Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Kilichokosewa kati ya Abubakar Salum na Salum Abubakar

MAISHA ya Abubakar Salum ‘Sure Boy’ yalikuwa ya kusisimua. Alikuwa staa mkubwa pale Jangwani. Mfupi, ana kasi, ana chenga. Watu wa Jangwani wakamuita Sure Boy. Alikuwa winga tisho kwelikweli.

Baadaye akamrithisha mwanaye kipaji, Salum Abubakar. Majina yao yanachanganya kiasi. Baba ni Abubakar Salum, mtoto ni Salum Abubakar. Wote majina yao ya utani ni Sure Boy. Huyu Sure boy mtoto alilirithi hadi jina la kupachikwa la baba yake.

Huyu Sure Boy mtoto ana kipaji maridhawa lakini anacheza mpira tofauti na baba yake. Sure Boy mtoto anacheza katikati. Sure Boy baba alikuwa anacheza winga. Ubora mkubwa wa Sure Boy mtoto ni katika kumiliki mpira na kuuficha. Ngumu kumnyang’anya mpira Sure Boy mtoto.

Kinachoendelea kati ya Sure Boy na baba yake ni kitu cha kujifunza. Sijawahi kusikia kama Sure Boy mkubwa anasimamia dili za baba mtoto wake. Wakati mwingine wazazi wa kiume huwa hatukai karibu sana na watoto wake.

Mara kadhaa utakuta mtoto wako analelewa na mama yako na baba yake wa kambo. Nimeliona hilo kwa mastaa wengi. Sio wa mpira tu, hata muziki. Ghafla unashtukia mtoto ana kipaji kubwa. Unapojaribu kurudi kwa mtoto unakuta hana mapenzi makubwa kwako kuliko kwa Mama yake.

Sijui malezi ya Sure Boy yalikwendaje. Sijui. Nimetoa tu mfano hapo juu bila ya kutafiti lakini lengo langu kubwa ni kutafakari namna ambavyo wazazi wengi wa wanasoka wetu wa sasa walivyokosa dili za kusimamia vijana wao kwa sababu kuu mbili.

Kwanza kabisa ni hili la kuwa na uhusiano mbovu na mtoto angali akiwa mdogo mpaka anapokuwa na kubainika kuwa na kipaji. Kitu cha pili ni wazazi wao kukosa elimu ya kutosha nje ya soka ambayo inamuwezesha kumsimamia mwanae akiwa kama Meneja wake.

Kwa mfano, nilitazamia Sure Boy mkubwa apige pesa katika mikataba walau mitatu ambayo mwanae amewahi kusaini na Azam katika nyakati mbalimbali. Sio pesa ya kuomba, ni pesa ya kazi yake ya kumsimamia mwanae. Ni kamisheni kama zilivyo kamisheni nyingine.

Achilia mbali kwa mwanae, lakini Sure Boy mkubwa angeweza kuwa katika nafasi nzuri ya kuwasimamia rafiki za mtoto wake. Inajulikana pale Azam Sure Boy ana mastaa kibao ambao ni rafiki zake. Hawa angeweza kuunganishwa na mwanae kwa ajili ya kazi hiyo.

Hivi ndivyo akina Neymar walivyowapa jeuri ya pesa baba zao. Neymar amegandwa na baba yake, Neymar Senior. Ndiye anayemsimamia kwa kila kitu. Mzee mzima amepiga dili kuanzia uhamisho wa Neymar kutoka Santos kwenda Barcelona, kisha kutoka Barcelona kwenda PSG, na sasa anasubiri kusimamia dili ya Neymar kutoka PSG kurudi Barcelona.

Kiungo wa Juventus, Adrien Rabiot dili zake zote zinasimamiwa na mama yake, Veronique Rabiot. Huyu mama ndiye anayepiga soga katika maongezi yote ya mikataba ya mwanaye. Naye ana kamisheni yake kwa kiasi kikubwa.

Mifano hii ni mingi lakini ukweli ni kwamba hawa wote hawafanyi hizi kazi kwa sababu ni wazazi. Hapana. Vilevile wamejiendeleza kielimu kujua kinachoendelea katika mchezo wa soka. Kujua namna ya kufanya mazungumzo ya aina hii.

Siwalaumu sana wachezaji wa zamani. Akina Sure Boy hawakupewa elimu kubwa ya soka. Wangepewa leo hii wanasoka wengi wa zamani dili zao zingekuwa zinasimamiwa na wazazi hao. Hata wale wazazi ambao hawakucheza soka kwa kiwango kikubwa wangeweza kuwasimamia watoto wao ili wapige pesa.

Nawalaumu wanasoka wa kileo. Sijui kama wanajua kinachoendelea sana katika kile ambacho wanafanyiwa leo. Kuna baadhi yao wa wasimamizi. Inafikirisha kujua kama na wao wamejipanga kufanya kazi ya usimamizi katika siku za usoni.

Mwanasoka anapomaliza kucheza soka kuna uwanja mkubwa anaoweza kuutumia kupitia kazi aliyowahi kufanya. kuna anayeweza kuwa mchambuzi, mwandishi wa habari, wakala wa wachezaji, kocha, na kazi nyingine.

Hili la kusimamia wanasoka wa kizazi kijacho ni muhimu kwa wanasoka wa sasa hata hivyo naona wanasoka wa kigeni wanakuwa wajanja zaidi katika hili. Kwanza kabisa karibu wote wana Mameneja wao na mawakala wao. Na si watu wa kubabaisha.

Kupitia wao wanaweza kujifunza zaidi kazi hii. Itashangaza baadaye mchezaji kama Jonas Mkude atakaposhindwa kuwa meneja wa baadhi ya wachezaji. Muda wake mwingi alipata bahati ya kusimamiwa na meneja wake.

Hawa akina Sure Boy wanaweza kujitetea kwamba achilia mbali elimu, lakini hawakupata fursa ya kusimamiwa na mameneja au mawakala. Wakati huo hawakuwepo nchini. Lakini itashangaza baadae wakati Sure Boy mtoto atakaposhindwa hata kuifanya kazi hii kwa mtoto wake na kuruhusu pesa nyingi itoke nje ya familia.

Majuzi nilisikia staa wa zamani wa Coastal Union, Kassa Mussa ndiye Meneja wa staa wa sasa wa Coastal Union na timu ya taifa, Bakari Mwamunyeto ambaye anasakwa na klabu za Simba na Yanga. Hivi ndivyo ilivyopaswa kuwa kwa mastaa wa zamani.

Labda kwa sababu Kassa ametumia muda mwingi kuishi nchi za nje katika nchi za Ugiriki na Italia. Huenda huko ndiko ambako amechangamsha zaidi akili yake. Hata hivyo mastaa wengine walipaswa kuchangamka zaidi kama yeye.