Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kili Queens yaanza vyema, Zanzibar yakiona cha moto

MABAO mawili moja la kila kipindi yametosha kuifanya timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens kuanza vyema michuano ya Kombe la Chalenji 2022 inayofanyikia nchini Uganda, huku ndugu zao Zanzibar wakianza kwa kipigo cha aibu.
Zanzibar iliyocheza mapema mchana wa leo Alhamisi, ilifumuliwa mabao 5-0 na Ethiopia kabla ya Kilimanjaro kuinyoosha Sudan Kusini kwa mabao 2-0, yaliyowekwa kimiani na nahodha Amina Bilal dakika ya 38 na lingine la Diana Lucas aliyefunga dakika za majeruhi.


Michuano hiyo ya sita inayoendeshwa na Baraza la Vyama na Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati inafanyikia kwenye Kituo cha Ufundi cha Chama cha Soka cha Uganda (FUFA) kilichopo mji wa Njeru, ilifunguliwa jana kwa mechi za Kundi kabla ya leo kupigwa mechi za Kundi B.
Katika mechi ya kwanza, Ethiopia iliwasulubu Zanzibar kwa kuwafunga mabao 5-0 yaliyowekwa kimiani na Aregash Tadesse dakika ya pili, Loza Abera aliyefunga mara mbili dakika ya 27 na 55 kabla ya Kidist Zeleke kutupia mengine mawili katika dakika ya73 na 84.
Licha ya Zanzibar kutaka kuepuka aibu kwa kupambana mbele ya Wahabeshi, lakini mambo yalikuwa magumu na kumpa kazi Kocha Abdimutik Haji 'Kiduu' kujipanga kwa mechi yao ijayo dhidi ya Sudan Kusini kabla ya kumalizana na ndugu zao wa Kilimanjaro.
Katika mchezo wa jioni, Kilimanjaro iliyotwaa taji hilo mara mbili, wakiwa ndio vinara ilicheza soka tamu na kuchuana vikali na wapinzani wao kabla ya Amina Bilal kupiga mpira akiwa katikati ya uwanja na kudakwa na kipa wa Sudan Kusini kabkla ya kumponyoka na kutinga wavuni.


Sudan Kusini walionyesha ushindani wa hali ya juu, lakini iliangushwa na uzoefu kulinganisha na Kili Queens ambayo baada ya mabadiliko ya wachezaji katika kipindi cha pili ilizidi kuwakimbiza na kaika dakika za nyongeza, Diana Lucas aligongomea bao la pili na kuipa timu hiyo ushindi murua.
Matokeo hayo yameifanya Kili Queens kushika nafasi ya pili katika kundi hilo nyuma ya Ethiopia kwa tofauti ya uwiano wa mabao, kwani zote zimekusanya pointi tatu na zitarudi uwanjani Jumamosi wikiendi hii kwa kubadilishana wapinzani.
Katika mechi ya ufunguzi wa michuano hiyo zilizochezwa jana Jumatano wenyeji Uganda iliwanyoa majirani zao Rwanda kwa mabao 2-0, Burundi ikiinyoa Djibouti kwa mabao 3-0 kwenye mechi za Kundi A.