Barka: Siku moja nitakuwa nyota wa Barca
Muktasari:
- Barka, anayekipiga katika akademi hiyo maarufu ya Hispania, amekuwa akivutiwa na wachezaji wanaofanya vizuri na anatamani kupata nafasi ya kukutana nao ana kwa ana, kufanya nao mazoezi au kuzungumza nao.
Kinda wa Tanzania, Barka Seif, amesema anajisikia furaha kuwaona wachezaji wakubwa wanaofanya vizuri Barcelona na anaamini siku moja naye atacheza kwa kiwango hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti baba mzazi wa kinda huyo, Seif Mpanda amesema kiungo huyo mshambuliaji amekuwa akizungumza mara kwa mara tangu ajiunge na akademi hiyo msimu huu.
Barka, anayekipiga katika akademi hiyo maarufu ya Hispania, amekuwa akivutiwa na wachezaji wanaofanya vizuri na anatamani kupata nafasi ya kukutana nao ana kwa ana, kufanya nao mazoezi au kuzungumza nao.
Kwa mujibu wa baba yake, tayari ameshapata nafasi ya kukutana na baadhi ya wachezaji hao akiwemo Karim Adeyemi na Patri Guijarro jambo linalompa hamasa ya kufikia malengo yake. “Anatamani kukutana na wachezaji wote wa Barcelona na ameshakutanao baadhi. Wachezaji wote kama Lamine Yamal, Raphinha wanaocheza vizuri anavutiwa nao,” amesema Mpanda na kuongeza “Ndio alishawahi kuniambia anatamani siku moja afike pale lakini tayari amefanikisha ndoto ya kucheza kwenye akademi anaamini atapata nafasi Barcelona.”
Ameongeza kuwa kiwango anachokionyesha kinda huyo kinawakosha makocha ambao wanaamini kwenye maendeleo yake.
“Tathmini ya makocha wa La Masia kuhusu maendeleo ya Barka wanamtazama kama kijana ambaye atakuja kuwa hatari mbeleni.”
Kabla ya kujiunga na La Masia Juni 2026, Barka alikuwa akiitumikia CF Damm, ambako alionyesha ubora kwa kufunga mabao 41 katika mechi 28 za ligi ya vijana msimu wa 2025/26.
Pia alifunga mabao 18 katika mechi 20 na kuchaguliwa katika kikosi bora cha vijana chini ya miaka 12 cha Catalonia.
Tangu alipojiunga na La Masia, Barka ameendelea kuonyesha uwezo wake, akifunga mabao sita katika mechi tatu za ligi ya vijana.