Ibenge ashindwa kujiunga na kambi ya Azam Rwanda
Muktasari:
- Azam iliondoka nchini wiki iliyopita kuelekea Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao ambapo ratiba ya klabu hiyo ilitaka kutumia wiki mbili za kukinoa kikosi hicho.
KAMA inavyofahamika kuwa kikosi cha Azam FC kiko nchini Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao 2026-2027, lakini habari mpya ni kwamba kocha mkuu, Florent Ibenge raia wa DR Congo, wasaidizi wake na wachezaji kutokea nchi hiyo wameshindwa kuungana nao.
Azam iliondoka nchini wiki iliyopita kuelekea Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao ambapo ratiba ya klabu hiyo ilitaka kutumia wiki mbili za kukinoa kikosi hicho.
Mwanaspoti linafahamu kuwa wakati kikosi hicho kikiendelea na maandalizi, hapa nchini Ibenge na baadhi ya wachezaji wamesalia jijini Dar Es salaam.
Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti kwamba, Azam haikuondoka na kikosi chote kwenda Rwanda kwa sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wakati wanajiandaa na safari hiyo.
“Rwanda na DR Congo wana mgogoro wa kisiasa, hivyo kumekuwapo na ugumu wa raia wa DR Congo kuingia nchini humo. Ndio maana kocha, wasaidizi wake na baadhi ya wachezaji walishindwa kupata kibali,” kilieza chanzo.
“Hesabu za Azam ni kuirudisha timu Chamazi au kuipeleka Kenya ili kumalizia maandalizi ya msimu ujao kwa sababu mabosi bado wanaamini kuna muda wa kutosha.”
Mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo aliliambia gazeti hili: “Hatujaja Rwanda na kocha na wachezaji wenye asili ya Congo, sijajua sababu ingawa mazoezi yanaendelea kama kawaida.”
Hii sio mara ya kwanza kwa wachezaji raia wa DR Congo kukataliwa kuingia nchini Rwanda, kwani hivi karibuni kiungo mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu alishindwa kujiunga na kikosi hicho kwa wakati.
Azam ikiwa katika maandalizi hayo, itafungua msimu wa Ligi Kuu Bara, Agosti 15, 2026 kucheza dhidi Polisi Tanzania, mechi itakayopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.