Kipre akunjua moyo kwa Fei Toto

Muktasari:
- Kipre aliyeitumikia Azam kwa misimu miwili na kuweka rekodi ya kufunga mabao 12, aliondoka na kutimkia MC Alger ya Al geria msimu huu ambako ndiko anakipiga kwa sasa.
WAKATI msimu ukimalizika, staa wa zamani wa Azam FC, Kipre Junior ameweka wazi jina la kiungo mwenzake aliyemkosha zaidi msimu huu na kupiku rekodi yake, akimtaja Feisal Salum.
Kipre aliyeitumikia Azam kwa misimu miwili na kuweka rekodi ya kufunga mabao 12, aliondoka na kutimkia MC Alger ya Al geria msimu huu ambako ndiko anakipiga kwa sasa.
Muivory Coast huyo alicheza na Fei msimu mmoja, huku Mzanzibar huyo akiongoza kwa kufunga mabao 19, yeye akiwaburuza kwa asisti akiwa nazo tisa.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu Kipre alisema, anampongeza kiungo huyo kwa kutendea haki nafasi aliyomuachia ndani ya klabu hiyo.
Alisema kuwa Fei anastahili mafanikio hayo kwa kuwa ni mmoja kati ya viungo bora ambao amewahi kucheza nao alipokuwa Tanzania na uwezo wake ni mkubwa sana.
“Fei ni kiungo akiyekamilika ambaye sio tu ana uwezo wa kutoa asisti ila hata kufunga, natamani siku moja nicheze naye tena, kwa sababu kazi inakuwa nyepesi uwanjani,” alisema Kipre Jr na kuongeza;
“Jambo zuri jingine ni hatua ya Fei kuchukua tuzo hiyo na kuiheshimisha timu yao kwa kuibakiza tuzo hiyo Chamazi, licha kwamba haijabeba ubingwa ila ni wazi ina mastaa bora.”
Azam imemaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 63.