Kambi ya Kagera Sugar usipime!

Muktasari:
Kambi hiyo ambayo imejitenga ikiwa ni kati ya nyumba chache zilizopo kiwanda cha zamani cha Sukari cha Kagera (Old Kagera Sugar) na kuna umbali fulani hivi kwenda kilipo kiwanda kipya (New Kagera Sugar).
MAJIRA ya mchana wa Jumapili, mwandishi anatinga ndani ya kambi ya timu ya Kagera Sugar iliyopo mjini hapa. Maskani ya kambi hiyo ipo Wilaya ya Misenyi katika Kata ya Nsunga umbali kutoka Bukoba kiasi cha kama kilomita 60.
Kambi hiyo ambayo imejitenga ikiwa ni kati ya nyumba chache zilizopo kiwanda cha zamani cha Sukari cha Kagera (Old Kagera Sugar) na kuna umbali fulani hivi kwenda kilipo kiwanda kipya (New Kagera Sugar).
Jina la kambi yao ni Ngado, lakini wachezaji kwa namna wanavyoielewa wakaibatiza jina la utani la Sobibo wakifanikisha na kambi moja matata ya Venezuela.
MAZINGIRA YA KAMBI
Kambi hiyo imejitenga, ukikitafuta kijiji kilicho karibu na hapo ni kilomita tatu, tena ni nyumba moja hapa nyingine ipo kule, yenyewe imezungukwa na mandhari ya kijani kibichi ambacho kinatengenezwa na miti na mazao ya kulimwa kama mashamba ya miwa, miti ya miembe na migomba.
Utakapokuwa unaingia, kushoto utakiona kiwanda hicho cha zamani ambacho kililipuliwa katika vita ya Idd Amin na kulia kuna uwanja ambao wao hutumia kwa mazoezi yao ya kila siku.
Mazingira ya uwanja wao huo wa mazoezi ni kijani kibichi, haujazungushiwa uzio na pembeni unapambwa na mashamba miwa iliyostawi.
Ratiba yao ya mazoezi ni kila jioni isipokuwa Jumapili kwa kawaida wachezaji hupumzika. Mazoezi yana vipindi viwili asubuhi na jioni, huwa ni kwa vipindi vichache pale wanachokuwa na maandalizi ya msimu napo ni asubuhi kwa juma inaweza kuwa mara mbili au tatu.
Ukitoka uwanjani kwenda ilipo kambi yenyewe ni kama mita 1000.
USIPOULIZA, UNARUDI KAPA
Kwa yeyote anayefika hapo, lazima atingishe kichwa na kukubali kweli hii ndio kambi na kama mchezaji anashindwa kucheza soka katika mazingira hayo, basi ana matatizo binafsi.
Kwanza utakutana na nyumba chache zinazoonekana hapo na mojawapo ni Meneja Mkuu, Mohamed Hussein na Kocha Mkuu, Mecky Maxime.
Ebwana meneja huyo ni mfugaji! Nyuma ya nyumba yake imezungukwa na mabanda ya kufugia mbuzi, kuku, kanga na bata. Ana mbuzi kama 175 hivi ambao huwatumia kwa ajili ya mboga na biashara.
Mwandishi alipokuwa anaingia, alimkuta meneja huyo kwenye vichaka akijiokotea mayai ya kanga ambao huyakimbia mabanda na kutagia porini.
Mwenyewe anasema, hakuwa anajua chaka hilo kwa sababu ya safari zake za mikoani na timu, hivyo ikawa kama zali kupagundua na kuokoa mayai hayo.
Yeye alikuwa ameketi barazani akipunga upepo ndipo akawaona kanga wanaingia katika chaka hilo kwa kasi na kutulia kwa muda, walipotoka alienda kuangalia si ndiyo akakuta mayai.
Lakini wakati wote huo, unakuwa hujaifikia kambi wanayoishi wachezaji wenyewe yaani Sobibo Camp na mwandishi alipouliza jamaa wapo wapi, akaonyeshwa mlimani usipoelekezwa hufiki, huko ndipo kwenye raha kamili.
Kambi hii kwa wale wazee wa starehe, huwezi kupata muda wa kwenda kuponda raha, ukiingia umeingia na akili yao inakuwa wao na mpira tu.
NDANI YA SOBIBO CAMP
Basi hapo ndipo mwandishi akakabidhiwa nahodha wa timu, George Kavila aliyeshuka kilimani baada ya kupigiwa simu kwa maelekezo hayo.
Kambi hiyo imewahi kutumiwa na wachezaji kadhaa nyota kama, Mrisho Ngassa, Mganda Michael Katende, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na wengine.
Ndipo walimo baadhi ya nyota kama Juma Jabu, Geofrey Taita, Danny Mrwanda, Hussein Sharrif ‘Casillas’ na Paul Ngwai wanaoichezea Kagera Sugar.
