Hapa mchawi lazima atafutwe, nani alimpa sumu Ommy
Muktasari:
Mwandishi na mwanazuoni wa Marekani, Harold Coffin ametupa nukuu nzuri. Anasema: “Envy is the art of counting the other fellow’s blessings instead of your own.”
KATIKA imani ya Buddha, kuna msamiati huu; Mudita. Maana yake ni ukarimu au furaha bila ubinafsi. Ukitaka maana kinyume cha Mudita ni husuda, kijicho, wivu na maneno mengine yenye tafsiri sawa na hiyo.
Mwandishi na mwanazuoni wa Marekani, Harold Coffin ametupa nukuu nzuri. Anasema: “Envy is the art of counting the other fellow’s blessings instead of your own.”
Kiswahili: Husuda ni sanaa ya kujishughulisha kuhesabu baraka za wengine badala ya zako.
Binadamu mwenye husuda anaweza kuwa anamiliki biashara yenye mtaji wa mabilioni, lakini akawa anamwonea kijicho mfanyabiashara milionea. Atafanya hila ili kumkwamisha mwenzake. Mwenye husuda furaha yake ni anguko la wengine.
Husuda zipo maofisini. Bosi anaweza kumwonea gere mfanyakazi wake. Mfanyakazi anapoteza hamu ya kula na anakosa usingizi kwa sababu ya ubora wa kazi za mfanyakazi mwenzake.
Mwenye husuda ni mbinafsi. Anaweza kumwonea kijicho mkewe au mumewe. Mafanikio ya mumewe au mkewe yanaweza kumkondesha. Unakuta mtu anaanzisha mradi binafsi kwa siri eti apate maendeleo binafsi ili amzidi mke au mume wake.
Unapaswa kuliweka hili akilini; mwenye husuda ni muuaji. Hata awe mwenzi wako wa maisha, ukishamgundua ni hasidi mwogope, kaa naye mbali. Kama anatamani yeye ndiye afanikiwe na wewe ubaki tegemezi kwake, huyo hashindwi kuhujumu unachofanya ili mapenzi yake yatimie.
Hili weka akilini; mwenye husuda atakuchukia bila sababu. Akiwa hana cha kukufanya ataumia hadi uzito wa mwili wake utashuka. Akiwa na uwezo wa kuyadhuru maisha yako, hatakuacha salama. Atakuchonganisha na wafanyakazi wenzio au bosi wako. Atahujumu kazi zako, na akiwa na nafasi atakubania.
Kama nyote ni wafanyabiashara, badala ashirikiane na wewe mpige hatua, atakuhujumu uanguke. Yupo radhi naye aathirike ili wewe uathirike zaidi.
Mtu mwenye husuda anaweza kuhakikisha umeshapoteza kazi, umefilisika na umegeuka chokambaya, ila akikuona una furaha, atataka kujua chanzo cha furaha yako ili akufanye usiwe na furaha. Anaweza kufanikiwa yote, ukawa mufilisi na huna furaha, ila kwa vile unapumua, atajiuliza; mbona hafi? Na akipata nafasi kweli atakuua!
Kisa cha mja mwenye husuda, alipata bahati ya kuulizwa na Mungu aseme hitaji lake lolote na atapewa, ila jirani yake atapewa mara mbili ya alichoomba. Akaona akiomba gari, jirani atapewa mawili, vivyo hivyo nyumba na kadhalika. Mja akaomba chongo, apoteze jicho moja kusudi jirani yake apoteze mawili.
Bahati mbaya mwenye husuda huwa hajijui. Dr Remmy kupitia wimbo Karola, anaimba: “Ukiwa mtenda mabaya wewe mwenyewe haujijui. Ukiwa mtenda mabaya kila siku utasema unaonewa.” Mwenye husuda anaweza kulalamika hatendewi haki.
BAADA YA MUHTASARI
Habari ambayo imeshitua wengi ni ugonjwa wa Ommy Dimpoz. Mshituko zaidi unaletwa na kile ambacho amekieleza kuwa chanzo cha ugonjwa wake ni sumu. Kwamba mitihani yote ambayo Dimpoz anaipitia, sababu ni sumu.
Mfumo wa kimwili wa Dimpoz umebadilishwa. Njia ya kawaida ya chakula imefungwa, ametengenezewa mpya. Tumbo limevutwa juu. Sauti yake haitoki sawasawa na imebadilika. Ukimsikiliza, inajenga wasiwasi kama ataweza kuimba kwa sauti ileile aliyokuwa akiimbia nyimbo zake.
Yote hayo yamesababishwa na kuharibika kwa bomba la kupitisha chakula (esophagus). Madaktari wamemtengenezea esophagus mpya. Kwa mujibu wa madaktari wake Kenya na Afrika Kusini, jinsi esophagus ya Dimpoz ilivyoharibika inatoa picha kwamba, aliwahi kula au kunywa sumu.
Dimpoz mwenyewe akabaki na mshangao, maana katika maisha yake hajawahi kula au kunywa sumu. Mshangao wake unatoa tafsiri kuwa katika maisha yake hajapata kuhudhuria hospitali kwa tatizo la sumu. Ingewahi kutokea angekumbuka. Na isingekuwa mshangao.
