Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii ndio sababu Maema kurudi Msimbazi


KIGALI: Wakati mashabiki wa Simba wakisubiri kuona sura mpya zitakazokamilisha kikosi, kuna kitu mabosi wa klabu hiyo wameshtukia na kukubaliana na kocha Steve Barker juu ya ombi lake la kumrudisha Neo Maema.


Wakati Maema akirudi, taarifa zinabainisha kwamba, Seleman Mwalimu ameondoka Rwanda na kurudi Tanzania kwa ajili ya kwenda Morocco kuungana na kikosi cha Wydad kufuatia mkataba wake wa mkopo na Simba kumalizika.

Maema ambaye aliitumikia Simba kwa mkopo wa msimu mmoja 2025-2026 akiwa mali ya Mamelodi Sundowns, ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi 2026-2027 baada ya Barker kueleza kuwa bado yupo kwenye mipango yake.

Awali Barker aliweka mapendekezo yake ya kuendelea na Maema, lakini uongozi ulionekana kusitasita, baada ya kuishuhudia timu ikicheza mechi mbili za michuano ya Kagame dhidi ya Mogadishu City na Jamus ikitoka 0-0 huku timu ikionekana haina muunganiko mzuri kutoka kwenye kiungo na ushambuliaji, ndipo ishu ya kumrudisha Maema ikachukuliwa kwa umakini sana ikiaminika kiungo huyo anaweza kutatua changamoto hiyo kwa kushirikiana na wenzake kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Katika msimu mmoja aliocheza ndani ya Simba, Maema haraka alikuwa mmoja wa viungo muhimu wa kikosi hicho na kuongeza uwiano katika kushambulia na kulinda. Uwezo huo umeifanya Simba kutaka kumbakiza kwa msimu mwingine huku ikiamini bado ana mchango mkubwa katika kikosi hicho.

Ndani ya benchi la ufundi la Simba, kuna imani kuwa Maema ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuongeza ushindani kikosini kutokana na uzoefu wake wa kucheza mechi kubwa pamoja na uwezo wake wa kutuliza presha ya timu.

Akizungumza akiwa kambini Kigali nchini Rwanda, Barker alisema maandalizi yanaendelea vizuri lakini bado kikosi chake hakijakamilika kutokana na kusubiri baadhi ya nyota kujiunga na timu, akiwemo Maema.

“Tumefurahishwa na wachezaji tuliowasajili kuongeza nguvu kikosini, bado tunawakosa mmoja au wawili, akiwemo Neo Maema ambaye tunatumaini atajiunga nasi muda si mrefu. Kwa ujumla maandalizi yanaendelea vizuri, lakini bado kuna mambo mengi ya kuboresha kabla ya msimu kuanza,” alisema Barker.

Kauli hiyo imeweka wazi kuwa Simba bado inaendelea na mchakato wa kuhakikisha inambakiza Maema, lakini wakati juhudi hizo zikiendelea, imeibuka kuwa kuna tofauti kubwa kati ya namna suala lake linavyoendeshwa na lile la mshambuliaji Seleman Mwalimu.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka chanzo cha ndani cha Simba, zinaeleza kuwa mkataba wa mkopo wa Mwalimu kutoka Wydad Athletic Club ulimalizika baada ya msimu uliopita, hivyo kwa taratibu za usajili alitakiwa kurejea Morocco kuripoti kwa waajiri wake kabla ya hatua nyingine yoyote kuchukuliwa.

Chanzo hicho kinasema Simba ilikuwa na nia ya kuendelea kubaki na mchezaji huyo kwa mkopo wa msimu mwingine, lakini mchakato ulipaswa kuanza baada ya Mwalimu kuripoti Wydad na kujiunga na maandalizi ya msimu mpya.

“Hakuna mgogoro kati ya Simba na Wydad. Kilichopo ni kufuata utaratibu unaotakiwa. Mchezaji anatakiwa kwanza arudi kwenye klabu yake, kocha mpya amuone, ndipo mazungumzo yaendelee. Simba bado ina nia ya kumbakiza, lakini uamuzi haupo upande mmoja pekee,” kilisema chanzo.

Inaelezwa kuwa benchi jipya la ufundi la Wydad chini ya kocha raia wa Ureno, Paulo Sergio, linataka kwanza kumuona Mwalimu katika maandalizi kabla ya kufanya uamuzi wa kama ataendelea kubaki kikosini, atatolewa tena kwa mkopo au klabu itaamua kufanya biashara nyingine.

Tofauti na taarifa zilizozagaa zikidai Simba ilikuwa tayari imekamilisha kila kitu kuhusu Mwalimu, ukweli ni kwamba mazungumzo bado yanaendelea na uamuzi wa mwisho utategemea pia tathmini ya benchi jipya la Wydad.

Mfano unaotolewa Simba ni ule wa Maema. Baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika, Simba iliomba ruhusa maalumu kutoka klabu yake ili aendelee kucheza mchezo mmoja wa mwisho wa Kombe la CRDB dhidi ya Azam uliofanyika Julai 4, 2026.

Baada ya ruhusa hiyo kutolewa, Maema aliichezea Simba mechi hiyo kabla ya kurejea Afrika Kusini kuripoti kwa klabu yake ya Mamelod kama taratibu zinavyotaka. Ni baada ya hapo ndipo Simba ilianza mazungumzo mapya ya kutaka kumbakiza.

Kwa Mwalimu hali ni tofauti kidogo. Taarifa zinaeleza tayari ameondoka kambini Kigali na kurejea Dar es Salaam huku hatua zinazofuata zikitarajiwa kuwa ni kukamilisha taratibu za kurejea Wydad kabla ya Simba kuendelea na mazungumzo ya kumrejesha kwa mkopo iwapo makubaliano yatafikiwa.

“Kwa sasa jambo la muhimu ni kusubiri hatua za Wydad baada ya maandalizi kuanza. Simba inaendelea na mazungumzo, lakini hatuwezi kusema kila kitu kimekamilika wakati mchakato bado unaendelea,” kiliongeza chanzo hicho.

Kwa sasa Wekundu wa Msimbazi wanaendelea na maandalizi kupitia michuano ya CECAFA Kagame nchini Rwanda, wakijiandaa na mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Singida Black Stars utakaochezwa Ijumaa Julai 31, 2026.

Ushindi katika mchezo huo utaweka hai matumaini ya kutinga nusu fainali, huku maandalizi ya Simba Day Agosti 8 na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga yakisalia kuwa sehemu muhimu ya ratiba kuelekea msimu wa 2026-2027.