Kamishna Mafunzo awatuliza mashabiki
Muktasari:
- Mafunzo imeshacheza mechi sita kati ya hizo imetoa sare nne na kufungwa michezo miwili na kukusanya pointi nne huku ikishika nafasi ya 15 ya msimamo wa ligi.
KAMISHNA wa Chuo cha Mafunzo, Kanali Khamis Bakari Khamis, amewatoa hofu mashabiki na wadau wa soka kuhusu mwenendo wa timu hiyo ambayo imekuwa ikipata matokeo mabaya katika Ligi Kuu Zanzibar msimu huu.
Kamishna huyo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Namala Suleiman alipomtembelea ofisini kwake, Kilimani Unguja.
Kanali Khamis amesema anaelewa kwasasa kuwa timu hiyo inakabiliwa na changamoto ya kupata matokeo mazuri katika michezo yake ya hivi karibuni, lakini hawapaswi kukata tamaa.
Kamishna huyo aliwataka mashabiki wa Mafunzo kuendelea kuwa na imani na timu yao huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuendeleza soka
"Nawasihi mashabiki wa Mafunzo msivunjike moyo kwa mwenendo wa timu yetu, hiki ni kipindi cha mpito, tutakaa sawa, endeleeni kutuunga mkono," amesema.
Kamishna amesema ligi imeongezeka thamani na mvuto kutokana na usimamizi mzuri ambapo kwa sasa imekuwa na ushindani kwa kila timu kupambana kuhitaji ubingwa ili kuwakilisha nchi kimataifa.
Vilevile, ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa ZFF huku akiwasihi mashabiki kuhudhuria viwanjani.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa ZFF, Namala Suleiman, amemshukuru Kamishina huyo kwa ushirikiano wake na mapokezi mazuri.
Pia, amesema ZFF itaendelea kuwa wasikifu na kupokea mawazo ya wadau kwa lengo la kujenga misingi imara na endelevu yenye kuipa thamani ligi hiyo.
Aidha, alieleza kupokea ushauri uliotolewa kuhusu namna ya kuboresha na kuendeleza vipaji vya soka Zanzibar, hatua inayolenga kuimarisha maendeleo ya mchezo huo.
Mafunzo imeshacheza mechi sita kati ya hizo imetoa sare nne na kufungwa michezo miwili na kukusanya pointi nne huku ikishika nafasi ya 15 ya msimamo wa ligi.