Kila bao chini ya VS, kanuni mpya zafichua mamlaka ya mwamuzi
Muktasari:
- Si umeshuhudia mechi za raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu waamuzi wakienda kuangalia ‘screen’ kuweka sawa uamuzi wa baadhi ya matukio yalikuwa na utata? Sasa teknolojia hiyo ndiyo imeanza kazi huku ikionekana kufanya uamuzi sahihi.
KANUNI mpya za Ligi Kuu Tanzania Bara za mwaka 2026 zimeweka utaratibu wa matumizi ya teknolojia ya Video Support System (VS), ikilenga kupunguza utata katika uamuzi wa waamuzi wakati wa michezo.
Si umeshuhudia mechi za raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu waamuzi wakienda kuangalia ‘screen’ kuweka sawa uamuzi wa baadhi ya matukio yalikuwa na utata? Sasa teknolojia hiyo ndiyo imeanza kazi huku ikionekana kufanya uamuzi sahihi.
Kanuni ya 20, yenye vifungu 11, imeainisha namna teknolojia hiyo itakavyotumika, ikiwamo mazingira ambayo timu inaweza kuomba mwamuzi kurejea picha za tukio na muda ambao ombi hilo linapaswa kuwasilishwa.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, VS itatumika kusaidia mwamuzi kujiridhisha kuhusu tukio ambalo uamuzi wake umezua malalamiko kutoka kwa timu wakati mchezo ukiendelea.
Uamuzi unaoweza kuhitaji marejeo ya VS ni pamoja na bao au siyo bao, penalti au siyo penalti, kosa linalostahili kadi nyekundu ya moja kwa moja au kadi ya pili ya njano, pamoja na kumtambua mchezaji aliyefanya kosa endapo kuna malalamiko kuwa mwamuzi amemwadhibu mchezaji asiyehusika.
Hata hivyo, timu haitaruhusiwa kumlazimisha mwamuzi kutumia VS. Kanuni inaeleza kuwa matumizi hayo yatafanyika pale timu inayodhani inaweza kuathirika na uamuzi itakapoomba mwamuzi ajiridhishe kwa kurejea picha za tukio husika.
KOCHA NDIYE MWOMBAJI
Katika utaratibu huo, Kocha Mkuu au kiongozi mwingine wa juu katika benchi la ufundi ndiye mwenye mamlaka ya kuwasilisha ombi la marejeo ya picha kwa VS kupitia mwamuzi wa akiba, maarufu kama fourth official.
Mchezaji akiona kuwa kuna tukio linalohitaji marejeo, hataruhusiwa kwenda moja kwa moja kwa mwamuzi. Badala yake, anatakiwa kumjulisha Kocha Mkuu au kiongozi wa benchi kwa ishara ili kiongozi huyo awasilishe ombi kwa mwamuzi wa akiba.
Kanuni imeweka wazi kuwa ni marufuku kwa mchezaji kumkabili mwamuzi kwa lengo la kuomba au kushinikiza marejeo ya VS. Mchezaji atakayekiuka masharti hayo anaweza kuadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62.
DAKIKA MOJA TU
Moja ya masharti muhimu yaliyowekwa ni muda wa kuwasilisha malalamiko. Timu inayotaka tukio lirejeweshwe kupitia VS inapaswa kufanya hivyo haraka iwezekanavyo ndani ya dakika moja tangu tukio litokee au kabla mwamuzi hajaruhusu mchezo kuendelea baada ya tukio hilo.
Iwapo ombi litawasilishwa baada ya muda huo, mwamuzi wa akiba hataliwasilisha kwa mwamuzi wa mchezo. Mwamuzi pia hatasimamisha mchezo wala kubadili uamuzi wake wa awali kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa nje ya muda uliowekwa.
Pamoja na utaratibu huo, mwamuzi mwenyewe amepewa mamlaka ya kuomba marejeo ya VS hata kama hakuna timu iliyolalamika, endapo atakuwa na mashaka kuhusu tukio fulani na kuona kuwa anahitaji kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua.
MWAMUZI ANA NENO LA MWISHO
Baada ya kupokea ombi, mwamuzi wa akiba atawasiliana na mwamuzi wa mchezo. Ikiwa mchezo utaendelea baada ya tukio linalolalamikiwa, mwamuzi atasimamisha mchezo na kwenda eneo lililowekwa kwa ajili ya VS ili kurejea picha za tukio hilo.
Katika mchakato huo, mwamuzi atasaidiwa na maafisa wa mfumo, akiwamo floor manager wa mrusha matangazo pamoja na ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) aliyepo uwanjani. Watahusika kurejesha picha za tukio kwa kutumia mionekano tofauti ya kamera kadri itakavyowezekana.
Kanuni imeweka pia msingi kwamba uamuzi wa awali wa mwamuzi hautabadilishwa isipokuwa ithibitike wazi bila utata kuwa uamuzi huo ulikuwa wa makosa. Endapo baada ya kurejea picha bado kutakuwa na utata kuhusu uhalisia wa tukio, uamuzi wa awali utaendelea kubaki.
KILA BAO LITAPITIWA
Katika hatua nyingine muhimu, kanuni imeelekeza kuwa kila baada ya bao kufungwa, mwamuzi wa akiba atafanya marejeo ya tukio hilo kupitia VS ili kubaini kama kulikuwa na kosa kabla ya bao kufungwa.
Iwapo mwamuzi wa akiba ataona kuna tukio lililoweza kuathiri uhalali wa bao, atawasiliana na mwamuzi wa mchezo.
Endapo kutakuwa na tofauti kati ya alichokiona mwamuzi wa mchezo na taarifa kutoka kwa mwamuzi wa akiba, mwamuzi mkuu ndiye atakayefanya marejeo mwenyewe ili kujiridhisha. Uamuzi wake wa mwisho ndio utakaotumika.
VS IKIPATA HITILAFU
Kanuni pia imezingatia uwezekano wa mfumo wa VS kupata hitilafu. Iwapo teknolojia hiyo haitafanya kazi, mchezo utaendelea bila matumizi ya VS.
Katika mazingira hayo, makocha na manahodha wa timu husika wanapaswa kufahamishwa kuhusu hitilafu hiyo kabla ya mchezo kuanza au mara tu hitilafu itakapotokea.
Kwa kuanzishwa kwa utaratibu huo, matumizi ya VS katika Ligi Kuu Tanzania yanatarajiwa kuongeza usahihi wa maamuzi katika matukio muhimu huku yakimpa mwamuzi mamlaka ya mwisho katika kutafsiri tukio na kufanya uamuzi.