Katwila: Geita Gold hatujakata tamaa
Muktasari:
- Geita Gold imekuwa katika mwenendo usioridhisha, ikicheza mechi 11, imeshinda mbili, sare tatu na kupoteza sita, huku ikikusanya pointi tisa zinazoiweka nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi.
KOCHA wa Geita Gold, Zuberi Katwila amesema hawajakata tamaa licha ya timu hiyo kupitia kipindi kigumu cha matokeo mabaya Ligi Kuu Bara na kipaumbele chao kwa sasa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji ili warejeshe kujiamini na kuanza kupata ushindi.
Geita Gold imekuwa katika mwenendo usioridhisha, ikicheza mechi 11, imeshinda mbili, sare tatu na kupoteza sita, huku ikikusanya pointi tisa zinazoiweka nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi.
Katika mechi 11 ilizocheza, Geita Gold imefunga mabao 11 na kuruhusu 18, ikiwa na tofauti ya mabao saba hasi. Kwa wastani, timu hiyo inafunga bao moja kwa mchezo huku ikiruhusu mabao 1.6.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katwila amesema pamoja na matokeo hayo, haoni sababu ya kuwalaumu wachezaji wake kwa sababu wanajituma na wanaonesha nia ya kupata ushindi, lakini wanakabiliwa na changamoto ya kutafsiri kiwango wanachokionesha uwanjani kuwa matokeo.
“Bado hatujakata tamaa, tunachotaka kufanya kwa sasa ni kuwajenga wachezaji wetu kisaikolojia. Tunahitaji warudi kwenye hali nzuri ya kujiamini kwa sababu matokeo tunayopata hayafanani na juhudi wanazozionyesha,” amesema Katwila.
“Kuna michezo tunacheza vizuri, tunapambana na kutengeneza nafasi, lakini mwishowe tunakosa matokeo. Hii ni changamoto ya muda tu, tukipata ushindi mmoja naamini mambo yatabadilika na timu itarudi kwenye hali yake.”
Amesema hataki kuwatupia lawama kwa sababu anatambua kiu yao ya kushinda, badala yake benchi la ufundi linatakiwa kutafuta namna ya kuwasaidia kurejesha utulivu na kujiamini.
Changamoto kubwa zaidi imeonekana kwenye safu ya ushambuliaji, ambapo katika michezo sita imeshindwa kufunga bao, ikiwamo vipigo vya mabao 4-0 dhidi ya Pamba Jiji, 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji, 2-0 dhidi ya Simba na 1-0 dhidi ya Yanga.