Chirwa aiokoa Geita, TRA United ikikwama nyumbani
Muktasari:
- Chirwa aliifungia Geita Gold bao hilo dakika ya 70, zikiwa zimepita dakika 20 baada ya Anni Elijah kuifungia TRA United bao la kuongoza. Matokeo hayo yaliifanya Geita Gold kuondoka na pointi moja katika mchezo ambao wenyeji walikuwa na matumaini ya kutumia vizuri uwanja wao kupata ushindi.
MSHAMBULIAJI wa Geita Gold, Obrey Chirwa, ameendelea kuwa tegemeo la kikosi hicho baada ya kufunga bao la kusawazisha na kukiokoa dhidi ya TRA United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Chirwa aliifungia Geita Gold bao hilo dakika ya 70, zikiwa zimepita dakika 20 baada ya Anni Elijah kuifungia TRA United bao la kuongoza. Matokeo hayo yaliifanya Geita Gold kuondoka na pointi moja katika mchezo ambao wenyeji walikuwa na matumaini ya kutumia vizuri uwanja wao kupata ushindi.
Bao hilo linaongeza uzito wa mchango wake katika safu ya ushambuliaji ya Geita Gold msimu huu, akionyesha umuhimu wake katika nyakati ambazo timu inahitaji mchezaji wa kubadilishia matokeo.
Bao la leo linamfanya Chirwa afikishe idadi ya mabao matano ya Ligi Kuu.
Mshambuliaji huyo raia wa Zambia alikuwa pia miongoni mwa wachezaji walioisaidia Geita Gold kupata pointi katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam FC, baada ya kufunga penalti dakika ya 45.
Nyota huyo pia alifunga bao la uokozi dhidi ya Azam na la kusawazisha dhidi ya TRA United, Chirwa amekuwa na mchango wa moja kwa moja katika mechi mbili ambazo Geita Gold imepata pointi moja.
Kwa upande wa TRA United, sare hiyo inaendeleza mwenendo wa kupata mfululizo nyumbani awali timu hiyo ilitoka suluhu dhidi ya Yanga.
Matokeo hayo yanaifanya TRA United kusalia nafasi ya 13 kwenye msimamo ikicheza mechi tisa, imeshinda moja, sare tano na kupoteza tatu ikikusanya pointi nane.
Pointi moja iliyoipata Geita Gold inaifanya isalie nafasi ya 12 kwenye msimamo ikicheza mechi 10 ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza tano.