Inspector Haroun aionya Yanga
Muktasari:
- Haroun alisema anaiona dabi ya msimu huu ikiwa ya moto na Simba sasa imeanza kuonekana tofauti baada ya kipindi cha kujenga na kutafuta mchanganyiko sahihi wa kikosi.
MWANAMUZIKI Inspector Haroun ‘Babu’, ambaye ni shabiki kindakindaki wa Simba, ameingia kwenye presha ya Dabi ya Kariakoo akitabiri ushindi wa mabao mawili kwa timu yake na kuwaonya watani wao Yanga kujiandaa na kazi ngumu.
Haroun alisema anaiona dabi ya msimu huu ikiwa ya moto na Simba sasa imeanza kuonekana tofauti baada ya kipindi cha kujenga na kutafuta mchanganyiko sahihi wa kikosi.
“Naiona dabi ya msimu huu inakwenda kuwa dabi ya moto sana kwa sababu Simba Sports tulikuwa tunajitafuta, tulikuwa tunajenga timu, lakini sasa hivi tumekuwa na muunganiko mzuri,” anasema.
Kwa kujiamini, Haroun anasema hata Yanga wanafahamu ubora wa Simba, licha ya utani unaoendelea kuelekea mchezo huo.
“Tuko vizuri na kisaikolojia wanajifanya wako kimya, lakini wanafahamu muziki wa Simba,” anasema.
SIMBA IPO KWENYE DAMU
Haroun anasema ushabiki wake wa Simba si wa jana, tangu enzi za mchezaji Mohamed Mwameja anaishabikia Simba na ushabiki umeanzia kwenye familia yake, akifichua baba yake Mzee Kaena na baba yake mdogo walikuwa mashabiki wa timu hiyo.
“Mimi ujue Simba ipo kwenye damu. Mzee wangu Mzee Kaena alikuwa Simba, baba yangu mdogo pia alikuwa shabiki kindakindaki wa Simba. Kwa hiyo mimi ni mwana Simba na tangu enzi za Mohamed Mwameja nipo naishabikia Simba,” anasema.
Anasema akiwa mtoto katika eneo la Wireless nyumba namba 25 kabla hajaamia Mikoroshini, nyumbani kwao kulikuwa na bendera ya Simba, huku utani wa Simba na Yanga ukiwa sehemu ya maisha yao.
“Nilikuwa nafurahia huu utani wa jadi. Mzee wetu Mzee Kaena alikuwa jirani na Mzee Manara pale Wireless. Akipita pale wanataniana na baba kuhusu Simba na Yanga na sisi tunafurahi, pia kulikuwa na mama mmoja anaitwa Mama Yanga ilikuwa Simba ikifungwa tu anakuja nyumbani kututania kwa kumwaga maji uwanjani kwetu na sisi Simba ikishinda tunaenda kumwaga maji kibarazani kwake,” anasema.
Haroun anasema licha ya kuwa shabiki wa Simba, ana marafiki wengi wanaoshabikia Yanga na hilo halijawahi kuwa kikwazo kwenye urafiki wao.
“Mpira ni upendo na rafiki zangu pia wapo Yanga. Tunajadili mpira, mwishowe kila mtu anashabikia klabu yake. Kwa hiyo hatutengani kwenye hilo kwa sababu sisi ni Watanzania,” anasema.
Akizungumzia dabi hiyo, anasema Simba ina wachezaji anaowaamini wanaweza kuleta madhara kwa Yanga, akiwataja Libasse Gueye, Mpanzu na Clotous Chama ‘Triple C’, huku kikosi chake cha kwanza leo Jumamosi ni cha kocha Steve Barker.
“Juzi kati nilikuwa Geita tukawa tunapiga stori na rafiki yangu mmoja kuhusu hii dabi. Nikamwambia hii dabi inaenda kuumiza kwa sababu nikimwangalia Libasse Gueye,
nikimwangalia Mpanzu, nikimwangalia Chama, Triple C ambaye yuko bora kipindi chote huku Rushine De Reuck ataongoza ukuta wa Simba, naona kabisa watani wakae sawa na watakufa mbili,” anasema.
DOUMBIA AANZIE BENCHI
Katika mpango wake wa kikosi, Haroun anamtaka Mpanzu kuanza kama namba tisa, huku Doumbia akianzia benchi na kuingia kipindi cha pili.
“Tunaanza na mchezaji namba tisa lakini pale aanze Mpanzu. Wakati huo Doumbia ananzia benchi,”€ anasema na kuongeza, Doumbia angeingia kipindi cha pili baada ya Simba kupata mabao mawili, akiamini uwepo wake unaweza kuongeza presha na kuwasha mashabiki.
“Yeye nataka aingie kipindi cha pili wakati huo mtani kashapigwa mbili. Doumbia anaingia anaenda kuwamshaamsha, Doumbia kipenzi cha mashabiki hivyo mashabiki wa Simba wakiwa na furaha ya mabao mawili kutoka kwa timu yao huku Doumbia nae anawapa furaha kwa uwepo wake tu uwanjani hata kwa dakika 20,” anasema.
Kwa upande wa kuwa na jezi ngapi Haroun amesema ana jezi za Simba za misimu yote
“Mimi kwa upande wa Simba nina jezi za misimu yote kila jezi ikitoka, nakumbuka kuna mwaka mmoja mimi na professor J tulitoka tukamfuata Selemani Matola kambini akatupatia jezi ya Simba kipindi hicho jezi ya Simba ni adimu enzi za Azim Dewji miaka ya 90 hiyo.