Idrisa Nahoda aweka rekodi ZPL
Muktasari:
- Nahoda alifunga bao hilo dakika ya 45+4 wakati Kipanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMKM, katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Mao A, Unguja. Bao lingine la Kipanga lilifungwa na Islam Hamisi dakika ya 59, huku lile la KMKM mfungaji akiwa Mateo Anton dakika ya 62 kwa penalti.
WAKATI msimu wa Ligi Kuu Zanzibar 2026-2027 ukianza Agosti 29, 2026, nyota wa Kipanga FC, Idrisa Nahoda ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao ndani ya ligi hiyo.
Nahoda alifunga bao hilo dakika ya 45+4 wakati Kipanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMKM, katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Mao A, Unguja. Bao lingine la Kipanga lilifungwa na Islam Hamisi dakika ya 59, huku lile la KMKM mfungaji akiwa Mateo Anton dakika ya 62 kwa penalti.
Wakati Nahoda akiweka rekodi hiyo, msimu uliopita mfungaji wa bao la kwanza Ligi Kuu Zanzibar alikuwa Mohamed Mussa wa Uhamiaji aliyefanya hivyo katika mechi dhidi ya Polisi Zanzibar.
Mbali na hilo, katika mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) 2026-2027 yamefungwa mabao 16, huku ushindani ukionekana kuwa mkubwa zaidi.
Polisi Zanzibar imeanza kwa kuitibulia safari ya kutetea ubingwa, KVZ iliyotwaa msimu uliopitwa kwa kuitandika bao 1-0, huku pia bingwa wa Kombe la FA, KMKM nao wakianza na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Kipanga.
Timu zilizopanda daraja ambazo ni Mwenge na Wembe kutoka Pemba, huku Black Sailors na Raskazone za Unguja, hakuna iliyopata ushindi.
Katika mechi zao za kwanza, Mwenge imetandikwa mabao 2-0 na Muembe Makumbi, wakati Wembe ikichapwa 1-0 na Uhamiaji, huku Raskazone ikitoka 0-0 na Fufuni, matokeo ambayo pia imeyapata Black Sailors mbele ya Chipukizi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Chipukizi, Suleiman Mohammed 'Gamera' alisema wachezaji walikuwa na presha ya mchezo ndio sababu ya kushindwa kufanya ambacho walikihitaji.
Kocha huyo alisema kwa kawaida mwanzo huwa mgumu lakini mechi zinavyochanganya ndivyo ambavyo wachezaji wanakaa sawa, hivyo bado ana imani ya kufanya vizuri.
Naye Kocha Mkuu wa Zimamoto, Abdallah Mohamed 'Bares' aliwapongeza vijana wake kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Mafunzo, akisema timu hiyo ilibadilisha mbinu kipindi cha pili baada ya kukosa nafasi kipindi cha kwanza.
Alisema, waliingia na mpango tofauti kipindi cha kipindi baada ya kuwasoma wapinzani wao, jambo lililowasaidia kuutawala mchezo na hatimaye kupata ushindi huo.