Inspector Haroun: Simba wametimiza utabiri wangu
Muktasari:
- Babu, ambaye ni shabiki wa Simba, alikuwa ametabiri timu hiyo kufunga mabao mawili dhidi ya watani wao wa jadi, utabiri ambao umetimia baada ya Simba kupata mabao mawili na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
INSPECTOR Haroun, maarufu Babu, ametamba baada ya Simba kuichapa Yanga mabao 2-1 katika Dabi ya Kariakoo iliyochezwa jana, akisema matokeo hayo yamethibitisha utabiri wake wa kabla ya mchezo kwamba Mnyama angefunga mabao mawili.
Babu, ambaye ni shabiki wa Simba, alikuwa ametabiri timu hiyo kufunga mabao mawili dhidi ya watani wao wa jadi, utabiri ambao umetimia baada ya Simba kupata mabao mawili na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumza baada ya dabi hiyo, Babu alisema ametulia baada ya kuona Simba ikifanya kile alichokuwa amekisema kabla ya mchezo, huku akionyesha furaha yake kwa matokeo yaliyopatikana katika pambano hilo lililokuwa likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hizo mbili.
“Hatutaki kelele, roho zimetulia sasa, na utabiri wangu umetimia,” alisema Babu, akisisitiza kuwa matokeo hayo yamempa sababu ya kujivunia kauli yake ya kabla ya mchezo.
Hata hivyo, furaha yake kwa ushindi wa Simba haikumzuia kuzungumzia kiwango cha kipa Rushine, akipendekeza apumzishwe kwa muda kutokana na kile alichodai kuwa ni kushuka kwa kiwango, huku akitaka benchi la ufundi liwape nafasi wachezaji wengine.
“Rushine apewe mapumziko, kiwango kinashuka. Jana ameshindwa kucheza jihadi. Kwenye bao la Cassali, Derick alitakiwa kuzuia, lakini alionekana kuchelewa,” alisema Babu.
Aliongeza kuwa Rushine anapaswa kupewa nafasi ya kupumzika ili aweze kurejea akiwa katika kiwango bora, huku akilitaka benchi la ufundi kutumia dirisha dogo la usajili kuimarisha kikosi hicho kwa kuongeza kipa mwingine.
“Mwalimu awape nafasi mabeki wengine, Rushine apumzike atarudi vizuri, lakini dirisha dogo tupate kipa,” alisema Babu, akitoa maoni yake kuhusu maeneo ambayo Simba inapaswa kuyafanyia kazi licha ya ushindi huo dhidi ya Yanga.