Barka Seif kwenye njia za Lamine Yamal
Muktasari:
- Mchezo wake wa hivi karibuni katika Ligi ya vijana ya U-13 umekuwa ushahidi mwingine wa mwendelezo huo baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Hospitalet.
UNAWEZA kudhani ndoto, lakini ni uhalisia kuwa kijana kutoka Tanzania yupo kwenye viunga vya akademi ya FC Barcelona maarufu La Masia anakiwasha kweli kweli.
Barka Seif ni balaa jingine katika soka la vijana la Hispania akionyesha kiwango bora kila anapopata nafasi.
Mchezo wake wa hivi karibuni katika Ligi ya vijana ya U-13 umekuwa ushahidi mwingine wa mwendelezo huo baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Hospitalet.
Bao hilo limemfanya afikishe idadi ya mabao 10 na asisti mbili kwenye mechi sita alizocheza. Hiyo ni rekodi inayovutia kwa kijana anayekua katika mazingira ya ushindani mkubwa wa soka la vijana.
NJIA YA LAMINE YAMAL
Baadhi ya mashabiki wameonyesha kuwa na matumaini makubwa na kinda huyo ambaye wanaamini anaweza kuja kuwa kama nyota wa Barcelona, Lamine Yamal anayetamba ulimwenguni kwa sasa.
Hivyo ni kama makuzi ya Barka anapita njia ya nyota huyo wa Barcelona aliyejiunga na akademi ya klabu hiyo akiwa na umri wa miaka saba mwaka 2014, akitokea CF La Torreta. Alipitia makundi mbalimbali ya vijana kabla ya kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza na kucheza mechi yake ya kwanza Aprili 2023 akiwa na miaka 15, miezi tisa na siku 16. Leo ni mmoja wa wachezaji wanaotazamwa kuwa na ushawishi mkubwa katika soka la dunia.
Vivyo hivyo kwa Barka ambaye kabla ya kujiunga na La Masia Juni 2026, Barka alikuwa akiitumikia CF Damm, ambako alionyesha ubora kwa kufunga mabao 41 katika mechi 28 za ligi ya vijana msimu wa 2025/26.
Pia alifunga mabao 18 katika mechi 20 na kuchaguliwa katika kikosi bora cha vijana chini ya miaka 12 cha Catalonia.
Safari hiyo inatoa mfano wa namna La Masia inavyoweza kukuza kipaji cha mtoto hadi kufikia kiwango cha juu.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumzia kuhusu malengo yake Barka amesema "Siku zote nimekuwa na malengo ya kufika mbali na kucheza ligi hii na kuwa kama nyota wa Barcelona naamini siku moja nitafika."