Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kenya Police, Kawempe fainali ya kisasi, historia CECAFA

CECAFA Pict

Muktasari:

  • Hii si fainali ya kawaida, kwani inawakutanisha timu mbili ambazo tayari zimeonyesha kuwa zina uwezo mkubwa, lakini zikiwa na historia tofauti katika mashindano haya.

NI Kenya Police Bullets au Kawempe Muslim Ladies ya Uganda ndio zitakazominyana leo Agosti 31, katika fainali ya kuwania tiketi ya kuiwakilisha CECAFA kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa ya Wanawake Afrika.

Hii si fainali ya kawaida, kwani inawakutanisha timu mbili ambazo tayari zimeonyesha kuwa zina uwezo mkubwa, lakini zikiwa na historia tofauti katika mashindano haya.

Kwa Kenya Police Bullets, hii ni nafasi ya tatu mfululizo kufika hatua za juu za mashindano haya. Wakenya hao walimaliza wakiwa washindi wa pili mwaka 2024 na nafasi ya tatu mwaka 2025, hivyo fainali ya mwaka huu ni nafasi yao ya kurekebisha makosa ya misimu iliyopita.  Zaidi ya hapo, wameingia kwenye fainali wakiwa mabingwa wa Kenya kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Kenya FKF.

Kocha wa Police Bullets, David Bujego Rangon ameeleza kabla ya nusu fainali kwamba wamejaribu na kushindwa hapo nyuma, lakini msimu huu wamejiandaa kwenda mpaka mwisho. Kauli hiyo sasa ina maana kubwa zaidi kwa sababu wamefika kwenye mchezo mmoja unaoweza kuwapa kile walichokikosa mwaka 2024 na 2025.

CECA 01

NJIA YAO HADI FAINALI

Katika hatua ya makundi waliifunga Simba Queens ya Tanzania 2-1, kisha wakaifunga FC Ujeco ya Burundi 3-1 na baadaye wakaichapa Yei Joint Stars ya Sudan Kusini 5-0 kwenye nusu fainali. Hii inaonyesha kwamba Police wana uwezo wa kushinda mechi za presha, lakini pia wana silaha tofauti za kufungua ulinzi wa wapinzani.

Miongoni mwa majina yanayoweza kuamua fainali upande wa Police ni Martha Amunyoletelo, ambaye tayari ameonyesha kiwango bora kwenye mashindano haya. Alifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya FC Ujeco.

Katika nusu fainali dhidi ya Yei, Police walifunga mabao matano, huku Tereza Obuny, Martha O. Lorna Nyabuto na Rebecca Okwaro wakiwa miongoni mwa wafungaji. Hivyo, tatizo kwa Kawempe si mchezaji mmoja tu, bali namna ya kuzuia mfumo mzima wa mashambulizi wa Wakenya.

CECA 02

KAWEMPE

Upande wa pili kuna Kawempe Muslim Ladies, mabingwa wa Uganda ambao wanaingia kwenye fainali wakiwa na historia ya kuvutia.

Walicheza mara yao ya kwanza kwenye mashindano haya mwaka 2024, na tangu wakati huo wameendelea kujijenga. Mwaka huo walifika hatua ya mtoano, kabla ya kuondolewa na Commercial Bank of Ethiopia walionyesha uwezo mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuichapa FAD ya Djibouti 10-0, huku Hadija Nandago akifunga mabao matano peke yake.

Msimu huu Kawempe imeingia kwenye mashindano ikiwa bingwa wa Uganda baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu kwa msimu wa 2025/26 kwa pointi 52, moja mbele ya She Corporate.

Kikosi hicho kinachoongozwa na kocha Ayub Khalifa Kiyingi kimeonyesha utulivu mkubwa Kigali. Kimeanza kwa kuifunga CBE bao 1-0, kikaichakaza FC Ujeco 8-0, kabla ya kurudia kuifunga CBE 3-0 katika nusu fainali.

Silaha kubwa ya Kawempe ni Jovia Nakagolo, Agnes Nabukenya na Latifah Nakasi,  watatu hao walikuwa tayari wamefunga mabao mawili kila mmoja na walikuwa miongoni mwa wachezaji waliotarajiwa kuamua mchezo.

Nakagolo aliendelea kuthibitisha hilo dhidi ya CBE kwa kufunga bao la kwanza dakika ya 18, wakati Nabukenya alifunga bao la tatu dakika ya 70.

Kuna jambo moja linaloifanya fainali hii kuwa na mvuto zaidi: Kawempe inatafuta historia yake ya kwanza ya kutwaa taji la mashindano haya, wakati Police Bullets inatafuta kubadilisha historia ya kushindwa miaka miwili.

Hivyo mshindi wa fainali hiyo kati ya Police na Kawempe ndiye atakayepata tiketi ya kuiwakilisha kanda hiyo kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa ya Wanawake Afrika  mwaka huu.

CECA 03

FAINALI ITAAMULIWA WAPI?

Kwa upande wa Police Bullets, jambo la kuangaliwa ni kama Martha Amunyoletelo na safu yao ya ushambuliaji itaendelea na kasi waliyoonyesha kwenye hatua za awali. Kwa Kawempe, macho yatakuwa kwa Nakagolo, Nabukenya na Nakasi, huku uwezo wao wa kutengeneza nafasi na kutumia makosa ya ulinzi ukiwa silaha yao kubwa.

Lakini zaidi ya majina hayo, fainali inaweza kuamuliwa na timu itakayoweza kuvumilia presha, kulinda eneo lake la hatari na kutumia nafasi chache itakazopata. Hii ni Kenya dhidi ya Uganda, uzoefu dhidi ya njaa ya historia.