Kupanda kilimani hapo kama hauko fiti, utachemka na huko ndiko unakutana na nyumba moja kubwa iliyojitenga pembeni ikiwa imezungukwa na miti na mawe makubwa wenyewe wanasema, wakati mwingine nyoka huwa wanawatembelea.
Ndani ina vyumba vya kulala kama nane, sehemu ya chakula na mapumziko ambapo kuna televisheni moja kubwa wanayoitumia kwa ajili ya kuangalia mpira na taarifa mbalimbali kama habari na muziki.
Kabla hujaingia jikoni kunapoandaliwa msosi, pembeni kuna dispensa kubwa ya maji ambayo wachezaji wanapohitaji maji ya kunywa ni kitendo cha kwenda kufungua na kunywa, pia kuna friji kubwa inayotumika kuhifadhi vyakula kama mboga na mambo mengine.
Vyumba vinavyotumiwa na wachezaji ni vikubwa na vina hewa ya kutosha vingine wanaishi wachezaji wawili hadi wanne.
Wenyewe wanaishi kama nyumbani tu, utakuta wengine wapo juu ya mawe wanapiga stori, wengine wamejilaza ni hivyo yaani.
Hata hivyo, wakati wa tetemeko la ardhi lilipotokea, wachezaji hawakuwapo kambini, ila limeathiri baadhi ya sehemu katika nyumba hizo kwa kuacha ufa ikiwemo nyumba ya meneja.
Muda wote tulipokuwa tunatembea, mkononi Kavila alikuwa ameshika spika moja kubwa ambayo ilikuwa inapiga muziki mkubwa wajanja wa mjini wanasema, muziki mnene.
Kumbe bwana, spika hiyo ina kifaa maalumu (blue tooth) akiwa ameunganisha kwenye moja ya simu zake ili kupata burudani hiyo maisha yanaendelea.
Siku hiyo ilikuwa ni ya pili baada ya kufungwa mabao 6-2 na Yanga, wachezaji hawakuwa na amani sana, lakini mazingira ndiyo yaliyowafanya waonekane kama wenye amani.
Kavila anaichezea klabu hiyo kwa zaidi ya miaka tisa anasema: “Maisha ya hapa ni mazuri na tunaishi kwa amani kama tuko nyumbani, kambi hii huwa inawashinda wale wachezaji wenye mambo mengi, lakini ukija hapa kwa moja la kucheza mpira ni rahisi na unafanikiwa.”
MAMA PAULINA KIBOKO
Kwa mchezaji yeyote aliyewahi kuichezea Kagera Sugar, lazima atamfahamu Mama Paulina. Kwani ndiyo mpishi maarufu wa klabu hiyo tangu ilipopanda daraja mwaka 2004 na wachezaji waliopo sasa, wanamsifu kwa kupika vinono na kipimo chenye kueleweka.
Mama Paulina anafafanua ratiba ya msosi hapo kambini anasema: “Niko hapa tangu Kagera ilipopanda daraja, wachezaji wote waliopita hapa nimewapikia na naishi nao vizuri vijana wangu. Ratiba ya chakula cha hapa ni asubuhi, mchana na usiku na inategemea na aina ya kitakacholiwa siku hiyo.”
“Kwa kawaida asubuhi huwa inategemea, chai kwa chapati, maandazi na mayai, mchana ni wali au ugali na kitoweo cha samaki au nyama, mboga za majani, maharagwe na matunda na usiku ni hivyo, inaweza kuwa ndizi, ugali au wali na mboga ya samaki au nyama, mboga za majani, maharagwe na matunda, wakati mwingine ni pilau,” anasema Mama Paulina.
MALENGO YA TIMU
Akizungumzia kikosi chake, Meneja Mohamed Hussein anasema: “Hatuna wasiwasi kama ulivyowaona wachezaji hawana shida, wao ni kazi tu na hakuna mambo mengine.”
Kwa upande wa Kocha Maxime anayekinoa kikosi akitokea Mtibwa Sugar anasema: “Maisha ya hapa Kagera ni mazuri na hakuna usumbufu, utofauti na ubora wa kambi hii tangu nilipofika ni mazingira kwani kwa mchezaji anayekuja kwa lengo la kucheza soka lazima atafanikiwa.”
“Kama unavyoona hakuna mambo ya starehe, yule anayetaka mambo hayo lazima asafiri umbali mrefu zaidi ya kilomita 3-6, hivyo ni mazingira rafiki kwa wachezaji.”
Akizungumzia malengo yake msimu huu wa Ligi Kuu, Maxime anasema anataka kufanya vizuri na kuwamo katika nne bora.
“Malengo timu ifanye vizuri na tumalize katika nafasi nne za juu, ila kikosi hiki nitakifanyia marekebisho kwa kuongeza baadhi ya wachezaji katika dirisha dogo, nitafanikiwa tu, kwani hata mazingira yanaruhusu kufanya vizuri.”