Josiah hana haraka na Mkude
Muktasari:
- Mkude ambaye aliwahi kuichezea Simba, Yanga amekaa nje kwa msimu mzima tangu atoke kwa Wanajangwani hao msimu wa 2024/25, mpaka aliposajiliwa tena 2026/27 ndani ya kikosi cha Mashujaa FC.
BAADA ya kukaa nje kwa muda mrefu, mashabiki wanaosubiri kumuona Jonas Mkude akirejea uwanjani watalazimika kusubiri zaidi, baada ya kocha Aman Josiah wa Mashujaa kusema hana mpango wa kumharakisha kiungo huyo.
Mkude ambaye aliwahi kuichezea Simba, Yanga amekaa nje kwa msimu mzima tangu atoke kwa Wanajangwani hao msimu wa 2024/25, mpaka aliposajiliwa tena 2026/27 ndani ya kikosi cha Mashujaa FC.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha huyo alisema haoni sababu ya kumrudisha Mkude kwenye ushindani kwa presha ya kutaka kumuona uwanjani mapema, akisisitiza kuwa muhimu zaidi ni kuhakikisha mchezaji huyo anarudi akiwa tayari kimwili na kiakili.
“Hatuna sababu ya kumharakisha Mkude. Amekuwa nje kwa muda mrefu, kwa hiyo tunataka kumpa muda wa kutosha ili arudi vizuri. Tunataka kulinda hadhi yake na kuhakikisha akirudi anaweza kucheza katika kiwango ambacho watu wanamfahamu,” alisema Josiah.
Josiah alisema, Mkude si mchezaji ambaye anapaswa kurudishwa uwanjani kwa sababu tu amekuwa akifanya mazoezi. Baada ya muda mrefu bila kucheza, anahitaji kujenga tena utimamu wa mwili, kasi ya mchezo na kujiamini kabla ya kuingia kwenye ushindani wa mechi rasmi.
“Tunataka arudi akiwa tayari kabisa. Hatutaki acheze kwa sababu tu watu wanataka kumuona.Tunataka akirudi awe na uwezo wa kutoa kile tunachokijua kutoka kwake,” alisema.
Kocha aliongeza kuwa uzoefu wake ndio unaofanya benchi la ufundi kuwa makini zaidi na mchakato wa kurejea kwake, badala ya kumtupa moja kwa moja kwenye presha ya ushindani.
“Nataka siku Mkude atakaporejea uwanjani iwe mwanzo wa sura mpya yenye kiwango kizuri, badala ya kurejea mapema na kushindwa kuonyesha uwezo wake kutokana na kutokuwa tayari kikamilifu.”
Mkude amekuwa mmoja wa viungo wenye uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania akiwa alitokea kwenye timu ya vijana ya Simba na kuitumikia timu ya wakubwa kwa zaidi ya miaka 12, akatua Yanga lakini hakupata nafasi ya kutosha kwenye timu hiyo. Mashabiki wamekuwa wakimsubiri kwa hamu kubwa kutokana na ubora ambao aliwahi kuuonyesha huko nyuma.