Kinachoendelea Yanga Day, mastaa wa zamani watuma salamu
Muktasari:
- Tamasha la Yanga Day lililoanzishwa mwaka 2019, leo Agosti 9, 2026 linafanyika kwa mara ya nane.
SHUGHULI mbalimbali bado zinaendelea hapa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam katika kilele cha tamasha la Yanga Day linalofanywa na klabu ya Yanga, huku mashabiki wakionekana wanaendelea kufika eneo la tukio taratibu.
Tamasha la Yanga Day lililoanzishwa mwaka 2019, leo Agosti 9, 2026 linafanyika kwa mara ya nane.
Mwanaspoti lipo Uwanja wa Uhuru kukuletea kinachoendelea uwanjani hapo, kuna baadhi ya wanaopiga picha za kumbukumbu kufika eneo hilo, lakini pia Jeshi la Polisi likiendelea kuimarisha usalama.
Ukiachana na hilo, Mwanaspoti limezungumza na baadhi ya mastaa wa zamani wa Yanga, waliozungumzia kuhusiana na tamasha hilo.
Beki wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Shaibu 'Ninja' amesema: "Yanga ni familia, najua furaha ya kutambulishwa mbele ya mashabiki, hivyo nawatakia furaha njema mashabiki na wachezaji."
Mwingine aliyechangia hilo ni beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Kelvin Yondani amesema: "Ni kitu kizuri wachezaji wanapokutana na mashabiki wao kabla ya kuanza kwa msimu, hivyo niwatakie kila lenye heri."
Ukiachana na wachezaji hao waliowahi kuichezea Yanga, msanii wa filamu anayejulikana kwa jina la Dorah ambaye ni shabiki lialia wa Wanajangwani, amesema: "Natarajia kuona burudani mbalimbali kutokana kwa wasanii pamoja na wachezaji wapya, iwe uwanjani ama kuangalia TV."