Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kawempe Ladies mabingwa CECAFA ikifuzu Ligi ya Mabingwa 

BINGWA Pict

Muktasari:

  • Timu hiyo imebeba taji lake la kwanza baada ya kuipokonya JKT Queens iliyobeba mataji mara nyingi zaidi ikifanya hivyo mwaka 2022 na 2025.

KAWEMPE Muslim Ladies ya Uganda, imefuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake baada ya kutwaa ubingwa wa Kanda ya CECAFA kwa kuifunga Kenya Police Bullets bao 1-0 katika fainali iliyochezwa leo Agosti 31, 2026 kwenye Uwanja wa Kigali Pele, Rwanda.

Timu hiyo imebeba taji lake la kwanza baada ya kuipokonya JKT Queens iliyobeba mataji mara nyingi zaidi ikifanya hivyo mwaka 2022 na 2025.

Ushindi huo uliokuwa wa kusubiri hadi dakika za nyongeza, uliifanya Kawempe Muslim kumaliza kampeni hiyo bila kupoteza mchezo hata mmoja, baada ya kushinda mechi zote nne ilizocheza katika mashindano hayo.

Kipindi cha dakika 90 kilimalizika bila bao, licha ya Kawempe Muslim kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga. Kenya Police Bullets, waliowahi kumaliza nafasi ya pili kwenye mashindano hayo mwaka 2024, walifanikiwa kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Kawempe Muslim iliendelea kusukuma mbele na juhudi zake zikazaa matunda katika dakika ya 100, wakati mshambuliaji Agnes Nabukenya alipofunga bao pekee la mchezo huo. Nabukenya alitumia vizuri mpira uliomfikia ndani ya eneo la hatari na kuukwamisha wavuni.

Baada ya kufungwa, Kenya Police Bullets ilijaribu kuongeza mashambulizi ikisaka bao la kusawazisha ili kupeleka mchezo kwenye mikwaju ya penalti, lakini safu ya ulinzi ya Kawempe Muslim ilisimama imara hadi filimbi ya mwisho na kuipa timu hiyo taji.

Kocha wa Kawempe Muslim, Ayub Khalifa Kiyingi, amesifu juhudi za wachezaji wa kikosi chake baada ya mchezo huo, akisema ushindi huo umetokana na kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi chote cha mashindano.

Nabukenya ambaye ni nahodha wa Kawempe Muslim na shujaa wa fainali baada ya kufunga bao pekee, amewapongeza wachezaji wenzake kwa kujituma hadi kufikia hatua hiyo, huku akisisitiza kuwa ushindi huo umetokana na nguvu ya timu nzima.

Katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu, Commercial Bank of Ethiopia (CBE) imeibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Yei Joint Stars ya Sudan Kusini. 

Etsegenet Girma aliipa CBE bao la kwanza dakika ya 34 kabla ya Moureen Nankinga kusawazisha dakika tatu baadaye, lakini Beshadu Tadese akaifungia CBE bao la pili kabla ya mapumziko. 

Kipindi cha pili, CBE iliongeza mabao kupitia Mahelet Bekel, Emush Dandamo, Mihiret Ayele na Rediet Matios na kukamilisha ushindi wa 6-1.