Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ifahamu familia ya watoto saba wa Magufuli, wanne wakianza na herufi J

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu familia ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli haikuwa ikiweka wazi idadi ya watoto na wajukuu alionao marehemu, lakini Jumatatu katika mazishi ya kitaifa yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, watu wengi wamejua idadi hiyo.

Dodoma. Kwa muda mrefu familia ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli haikuwa ikiweka wazi idadi ya watoto na wajukuu alionao marehemu, lakini Jumatatu katika mazishi ya kitaifa yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, watu wengi wamejua idadi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi ndiye aliyeanika jambo hilo wakati akisoma wasifu wa marehemu.

Juzi kwa mara ya kwanza Watanzania walisikia yakitajwa majina saba ya watoto wa Rais Magufuli na wajukuu 10.

Kwa nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani, familia ya Rais inahesabiwa ni ‘familia ya kwanza ya nchi’ na huwekwa hadharani wakati rais anapoingia madarakani.

Utamaduni huo ni tofauti na Tanzania, ambapo kiongozi anayeingia madarakani si lazima ataje familia yake, labda atakapopenda mwenyewe.

Marais wengine wa Tanzania waliotangulia watoto wao walifahamika kwa baadhi ya Watanzania ama kwa yeye mwenyewe kuwataja, kutajwa kwenye wasifu wa mzazi wao au kutambulishwa kwenye shughuli mbalimbali.

Kwa upande wa Rais Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021, tangu aingie madarakani wakati wa ngwe ya kwanza ya miaka mitano kuanzia Novemba 5, 2015 hadi 2020 na alipoingia tena ngwe ya pili hakuwahi kuwaweka hadharani watoto wake.

Kuna wakati aliwahi kuwaeleza Watanzania kwamba mwanawe aliambukizwa virusi vya corona, lakini hakumtaja jina, umri wala shughuli anayofanya.

Pia, mara nyingine kwa Rais Magufuli kuitaja familia yake ni pale alipoeleza tukio la watoto wake watatu kufunga ndoa pasipo umma kufahamu, huku mmoja akifunga ndoa yeye akiwa madarakani.

Watoto wa Rais Magufuli hawajulikani, hawatabiriki wala hawaonekani kwenye anga za kisiasa kuchukua mkondo au kuwa maarufu kama walivyokuwa watoto wa wanasiasa wengine kama Dk Hussein Mwinyi (Rais wa Zanzibar), Amani Abeid Karume, Ali Karume na Ridhiwani Kikwete.

Wakati wa mchakato wa kuwapata wagombea ubunge wa CCM, jimbo la Kawe mshindi aliibuka Furaha Dominic Jacob ambaye Rais Magufuli mwenyewe alimtaja ni mtoto wa dada yake. Na vikao vya CCM havikumpitisha licha ya kuongoza kwenye kura za maoni.

Hata hivyo, juzi wakati Profesa Kabudi akisoma wasifu wa hayati Magufuli kwenye mazishi yake ya kitaifa jijini Dodoma, aliitaja familia hiyo kuwa ina watoto saba na wajukuu 10.

Profesa Kabudi aliwataja watoto hao ni Suzzan John Magufuli, Edna John Magufuli, Joseph John Magufuli, Jesca John Magufuli, Ruth John Magufuli, Jurgen John Magufuli, Jeremiah John Magufuli na Juliana John Magufuli aliyefariki dunia wakati baba yake akiwa waziri.

Jina maarufu kwa Watanzania wengi ni Jesca ambaye anaelezwa alisoma Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mtoto mwingine wa Rais Magufuli ambaye hafahamiki sana ni Edna anaye elezwa kusoma katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal College of Tanzania jijini Dar es salaam kuanzia 2006 hadi 2007.

Miaka michache baadaye naye alikwenda kusoma Shahada ya kwanza ya Mawasiliano ya Umma Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira jijini Dar es Salaam.

Mwingine ambaye naye hafahamiki sana ni Ruth anayeelezwa miongoni mwa viongozi katika Mkoa wa Morogoro akiwa katika nafasi ya katibu tawala.

Ndoa yake

Pia, Profesa Kabudi kwenye mazishi hayo alisema Rais Magufuli alifunga ndoa mwaka 1989 na Janeth Mathias Mbizo.

Rais Magufuli mwenyewe aliwahi kueleza kuhusu ndoa yake wakati akiwa kwenye mdahalo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba haikuwa na shamra shamra.

“Siku niliyooa watu wengi hawakujua…na haimaanishi sikuwa na pesa ya kununua koti au gauni la harusi kwa mke wangu, sikuona kama vitu hivyo ni vya msingi sana.

“Tulienda hapo kanisani pete tukanunuliwa na Padri, tena zilikuwa za shaba. Padri pia alitununulia soda, nakumbuka mimi nilikunywa pepsi na mke wangu alikunywa mirinda...Baada ya hapo nikaenda zangu lab (maabara) kuendelea na shughuli zangu.”

Padri aliyewafungisha ndoa hiyo na kutoa ufadhili wa pete na soda kwa mujibu wa Rais Magufuli anaitwa Msemwa na sasa yupo Tanga. “Mfuateni Father (Padri) Msemwa yeye atawaeleza vizuri zaidi.”

Magufuli pia alisema hata ndoa za watoto zake haziambatani na sherehe kubwa. “Mpaka sasa watoto zangu watatu wameshafunga ndoa na sikufanya sherehe kubwa. Mmoja alifunga ndoa tayari nikiwa madarakani lakini wala hamkusikia.”