Kama Messi, Ronaldo naye akosa penalti
Muktasari:
TOLEO lililopita, mwandishi Luca Caioli alizungumzia tukio la Messi kukosa penaltI katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea hali iliyomfanya mchezaji huyo atoke uwanjani akiwa ameficha sura yake kwa kutumia jezi. Sasa endelea….
TOLEO lililopita, mwandishi Luca Caioli alizungumzia tukio la Messi kukosa penaltI katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea hali iliyomfanya mchezaji huyo atoke uwanjani akiwa ameficha sura yake kwa kutumia jezi. Sasa endelea….
Kipa wa Chelsea, Petr Cech akatanua mikono yake tayari kukabiliana na mkwaju wa penalti. Messi alionekana kuwa na sura ya umakini, akafumua shuti, Cech akaruka upande wa kushoto lakini shuti la Messi lilikwenda juu kidogo na mpira ukagonga mwamba na kurudi uwanjani.
Ni pigo kubwa kwa Messi na Barca, filimbi ya kumaliza mchezo ilipopulizwa, Messi akaficha sura yake akitumia jezi, ulikuwa usiku wa hovyo kwake, haikujalisha kwamba alikuwa ndiye mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mwaka wa nne mfululizo akiifikia rekodi ya Gerd Muller ya miaka ya 1970.
Taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya lilimponyoka na ikawa hivyo hivyo kwa La Liga, ilikuwa zamu ya Ronaldo kubeba taji hilo, Nou Camp alipoiwezesha Real kuibuka vinara huku akiwa kivutio kwa soka la maana.
Ronaldo aliifungia Real bao la pili na kufanya ubao usomeke 2-1 na hapo kwa mara ya kwanza akalifurahia taji la La Liga. “Furaha iliyoje, nina furaha isiyo kifani, mashabiki wana haki ya kupata taji hili.” Alisema Ronaldo baadaye katika sherehe ya kufurahia ubingwa iliyofanyika katika ukumbi wa Plaza de Cibeles mjini Madrid.
Hata hivyo siku kama nne hivi baada ya kubeba taji la La Liga na ushindi wao dhidi ya Barca, mafanikio hayo yakapotea, pamoja na kuifungia Madrid mabao mawili katika mechi ya pili ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, mechi hiyo ilikwenda kwenye mikwaju ya penalti na kama ilivyokuwa kwa Messi, Ronaldo akakosa penalti yake.
Ilikuwa pigo kubwa kwa Ronaldo kukosa penalti katika hatua hiyo muhimu ambayo kama angepata ingeweza kuipeleka Real katika hatua nyingine, lakini tofauti na Messi, Ronaldo akaweka alama yake katika mechi hiyo ya dakika 120.
Alifunga kwa penalti katika dakika ya sita na kufunga bao jingine katika dakika ya 10 na kuifanya Real iwe mbele kwa mabao 2-0 kabla Robben hajaipatia Bayern bao pekee na kufanya matokeo yasomeke 2-1.
Juhudi za Ronaldo na wenzake kusaka bao jingine hasa baada ya mechi ya kwanza kulala ugenini kwa mabao 2-1 hazikuzaa matunda na ndipo timu zilipokwenda kwenye penalti na Real ikakwamia katika hatua hiyo.
Mbali na Ronaldo wengine wa Real waliokosa penalti zao katika mechi hiyo ya nyumbani ni Kaka na Sergio Ramos. Wakati kwa Bayern waliopata ni Alaba, Gomez na Schweinsteiger.
2012-13
Ronaldo aliuanza kinyonge msimu mpya wa 2012-13, licha ya kuifunga Barca katika Spanish Super Cup Agosti 2012, na kuwa mchezaji pekee kufunga katika El Clasico sita mfululizo, hakufurahia goli lake.
Baadaye waandishi wa habari wakamuuliza ni kwa nini hakufurahia, naye akawajibu katika namna ya kushangaza kidogo, “Inawezekana ni kwa sababu nina huzuni kidogo, sishangilii magoli kwa sababu sina raha.” Ronaldo alikataa kufafanua zaidi kuhusu kauli yake hiyo, na uvumi nao ukachukua nafasi yake, Je ni mkakati wake wa kutaka kuongezewa mshahara? Je anataka kuhama? Au alikuwa akitaka apendwe zaidi katika klabu hiyo?
Hatimaye mwisho wa msimu, Florentino Perez akazungumzia anavyoliona tukio hilo. Katika mahojiano yake na kituo kimoja cha redio Perez, Rais wa klabu ya Real Madrid akatoa ufafanuzi wake.
“Cristiano ameniambia hana raha na nikamwambia kwamba tunafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anakuwa na furaha, kwa sababu yeye ni mchezaji bora duniani sijui kama ana ofa Paris Saint Germain.“
Amepitia kipindi kigumu, hakuna zaidi, na baadaye kiwango chake kimekuwa vizuri.”
Itaendelea Jumamosi…