JKT Tanzania kuichalenji Azam FC nafasi ya tatu?
Muktasari:
- Katika msimamo wa ligi hiyo, Azam FC ipo nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi tisa, imeshinda sita, sare mbili, imepoteza moja, ina pointi 20, wakati JKT Tanzania ipo nafasi ya nne, imecheza mechi 10, imeshinda tano, sare mbili, imepoteza tatu, ina pointi 17.
KAMA JKT Tanzania ikishinda mechi dhidi ya Azam FC iliyo na pointi 20, itategemea na mabao ya kufunga na kufungwa, ili timu hizo ziweze kubadilishana nafasi katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Katika msimamo wa ligi hiyo, Azam FC ipo nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi tisa, imeshinda sita, sare mbili, imepoteza moja, ina pointi 20, wakati JKT Tanzania ipo nafasi ya nne, imecheza mechi 10, imeshinda tano, sare mbili, imepoteza tatu, ina pointi 17.
Ukiachana na msimamo wa ligi, mabeki wa JKT Tanzania watakuwa na kazi ya kuwazuia nyota wa Azam kama Abdul Suleiman aliye na mabao manne, Feisal Salum 'Fei Toto' (matatu) ambaye msimu uliopita alimaliza nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao akipachika 15.
Mwingine ni Idd Selemani 'Nado' mwenye mabao mawili na 2025-2026 alikuwa na mabao manane.
Kwa upande wa JKT Tanzania, miongoni mwa wachezaji wa kuchungwa ni Paul Peter mwenye mabao mawili na 2025-2026 alimaliza na mabao tisa.
Msimu uliopita, JKT Tanzania iliambulia pointi moja pekee kwa Azam, Oktoba Mosi, 2025 ilipotoka sare ya bao 1-1, huku ikipokea kichapo cha 3-0, Aprili 17, 2026.
Timu hizo zinakutana leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam kuanzia saa 12:30 jioni.
Kocha wa Azam, Florent Ibenge, amesema: "Kati ya timu zenye ushindani mkubwa JKT Tanzania ni miongoni mwao, tunatarajia utakuwa ni mchezo wenye chalenji nzuri ya ushindani, pia kupishana nafasi moja ni kitu ambacho kwa timu yangu kitasaidia kupambana zaidi."
Kwa upande wa nahodha wa Azam, Lusajo Mwaikenda, amesema: "Tumekuwa tukipambana sana kupata alama tatu kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na JKT Tanzania ni timu ngumu lakini inatupa nguvu ya kujituma zaidi."
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema: "Haitakuwa mechi rahisi, pamoja na hilo maandalizi yamekamilika, tupo tayari kwa mechi."
Mchezaji wa JKT Tanzania, Jafary Maneno, amesema: "Tayari benchi la ufundi limeishatuandaa, tupo tayari kuyafanyia kazi maelekezo yao ya mazoezini, haitakuwa mechi rahisi lakini tutapambana."
Mechi nyingine leo ni Coastal Union dhidi ya Dodoma Jiji, ambazo msimu uliopita kila timu ilivuna alama tatu katika uwanja wake wa nyumbani matokeo yakiwa Dodoma 2-0 Coastal Union (Septemba 27, 2025), Coastal Union 3-1 Dodoma (Aprili 15, 2026).
Kama Dodoma Jiji ikishinda mechi hiyo itakayoanza saa 3:00 usiku, itafikisha pointi 18, vivyo hivyo Coastal Union iliyopo nafasi ya nane na pointi 13, ikivuna alama tatu, inaweza ikazishusha Singida Black Stars iliyo na pointi 14 na Namungo yenye alama 15.
Kocha wa Dodoma Jiji FC, Vincent Mashami, amesema: "Siyo mechi rahisi, lakini tumejiandaa na tunatambua utakuwa mchezo wenye chalenji ya ushindani mkubwa."
Kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema: "Kila mechi kwetu ni muhimu kupata alama tatu, Dodoma ni timu yenye ushindani mzuri, lakini tumejipanga kukabiliana nao kuhakikisha tunatoka na ushindi."