Hapa isomeke vema; madaktari hawajasema Dimpoz amekutwa na sumu mwilini. Wala hawajaeleza kwamba, wamekuta sumu kwenye esophagus. Isipokuwa wameufafanua ugonjwa wa Dimpoz kuwa ni matokeo ya kula au kunywa sumu. Ila athari ya sumu ndiyo imemfanya Dimpoz awe tofauti leo.
Anapokula, akitaka kumeza inakuwa kama mapambano. Lakini, alipokwenda kwenye hospitalizetu zile akaambiwa kuwa ana kansa. Inashtua sana.
Gavana wa Mombasa, Kenya, Hassan Joho, alipompeleka Dimpoz hospitalini Kenya, akaambiwa tatizo lake sio kansa, ila limesababishwa na sumu. Dimpoz akaulizwa: “Umewahi kunywa au kula sumu?” Akabaki anatoa macho. Maana kumbukumbu zake hazimwambii kama mwili wake umewahi kupokea sumu, hasa iliyopita kooni.
Kenya ikawa haiwezekani kumfanyia oparesheni. Akapelekwa Afrika Kusini. Ikabidi afanyiwe vipimo upya, majibu yalipotoka, madaktari wa Afrika Kusini wakamuuliza swali lilelile: “Umewahi kula au kunywa sumu?” Kwa mara nyingine akatoa macho. Akaambiwa athari ya koo lake ni matokeo ya sumu.
Safari ya matibabu yake; Tanzania, Kenya na Afrika Kusini pamoja na maumivu ya kabla na baada ya upasuaji, imesababishwa na sumu. Hivi sasa hawezi kuimba kwa sauti aliyonayo labda mpaka apone. Na muziki ndiyo maisha yake.
Fikiri sauti ikishindikana kurejea kwenye hali yake ya zamani. Hapo kuimba itakuwa ndiyo basi. Vipi sauti ikitoka vizuri halafu ikawa tofauti na ya zamani? Kimsingi tafsiri ya karibu kuhusu ubaya wa walimwengu ipo kwa Dimpoz. Mchawi wake ni kielelezo cha uwepo wa shetani duniani.
TUMSAKE MCHAWI
Ni vigumu mno kwa Dimpoz kujua nani alimpa sumu, maana athari imetokea muda mrefu baadaye. Sumu ingempa matokeo siku alipoila au kuinywa, bila shaka angeweza kuvuta picha ni nani alihusika. Hata hivyo, tunaweza kumsaka mchawi kupitia utunzi wa nadharia.
Nadharia ya kwanza; akina nani ni maadui wa Dimpoz? Sumu si ya jana wala juzi, kwa hiyo hata ambao walipata kuwa na uhasimu naye zamani lakini sasa wanaelewana, inawezekana miongoni mwao kuna ibilisi fulani aliamua kumtenda.
Nadharia ya pili; akina nani hawampendi Dimpoz? Hapa inajumuisha muziki wake na mzunguko wa maisha yake ya kila siku. Bahati mbaya ni kwamba binadamu wengi ni wanafiki. Inawezekana machoni wanamwonesha upendo, ila pembeni wakatumbukiza sumu kwenye chakula au kinywaji cha Dimpoz.
Nadharia ya tatu; muziki wa Dimpoz ni mateso kwa akina nani? Inawezekana kuna watu humwona Dimpoz kama tishio kwao. Kila akitoa wimbo wanaumia. Labda wameshajaribu mbinu mbalimbali kumkwamisha bila mafanikio. Mwisho wakajiuliza; kwa nini asife? Wakamwekea sumu au wakakodi watu kumwekea sumu.
Nadharia ya nne; mapenzi ni mitihani jamani! Unaweza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu mwenye husuda. Huyo anaweza kushirikiana na wabaya wako kukumaliza. Vilevile kuwa na mpenzi mwenye wivu kupita kiasi ni janga. Anaweza kuhisi unamsaliti kisha akaona suluhu ni kukupa sumu. Waja ni katili sana.
Nadharia ya tano; ushindani wa muziki na kukomoana. Kwamba inawezekana sumu haikukusudiwa kumuua Dimpoz ila kuharibu koo ili ashindwe kuimba tena. Hiyo inaweza kusababishwa na watu wenye kushindana naye au yupo ambaye lengo lake lilikuwa kumkomoa tu.
Nadharia ya sita; kilichobainika ni athari baada ya sumu. Haipo wazi iliingia mwilini lini. Sasa basi, inawezekana Dimpoz alipewa sumu kabla hajawa mwanamuziki maarufu au hata utotoni.
Hizi ni nadharia tu. Kwa Dimpoz zinaweza kumtesa sana, matokeo yake akawahisi wasiohusika kabisa. Anachotakiwa kwa sasa ni kuzingatia maelekezo ya madaktari na kuongeza umakini kwa watu wanaomzinguka, maana wabaya hawana rangi. Tumuombee Dimpoz.