Kibaya atua Polisi Tanzania
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo msimu ujao anakwenda kucheza timu ya tano ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Ihefu (sasa Singida Black Stars) na Mashujaa.
KLABU ya Polisi Tanzania imeendelea kujiimarisha kuelekea msimu ujao wa 2026-2027 baada ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji Japhar Kibaya kwa mkataba wa miaka miwili.
Mshambuliaji huyo msimu ujao anakwenda kucheza timu ya tano ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Ihefu (sasa Singida Black Stars) na Mashujaa.
Moja ya rekodi zake bora ni kufunga mabao 14 kwenye Ligi Kuu Bara, wakati akiitumikia Mtibwa Sugar ndani ya misimu miwili.
Kibaya ametua Polisi Tanzania akiwa mchezaji huru kufuatia kumalizika kwa mkataba wake na Mashujaa FC, hatua iliyompa nafasi ya kujiunga na timu hiyo bila kikwazo chochote.
Usajili wa mshambuliaji huyo unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Polisi Tanzania kuongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji, huku benchi la ufundi likiamini uwezo wake utasaidia timu kufikia malengo iliyojiwekea msimu ujao. Kibaya ameondoka Mashujaa baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa kipindi kilichomjengea uzoefu mkubwa wa kucheza Ligi Kuu Bara, akionyesha uwezo wake wa kufunga mabao na kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.
Sasa mshambuliaji huyo anatarajiwa kuanza ukurasa mpya ndani ya Polisi Tanzania, ambapo atakuwa na jukumu la kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji wakati timu hiyo ikijiandaa kwa msimu mpya wenye ushindani mkubwa baada ya kupanda daraja kutoka Championship.
Mtu wa karibu na Kibaya aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Kibaya ameshasaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Polisi Tanzania, alishamalizana na Mashujaa, hivyo amesajiliwa kama mchezaji huru.”
Kibaya anasifika kwa kuwa mshambuliaji mzawa mwenye uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu pamoja na kutengeneza nafasi, jambo linalomfanya kuwa mchezaji tegemeo kwenye timu yoyote anayojiunga nayo.