Meddie Kagere: Simba imenipa zawadi ya ‘Birthday’
Muktasari:
- Mbali na Ligi Kuu Bara, Kagere aliwahi pia kuifungia Simba katika mechi za mashindano ya Afrika, ikiwamo dhidi ya Al Ahly ya Misri mwaka 2019.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba, Meddie Kagere, amesema ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga umekuwa zawadi maalumu kwake katika siku yake ya kuzaliwa, akifurahishwa na namna Wekundu wa Msimbazi walivyopambana na kugeuza matokeo katika Kariakoo Dabi iliyochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kagere, aliyekuwa uwanjani kushuhudia mchezo huo, amesema jambo lililomfurahisha zaidi ni kuona Simba haikukata tamaa baada ya kuruhusu bao la mapema lililofungwa na Peter Shalulile dakika ya tano.
Simba ilisawazisha kupitia Neo Maema dakika ya 68, kabla ya Elie Mpanzu kufunga bao la ushindi dakika ya 72 na kuipa timu hiyo pointi tatu muhimu.
“Kwanza nawapongeza wachezaji wa Simba kwa kazi kubwa waliyoifanya. Leo ni siku yangu ya kuzaliwa, nimefurahi sana. Matokeo haya ni kama zawadi kwangu. Nimefurahia namna walivyocheza, kwa sababu hata walipofungwa bao la kwanza hawakukata tamaa. Waliendelea kupambana na kufanikiwa kupata ushindi,” amesema Kagere.
Mshambuliaji huyo amesema wakati Yanga ilipopata bao la kwanza, baadhi ya watu waliokuwa karibu naye walikuwa na presha, lakini yeye aliendelea kuamini kuwa Simba ingeweza kurejea mchezoni.
Amesema aliwaambia wenzake kuwa Simba ikifanikiwa kusawazisha, ingeweza kupata bao la pili. Utabiri huo ulitimia baada ya Maema kusawazisha na Mpanzu kufunga bao la ushindi ndani ya dakika nne.
“Nilikuwa uwanjani na najua mambo yanavyokuwa. Kulikuwa na wenzangu waliokuwa na presha, lakini niliwaambia kitu kimoja: Simba ikirudisha bao moja, itapata la pili. Wengine wakaanza kuniambia kama naweza kuwa kocha, lakini bado najifunza,” amesema Kagere. Kauli ya Kagere ina uzito kutokana na historia yake ndani ya Simba, ambako alijijengea jina kama mmoja wa washambuliaji waliokuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao.
Alijiunga na klabu hiyo mwaka 2018 akitokea Gor Mahia ya Kenya na kuanza kwa kishindo, akifunga mabao 23 katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/19 na kutwaa tuzo ya mfungaji bora.
Kagere aliendeleza makali yake msimu wa 2019/20, alipofunga mabao 22 ya ligi na kutwaa tena tuzo ya mfungaji bora, hivyo kuwa miongoni mwa wachezaji waliotwaa tuzo hiyo kwa misimu miwili mfululizo.
Rekodi nyingine muhimu katika kipindi chake Simba ilikuwa kufikisha mabao 50 ya Ligi Kuu Bara akiwa na klabu hiyo. Alifikia hatua hiyo Desemba 2020 baada ya kufunga penalti katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC.
Mafanikio hayo yalidhihirisha mchango wake katika kikosi cha Simba, kilichokuwa kikisaka mafanikio katika mashindano ya ndani na ya Afrika.
Mbali na Ligi Kuu Bara, Kagere aliwahi pia kuifungia Simba katika mechi za mashindano ya Afrika, ikiwamo dhidi ya Al Ahly ya Misri mwaka 2019.