Prime
Hesabu mpya za Barker, Pedro Kariakoo Dabi
PRESHA ya Dabi ya Kariakoo imezidi kupanda baada ya timu za Yanga na Simba kukutana Fainali ya Kombe la Muungano itakayochezwa Jumatano Aprili 29, 2026, kisha Mei 3 mwaka huu, huku makocha wa timu hizo mbili wakifunguka namna ya akili zao zinavyopiga hesabu mpya.
Tuanze na Simba ambayo ilikata tiketi ya kwenda fainali Jumapili baada ya kuichapa Mlandege kwa mabao 3-0, kocha wake Steve Barker ameliambia Mwanaspoti amelazimika kubadili hesabu zake baada ya kufikiria namna ya kuingia kwenye dabi hizo mbili.
Barker amesema Simba inalitaka Kombe la Muungano kutokana na ukame wa mataji katika klabu hiyo na kikosi chake kitaingia na akili kubwa kuhakikisha wanatoka salama kwenye fainali hiyo.
Barker amesema hautakuwa mchezo rahisi kwa timu zote lakini akachekelea kila mchezaji wake muhimu yuko tayari kwa mechi hiyo kubwa ya uamuzi ambayo inasubiriwa na mashabiki wa Simba kuona kombe linatua Msimbazi.
“Unajua Simba haijashinda taji ndani ya misimu minne, kwa hiyo kuna akili mpya hapa lazima tuizingatie kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye hii fainali ili mashabiki wetu wasiumie,” amesema Barker.
“Haitakuwa mechi rahisi, tunakwenda kukutana na bingwa mtetezi, unapotaka kuwa bora lazima ushindane na walio bora, kitu kizuri ni kwamba wachezai wetu wako salama, ni hatua ya kwenda kufanyia kazi mbinu kabla ya mchezo huo.”
Simba imekuwa ikisaka mafanikio ya kubeba makombe kwa muda mrefu, huku ikifanikiwa kubeba Kombe la Muungano 2024 ilipoifunga Azam. Kabla ya hapo, mara ya mwisho ilishinda Ngao ya Jamii 2023.
Wakati Barker akiyasema hayo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves amesema kikosi chake kina hesabu za kwenda kulinda heshima yao kwa kutetea ubingwa wanaoushikilia lakini pia rekodi ya kutopoteza mbele ya wekundu hao kwa muda mrefu.
Pedro amesema kikosi chake kimeimarika na kwamba sasa wanacheza kama timu bingwa inayotaka kwenda kutetea mafanikio hayo na watajiandaa kwenye kila kitu ili washinde mechi hiyo.
“Timu hizi mbili zinatoka kukimbizana kwenye ligi ni lazima tuiheshimu Simba sio mchezo rahisi na itakuwa fainali ngumu, lakini kwetu sisi tulijiandaa kukutana na timu yoyote, tuna jukumu la kutakiwa kulinda ubingwa wetu, pia rekodi yetu,” amesema Pedro.
“Hakuna nafasi ya kuhofia lolote, tunakwenda kujipanga kukabiliana nao, tuna wachezaji bora wanaotaka kuthibitisha thamani na ubora wao, hii ni timu ambayo ina kiu ya mafanikio makubwa.”
Yanga itakutana na Simba kwenye fainali ya Kombe la Muungano itakayopigwa Aprili 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar na ikimalizika hiyo timu hizo zitakwenda kukutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Mei 3, 2026 jijini Dar es Salaam.
Rekodi zinaonyesha tangu mara ya mwisho Simba iifunge Yanga katika Ngao ya Jamii Agosti 13, 2023 kwa penalti 3-1, imepoteza mechi sita mfululizo walizokutana huku ya mwisho ikimalizika kwa 0-0.