Yanga Princess ilitawala, JKT Tanzania ilicheza kimbinu
Muktasari:
- Katika mechi hiyo licha ya Wananchi kupoteza lakini walikuwa bora kwenye umiliki wa mpira na idadi kubwa ya mashuti langoni lakini kwa JKT walicheza kiufundi zaidi na kuondoka na pointi tatu muhimu.
JUZI zilipigwa mechi tano za Ligi Kuu ya Wanawake ikiwemo ile ya Yanga Princess dhidi ya JKT Queens na maafande hao wa kike waliondoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 lakini takwimu zinaonyesha kitu tofauti.
Katika mechi hiyo licha ya Wananchi kupoteza lakini walikuwa bora kwenye umiliki wa mpira na idadi kubwa ya mashuti langoni lakini kwa JKT walicheza kiufundi zaidi na kuondoka na pointi tatu muhimu.
Kwa mujibu wa takwimu za Azam TV, Yanga Princess ilionekana kuishika mechi katika maeneo mengi muhimu, lakini baada ya dakika 90, alama tatu muhimu zilikwenda kwa JKT Queens walioonyesha nidhamu ya hali ya juu ya kimbinu na ukatili mbele ya lango.
YANGA PRINCESS ILIKUWA BORA HAPA
Ukiangalia takwimu hizo ni wazi Yanga ndio waliokuwa wakicheza kwa kasi na katika umiliki wa mpira iliongoza kwa asilimia 52 dhidi ya asilimia 48 za JKT.
Ingawa tofauti ya asilimia nne inaweza kuonekana ndogo kwenye karatasi, uwanjani ilimaanisha viungo wa Yanga, Agnes Pallangyo, Riticcia Nabbosa na Winifrida Charles walikuwa na uwezo mkubwa wa kuamua muda gani wa kupandisha mashambulizi na wa kutuliza mpira.
Pili, Yanga ilitawala katika kutengeneza nafasi na kushambulia. Ilipiga jumla ya mashuti 12 na sita yalilenga lango na mengine sita yakitoka nje . Hii ni mara mbili ya mashuti yote waliyopiga JKT (jumla ya mashuti sita, matatu yakilenga lango na matatu yakitoka nje).
Aidha, presha ya Yanga langoni mwa maafande hao ilizaa kona sita ikilinganishwa na kona moja iliyoipata JKT.
Takwimu hizo zinaonyesha safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo ilikuwa inaongozwa na Salamata Kouanda na Cynthia Musungu ilikuwa ikifika eneo la hatari la wapinzani wao mara kwa mara na kuwalazimisha mabeki wa JKT kufanya kazi ya ziada kuokoa hatari.
Hata hivyo, kutawala takwimu hizi kulikuja na gharama kubwa ya kukosa utulivu sehemu za mwisho. Kupiga mashuti sita yaliyolenga lango bila kufunga kunadhihirisha ubora wa kipa wa JKT, Naijat Abbas ambaye aliokoa mashuti matatu ya hatari kipindi cha pili, pia udhaifu wa washambuliaji wa Yanga katika kufanya maamuzi sahihi wanapokaribia goli.
Pia, kuotea mara tatu dhidi ya mara moja ya JKT kunaonyesha jinsi washambuliaji wa Yanga walivyokuwa na haraka ya kutaka kufunga, wakijikuta wakinasa kwenye mtego wa safu ya beki iliyokuwa inaongozwa na nahodha Anastazia Katunzi na Ester Maseke.
JKT MBINU
Siri kubwa ya ushindi wa JKT Queens katika mchezo huo haikuwa katika kumiliki mpira muda mrefu, bali ni ufanisi wa hali ya juu na nidhamu ya kimbinu. Wakati Yanga ilihitaji mashuti 12 bila kupata hata bao moja, JKT ilitumia mashuti yao matatu tu yaliyolenga lango kupata bao la moja la Asha Mwalala lililoamua mechi. Hii ndiyo tafsiri halisi ya ukatili katika soka kutumia nafasi chache zinazopatikana kwa asilimia kubwa.
Eneo la pili JKT walidhibiti presha na nidhamu ya mechi, ikifahamu fika Yanga ina kasi na inapenda kushambulia kupitia pembeni na katikati.
JKT ilijipanga vyema nyuma na kuwaacha Yanga wamiliki mpira katika maeneo yasiyo na madhara makubwa.
Walipopata mpira, walifanya mashambulizi ya kushtukiza yaliyokuwa na malengo mahususi, jambo lililowalazimu wachezaji wa Yanga kufanya madhambi mara kwa mara ili kuwazuia.
