipotoka walikuwa wakipiga simu kwenye maeneo mbalimbali ishara ya kupeana majukumu.
MZEE MPILI AUNGURUMA
Mmoja wa Wanachama mahiri wa Yanga kutoka Ikwiriri, Mzee Mpili amekiri kuyafurahia yote yaliyotokana na mkutano mkuu wa wikiendi iliyopita huku akisisitiza kuna mambo makubwa na mazuri yanakuja mbele kwenye kikosi hicho kuanzia sasa.
Mzee Mpili ambaye alinukuliwa hivikaribuni akiupinga mchezo wa watani wa jadi, amesema;
“Naomba dua kila kitu kiende vizuri, tunataka tufanye mabadiliko makubwa ndani ya timu na tusonge mbele. Hivyo tunahitaji kusajili na tunawaombea wadhamini wetu mungu awape nguvu kila kitu kiende sawa na tupate nguvu mpya,” alisema.