Kina Barka Seif wanaandaliwa Masaki
Muktasari:
- Mbaraka ambaye pia ni kocha wa Masala Princess, amesema mashindano hayo yanayofanyika kwa siku tano katika viwanja vya Starlight Masaki, Dar es Salaam, yanalenga kukuza vipaji vya wavulana katika makundi ya umri wa chini ya miaka 9, 11, 13 na 15.
MSIMAMIZI wa mashindano ya Icon Cup, Mbwana Mbaraka amesema wameanzisha michuano hiyo kwa lengo la kuwapa vijana nafasi ya kucheza mechi nyingi na kupata uzoefu utakaosaidia kujenga msingi wa timu bora za taifa za baadaye.
Mbaraka ambaye pia ni kocha wa Masala Princess, amesema mashindano hayo yanayofanyika kwa siku tano katika viwanja vya Starlight Masaki, Dar es Salaam, yanalenga kukuza vipaji vya wavulana katika makundi ya umri wa chini ya miaka 9, 11, 13 na 15.
Amesema wakati Tanzania ikiendelea na maandalizi ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027, ni muhimu kuwekeza pia katika soka la vijana ili kuwa na kizazi kitakachoweza kulinda na kuendeleza mafanikio ya soka nchini.
Mbaraka aliwahi pia kuwafundisha baadhi ya vipaji kama Barka Seif anayefanya vizuri katika akademi ya La Masia na ligi ya vijana, Hispania.
“Mashindano haya tumeanzisha ili vijana wapate mechi nyingi na uzoefu. Tukiangalia sasa hivi Tanzania tunaandaa AFCON, tumeona tuandae haya ili baadaye tuweze kupata timu za taifa bora,” amesema Mbaraka.
Ameongeza baada ya mashindano hayo wana mpango wa kuanzisha ligi ya vijana katika makundi hayo ya umri ili kuwapa nafasi maskauti na makocha wa timu za taifa kuwafuatilia wachezaji.
Kuhusu udhibiti wa umri, amesema wanatumia taarifa za shule, madarasa na vyeti vya kuzaliwa, huku akionya kuwa watakaobainika kudanganya wataondolewa kwenye mashindano.
Mwalimu wa makocha kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wame Mkisi amesema “Tuko hapa tumekuja kuangalia vijana na wako vizuri. Unaona kwa sababu ndiyo kwanza wanaanza, huwezi kuona vitu vya ajabu vingi sana, lakini changamoto bado ipo kwenye udanganyifu wa umri. Hakuna haja ya kudanganya kwenye umri mdogo, waacheni watoto wacheze na wafurahie mpira,” amesema Mkisi.