Takwimu zinaonyesha Yanga ilicheza madhambi mara 20 dhidi ya 14 za JKT Queens, na kuambulia kadi mbili za njano huku JKT ikimaliza mechi bila kadi yoyote.
Hii inathibitisha JKT ilikuwa na utulivu mkubwa wa kiakili na iliposhambuliwa, ilikaba kwa akili bila kutumia nguvu zilizopitiliza na iliposhambulia, iliwafanya Yanga wapaniki na kucheza rafu zilizowapotezea mwelekeo na muda wa mechi.
Mechi hii inatoa funzo kubwa kwa benchi la ufundi la Yanga. Kucheza vizuri, kumiliki mpira kwa asilimia 52 na kupata kona sita ni hatua nzuri ya kiuchezaji, lakini soka la ushindani linahitaji matokeo.
Bila kuboresha umakini katika umaliziaji na kupunguza presha isiyo ya lazima inayozalisha faulo nyingi hasa wanapokutana na timu zinazocheza kwa akili kama JKT, Simba na Mashujaa itaendelea kushuhudia pointi tatu zikienda kwa wapinzani wao.
SIMBA MWENDO WA KICHAPO
Mabingwa watetezi, Simba Queens imeendelea kuonyesha bado ina kiu ya kutetea taji lao baada ya kuanza msimu kwa kasi, ikishinda mechi zote tatu za mwanzo na kukusanya pointi tisa baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa Queens.
Simba ilianza kwa kuichapa Kilimanjaro Wonders mabao 3-0 katika mechi ya ufunguzi, kabla ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate Princess raundi ya pili.
Katika raundi ya tatu, mabingwa hao waliendeleza ubabe kwa kuichapa Mashujaa Queens mabao 2-0, ushindi unaowafanya wafikishe mabao sita huku wakiwa hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa katika mechi hizo tatu.
TAUSI FC BADO CHANGAMOTO
Wakati Simba ikiendelea kutembea kifua mbele, hali ni tofauti kwa Tausi FC ambayo imeendelea kukumbana na wakati mgumu mwanzo wa msimu huu baada ya kupoteza mechi zote tatu.
Tausi ilianza kwa kichapo cha mabao 5-2 kutoka kwa Bunda Queens, ikafuatiwa na kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Alliance Girls katika raundi ya pili, kabla ya kukubali kichapo kingine cha mabao 2-0 kutoka kwa Ceasiaa Queens.
Matokeo hayo yanaifanya Tausi kuwa miongoni mwa timu ambazo bado hazijapata pointi msimu huu, huku changamoto kubwa ikiwa ni namna ya kurekebisha safu yao ya ulinzi ambayo tayari imeruhusu mabao tisa katika michezo mitatu.
Matokeo ya mechi nyingine za mzunguko wa tatu, Alliance Girls ikiwa Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, imetoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Bunda Queens, Bunda Girls imepata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Geita Queens, Ceasiaa Queens imeitandika Tausi FC mabao 2-0 na Kilimanjaro Wonders ikitoka suluhu dhidi ya Fountain Gate Princess.
Alliance imekuwa na mwanzo mzuri ikikusanya pointi saba kwenye mechi tatu ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ceasiaa Queens kisha ikaitandika Tausi FC mabao 2-1 kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Bunda Queens.
WASIKIE HAWA
Kocha wa Yanga Princess, Said Maulid ‘SMG’ anasema kipindi cha kwanza hawakuwa bora kutokana na wachezaji wake kuwa na hofu ya kucheza na timu kubwa kama JKT.
“Kipindi cha pili niliwaeleza watoe hofu wapambane bado wanaweza kufanya vizuri na mabadiliko ya dakika 45 za kipindi cha pili yalisaidia sana kuwaingiza Rehema Mohamed, Sandrine Mutuyimana ambao waliongeza kasi zaidi kwenye eneo la ushambuliaji, tunaamini tunayo nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwa sababu kwa sasa timu imeanza kuimarika.”
Kocha msaidizi wa JKT Queens, Azishi Kondo anasema walicheza kimbinu zaidi wakijua Yanga inashambulia hivyo wakamaliza mechi mapema kipindi cha kwanza.
“Sisi tulicheza kipindi cha kwanza tukamaliza mechi lakini kipindi cha pili niliwaambiwa wachezaji wangu kuwa Yanga itakuja kwa kutushambulia zaidi hivyo tunapaswa kulinda hiki tulichokipata lakini tuwashambulie kwa kushtukiza.”