Waziri Pembe ataka vipaji vinavyouzika nje
Muktasari:
- Alisema, hawataishia kuibua tu vipaji, badala yake kuvisimamia na kuhakikisha vinauzika ndani na nje ya Tanzania.
WAZIRI WA Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwa kuibua vipaji vya vijana kwenye michezo watakaoiwakilisha nchi.
Alisema, hawataishia kuibua tu vipaji, badala yake kuvisimamia na kuhakikisha vinauzika ndani na nje ya Tanzania.
Waziri huyo aliyasema hayo wakati akizungumza na Mkurugenzi wa Taasisi ya kutafuta Vipaji (TDS), Feisal Chipsiya kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) baada ya kutembelea viwanja vya michezo. Waziri Pembe, ameahidi kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kutafuta vipaji na kuwashawishi kujiunga na mpira kwani kwasasa umekuwa ajira.
“Vijana wanapaswa kuchangamkia fursa ya michezo, miundombinu imeboreshwa, hiyo ni wakati wa kuonesha vipaji vyenye uwezo wa kuuzika ndani na nje ya Tanzania,”.
Alisema, vipaji vingi hupatikana endapo vitaandaliwa vizuri kwa kuwepo kwa mazingira rafiki na upatikanaji wake kuwa rahisi.
Aliwasisitiza vijana wenye vipaji kushiriki kwenye michezo kwa lengo la kuboresha vipaji na kuongezewa ujuzi wa namna ya kujitunza na kujiendeleza.