Prime
Hizi hapa sababu za Yanga kuhama Chamazi
Muktasari:
- Yanga imetangaza rasmi juzi usiku itahamnia Uwanja wa KMC Complex ambao ni uwanja wa timu ya KMC unaotumiwa pia na vinara wa Ligi Kuu kwa sasa, Simba baada ya kuweka maskani Chamazi kwa muda mrefu kwa mechi za nyumbani za michuano ya ndani na ile ya kimataifa.
YANGA imeukimbia Uwanja wa Azam Complex sasa inajipanga kuanza maisha mapya viunga vya KMC Complex baada ya kutangaza rasmi kuhamia hapo, ikifichuka sababu zilizowafanya mabosi wa klabu hiyo kongwe waitoe timu hiyo huko, huku wamiliki wa uwanja huo wakijibu mapigo kwa kujitetea.
Yanga imetangaza rasmi juzi usiku itahamnia Uwanja wa KMC Complex ambao ni uwanja wa timu ya KMC unaotumiwa pia na vinara wa Ligi Kuu kwa sasa, Simba baada ya kuweka maskani Chamazi kwa muda mrefu kwa mechi za nyumbani za michuano ya ndani na ile ya kimataifa.
Licha ya Yanga kutoweka wazi sababu za msingi ambazo zimewafanya kuukimbia Uwanja wa Azam Complex, lakini Mwanaspoti limepenyezewa ni pamoja na kuona kama uongozi wa uwanja huo umeshindwa kuwa na weledi kwa kusambaza baadhi ya video ambazo zinahusishwa na matukio ya timu hiyo.
Hata hivyo, uongozi wa Azam umejibu hoja hiyo ukidai hawahusiki na kurekodiwa kwa video hizo wala hawana uhakika kama zinawahusu Yanga.
“Hizo video uongozi wetu umeziona tu mitandaoni na wala hazijatoka katika kamera zetu za ulinzi kama inavyodaiwa na ukiziangalia vizuri zinaonyesha kama zimerokidiwa kwa simu,” alisema Meneja wa Uwanja wa Azam Complex, Amir Juma alipotafutwa na Mwanaspoti.
“Hata hizo video za uchafu wa chumbani unawezaje kuthibitisha umetoka kwenye uwanja wetu, hatuwezi kusema ni Yanga na wala hazijatoka kwetu,” alisisitiza Juma.
Hata hivyo, utetezi wa wenye uwanja ukiwa hivyo, Mwanaspoti limefichuliwa sababu ya pili, inayoelezwa kuilazimu Yanga kuukimbia uwanja huo ni hatua ya uwanja huo kupungua uwezo wa kubeba mashabiki tangu uwekwe viti vya kukaa ikidai unawanyima mapato.
Juma amekiri uwanja huo kupungua akisema maamuzi hayo yametokana na hesabu zao za kuupandisha hadhi uwanja wao.
“Ni kweli uwanja umepungua, kwanza sio tu tangu tulipoweka viti, hatua ya kupungua uwanja ilianzia pale tulipoweka ubao wa matangazo wa kidigitali, kabla hatujaweka ubao huo tulikuwa tunachukua mashabiki 10,000,” alisema meneja huyo na kuongeza;
“Baada ya kuweka ubao huo ukapungua kwa mashabiki 3000, baadaye tukaweka viti nako ukapunguza kidogo mashabiki hadi 4,600 lakini hapa tuwe wazi, Azam Complex lazima uwanja ukue kwa kuwa wa kisasa zaidi ili kuupandisha hadhi, maboresho yetu yataendelea na bado tulikuwa na nafasi ya kuwahudumia kwa kuwa sio kila mchezo ulikuwa unajaa.”
AZAM KUWASAKA YANGA
Meneja huyo ameongeza, licha ya Yanga kutangaza maamuzi hayo wao bado hawajapokea barua rasmi kwa uongozi wao kuhusu maamuzi hayo na wamepanga kuwatafuta na kuzungumza nao.
“Unajua haya yametokea siku ya mapumziko labda barua wametuma na ipo ofisini kwetu hivi ninavyoongea na wewe hatuna taarifa rasmi, lakini Azam Complex tutawatafuta Yanga na kujaribu kuzungumza nao kutokana na maamuzi hayo, hizi ni taasisi mbili zina nafasi ya kukaa mezani,” alisema Juma na kuongeza;
“Maboresho ni kitu endelevu hatuwezi kuishia hapa, yatakuja pia maboresho ya kutanua majukwaa ya mashabiki huko mbele haya yote yanalenga kuufanya uwanja huu kukidhi mataka ya kibiashara.”
Yanga ilianza kuutumia Uwanja wa Azam Complex, Machi 12, 2023 kwa mchezo wa Li Kuu dhidi ya Geita Gold ikishinda kwa mabao 3-1, kisha ikautumia kwa michezo 18 ya mashindano.
Kwenye mechi hizo zimo mechi 14 za Ligi Kuu Bara, mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la FA na kuifanya timu hiyo kuipa Azam Complex zaidi ya sh 106 milioni kutokana na ada ya sh 5,900,000 kwa mchezo mmoja.
Endapo Yanga itasimamia maamuzi yao hayo Azam Complex inaweza kupoteza mapato ya Sh 59 milioni kwa mechi 10 za nyumbani za mabingwa hao watetezi zilizosalia msimu huu.