Kidawa anahitaji kurudi Bara
Muktasari:
- KVZ imemsajili kiungo huyo akitokea KMC ambapo kabla ya huko alikuwa akiitumikia Mlandege.
KIUNGO wa KVZ, Suleiman Juma Kidawa, amesema kurudi kucheza Ligi Kuu ya Zanzibar sio kwamba amefeli ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, bali ameangalia maslahi binafsi kwani bado zipo timu ambazo zinamuhitaji.
KVZ imemsajili kiungo huyo akitokea KMC ambapo kabla ya huko alikuwa akiitumikia Mlandege.
Amesema, watu wengi wanaamini kuwa amefeli baada ya kucheza nusu msimu ndani ya Ligi Kuu Bara, lakini sio kweli bali vipo vitu ambavyo vimemshawishi kujiunga na KVZ.
“Nimerudi kucheza tena nyumbani, sijafeli, bali nimeangalia maslahi binafsi, nina malengo yangu ndio sababu ya kujiunga na KVZ msimu huu,” amesema.
Kiungo huyo amesema ana nia ya kurudi tena Ligi Kuu Bara na amepanga hivyo kati ya dirisha dogo au kubwa lijalo, hivyo atapambana na kuongeza kiwango chake vizuri kufikia malengo hayo.
Pia, Kidawa amesema Ligi Kuu Bara ina uwekezaji na ushindani mkubwa, hivyo kwa upande wake kama mchezaji anahitaji kurudi kucheza huko kwakuwa alikuwa na uwezo wa kucheza kikosi cha kwanza msimu uliopita.
Kidawa amesema, amepata nafasi ya kujifunza vitu vingi ikiwemo kuboresha uchezaji wake, mbinu na juhudi kwani bila ya kufanya mazoezi kwa bidii ni ngumu kucheza Ligi Kuu Bara kwa sababu unakutana na wachezaji tofauti kutoka mataifa mbalimbali.
Kiungo huyo amesema, kutokana na usajili wa KVZ wanaweza kutetea ubingwa, ndiyo maana wanajiandaa kuhakikisha wanafanikisha hilo.
Mbali na hilo, amewataka mashabiki wa KVZ watarajie mambo mazuri kutoka kwao kwa sababu nia yake ni kuipambania nembo hiyo kuhakikisha wanafanya vizuri katika ligi ya ndani na kimataifa. bania malengo ya timu.