Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CECAFA ibadilishe haya!

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa CECAFA mashindano ya mwaka huu yanashirikisha timu 10 katika makundi matatu. Mfumo huo una timu nne katika Kundi A, huku Kundi B na C zikiwa na timu tatu kila moja. Timu mbili za juu Kundi A zinaingia nusu fainali, sambamba na za kileleni Kundi B na C.

MASHINDANO ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika ukanda wa CECAFA yamekuwa moja maendeleo ya soka la wanawake Afrika Mashariki na Kati. Hata hivyo, mfumo unaotumika si rafiki. Sasa swali ni kweli unatoa ushindani unaostahili kwa ukanda wenye nchi nyingi na vipaji vingi?

Kwa mujibu wa CECAFA mashindano ya mwaka huu yanashirikisha timu 10 katika makundi matatu. Mfumo huo una timu nne katika Kundi A, huku Kundi B na C zikiwa na timu tatu kila moja. Timu mbili za juu Kundi A zinaingia nusu fainali, sambamba na za kileleni Kundi B na C.

Bingwa wa mashindano ndiye anayekata tiketi ya kuiwakilisha CECAFA katika Ligi ya Mabingwa Afrika.


TIMU 10

CECAFA ina vyama vya soka 12, na kwa wanawake kuna nchi zenye ligi zinazozidi kuimarika kama Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Rwanda na Burundi, huku Sudan Kusini, Sudan, Somalia, Djibouti na Zanzibar pia zikiwa sehemu ya mfumo wa mashindano ya ukanda. Kwa hiyo, kukutanisha timu 10 kufuzu Ligi ya Mabingwa kunaweza kuonekana kama kutotumia kikamilifu uwezo wa ukanda huo.

Tatizo kubwa ni mgawanyo wa nafasi za kufuzu. Kundi lenye timu nne linatoa michezo mingi zaidi kuliko makundi yenye timu tatu. Zaidi ya hapo, timu mbili kutoka Kundi A zinaweza kufuzu nusu fainali, wakati timu kutoka Kundi B na C zinahitaji kushinda makundi yao ili kufika hatua hiyo.

Hii inaweka mazingira ambayo thamani ya ushindi wa timu inaweza kuwa tofauti na ya nyingine kutokana na ukubwa wa kundi. 

MFUMO UBADILISHWE

CECAFA inapaswa kubadilisha mfumo, ambapo kila nchi inapaswa kutoa timu moja lakini kilichotokea nchi 10 tu ndizo zinatoa timu moja.

Kila nchi itoe angalau timu mbili, pale ambapo kuna uwezo wa ligi na usajili unaokidhi vigezo vya mashindano. Mfano Tanzania zingeangaliwa timu zilizomaliza nafasi mbili za juu ambazo ni Simba Queens na JKT Queens, vivyo hivyo kwa Kenya, Police Kenya na Vihiga. Ikiwa nchi 12 zitashiriki maana yake timu 24 na siyo 12. Hapa ndipo mfumo unaweza kubuniwa kwa hatua mbili ili mashindano yasiwe marefu kupita kiasi.

Hatua ya kwanza inaweza kuwa ya mchujo, ambapo timu kutoka nchi zenye viwango vya chini vya ushindani zianze raundi ya awali. Timu zilizopo juu kwenye viwango zianzie hatua ya makundi.

Njia nyingine rahisi zaidi ni kuwa na timu 12 kila nchi ikitoa timu moja, lakini kuweka msisitizo kwamba CECAFA itoe nafasi nne za ukanda kwenye hatua inayofuata ya CAF.


KWA NINI NAFASI NNE

Kwa nini CECAFA ipewe nafasi moja tu wakati ukanda una idadi kubwa ya vyama na ligi zinazozidi kukua?

Ushindi wa timu moja  unamaanisha timu inaweza kutumia msimu mzima kujenga kikosi, halafu ikaangukia katika mchezo mmoja au miwili na ukanda ukabaki bila uwakilishi mwingine.

Badala yake, timu nne bora zipewe tiketi ya kwenda Ligi ya Mabingwa Afrika.


MAKUNDI YAWE SAWA

Kama CECAFA itaendelea kutumia mfumo wa makundi, jambo la kwanza kurekebisha ni usawa wa makundi. Usiwe na kundi la timu nne na mengine ya timu tatu. Kama ni timu 12, zigawanywe katika makundi manne yenye timu tatu kila moja, au makundi matatu yenye timu nne kila moja. Mfumo bora zaidi ni makundi matatu ya timu nne.

Kila timu icheze mechi tatu. Washindi wa makundi matatu pamoja na timu bora iliyomaliza nafasi ya pili waingie nusu fainali. Kutoka hapo, washindi wa nusu fainali waende fainali, huku timu mbili zilizofika nusu fainali lakini zikashindwa zipate nafasi katika mfumo wa kufuzu kulingana na kanuni zitakazowekwa. Lakini kama lengo ni kupata timu nne, mfumo mwingine unaweza kuwa rahisi zaidi: timu mbili bora kutoka kila kundi zifuzu robo fainali, kisha timu nne za nusu fainali zipate tiketi ya CAF. Hapo mashindano yatakuwa na ushindani mkubwa kuanzia hatua ya makundi. CECAFA isibaki kuwa mashindano ya bingwa mmoja.


MTAZAMO

Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake imeendelea kukua, na maeneo mengine yanaonyesha namna mashindano ya kikanda yanavyoweza kutumika kukuza ushindani. Kwa mfano, COSAFA pia ina mashindano yake ya kufuzu mwakilishi wa ukanda katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

CECAFA inapaswa kujiuliza: tunataka kumpata bingwa wa ukanda au tunataka kujenga timu nne zitakazoweza kushindana Afrika?

Jibu likiwa ni kujenga ushindani wa Afrika, basi nafasi moja haitoshi.

Timu kama Simba Queens, JKT Queens, Kenya Police Bullets, Kampala Queens, Commercial Bank of Ethiopia na nyingine zimeonyesha kwamba kuna uwezo mkubwa ndani ya ukanda. CECAFA yenyewe imetaja klabu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Rwanda na Burundi katika mashindano yake.


FEDHA

Marekebisho yasibaki kwenye mfumo wa makundi pekee, bali CECAFA inapaswa kuwa na mfuko maalumu wa mashindano ya wanawake, ambao utasaidia gharama za usafiri, malazi, waamuzi, tiba na maandalizi ya timu. Vilevile, timu zote zipewe muda sawa wa mapumziko. Isitokee timu moja icheze baada ya saa 48 wakati nyingine inapumzika siku tatu au nne.

CECAFA ina nafasi ya kufanya mashindano ya wanawake kuwa makubwa zaidi Afrika. Lakini hilo haliwezi kufikiwa ikiwa mfumo unaendelea kutegemea timu chache na tiketi moja pekee ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wazo la msingi linapaswa kuwa wazi; ongeza ushiriki, sawazisha makundi, ongeza michezo, ongeza nafasi za kufuzu na ongeza uwekezaji.