Hiki hapa kinachoikwamisha Tausi FC
Muktasari:
- Changamoto hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizomfanya aliyekuwa akiisimamia timu hiyo kuona ugumu wa kuendelea na uwekezaji huo, hasa kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa kuliko matarajio yake.
TAUSI FC, ambayo ilikuwa miongoni mwa timu zilizotoa ushindani mkubwa katika ligi ya wanawake msimu uliopita, imeanza vibaya msimu huu baada ya kupoteza mechi zote tatu za mwanzo.
Timu hiyo, iliyokuwa ikijulikana awali kama Ukerewe Queens kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa Tausi, ilipanda daraja kutoka Ligi ya Mkoa. Hata hivyo, ilijipambanua kwa uwekezaji mkubwa uliohusisha usajili wa makocha wenye uzoefu, wachezaji nyota na wa kimataifa, pamoja na mfumo wake wa uendeshaji.
Lakini msimu huu mambo yameonekana kwenda tofauti, huku timu hiyo ikianza kwa kusuasua. Taarifa zinaeleza kuwa aliyekuwa akiisimamia timu hiyo ameamua kujiondoa kutokana na changamoto mbalimbali za kiuendeshaji, ikiwamo gharama kubwa za vibali vya wachezaji wa kigeni.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, gharama za vibali hivyo zimekuwa mzigo mkubwa kwa uendeshaji wa timu hiyo. Inadaiwa kuwa kibali cha mchezaji mmoja wa kigeni kinagharimu Sh12 milioni.
Aidha, wakala anayewasimamia nyota wa Tanzania, Clara Luvanga na Aisha Masaka, Anton Maksimov ndiye anayetajwa kuinunua Tausi, lakini inadaiwa ameamua kuachana nayo kufuatia kuongezeka kwa gharama za vibali vya wachezaji.
Tausi ina zaidi ya wachezaji 10 wa kigeni, hali inayofanya gharama za vibali pekee kuwa kubwa na kuibua maswali kuhusu uwezo wa timu hiyo kuendelea kugharamia kikosi chake cha sasa.
"Kuna taarifa kwamba sasa hivi Tausi iko chini ya Alliance Girls wanaisimamia, lakini wachezaji wengi wa kigeni hawajaingizwa kwenye mfumo. Kwa hiyo, Anton ameiacha kwa sasa kutokana na mzigo wa vibali," amesema kiongozi mmoja wa timu hiyo.
Changamoto hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizomfanya aliyekuwa akiisimamia timu hiyo kuona ugumu wa kuendelea na uwekezaji huo, hasa kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa kuliko matarajio yake.