Gomes awapa ahueni Yanga, amtaja Kibu, Manyama

Muktasari:

RIPOTI ya Kocha wa Simba, Didier Gomes amekabidhi kwa uongozi ripoti ambayo itawapa ahueni Yanga na itawashusha pumzi kwenye mbio za kuwania mastaa wapya katika dirisha hili la usajili.

RIPOTI ya Kocha wa Simba, Didier Gomes amekabidhi kwa uongozi ripoti ambayo itawapa ahueni Yanga na itawashusha pumzi kwenye mbio za kuwania mastaa wapya katika dirisha hili la usajili.

Kocha huyo raia wa Ufaransa amewaambia Simba kwamba anataka wasajiliwe wachezaji wapya watatu tu lakini wengi wao wanaweza kuwa raia wa kigeni.

Hiyo inamaanisha hakutakuwa na purukushani ya usajili wa wachezaji wazawa baina ya watani wa jadi msimu huu.

Gomes ameliambia Mwanaspoti kwamba kuna kitu anakifikiria kuhusiana na mastaa wa kigeni lakini atakiweka wazi baada ya kumalizika kwa mechi zote za msimu akimaanisha kombe la FA na Ligi.

Alisema amefuatilia ligi ya ndani na kuangalia timu mbalimbali kuna baadhi ya wachezaji amevutiwa nao na anaamini kama akiwapata kuna vitu vichache anaweza kuwabadili na wakaongeza kitu.

Lakini amesisitiza kwamba akili yake haipo sana kwenye wachezaji wa ndani na hata kama asiposajili kabisa eneo hilo haiwezi kumuathiri kwavile anaamini anao wengi wanaowazidi.

“Nadhani kuhusu Edward Manyama, Kibu Denis na wachezaji wengine ambao wapo katika timu zao na mikataba haijamalizika tusubiri ila msimu ukimalizika nitakueleza,” alisema Gomes.

“Usajili wa wachezaji wandani nadhani si uhitaji mkubwa kwetu kwani ambao nipo nao katika timu ni bora mno na nimewaeleza nahitaji kuwa nao zaidi lakini kama kuna ambaye atapata maslahi mengine anaweza kwenda nampa ruhusa na nafasi yake tutaongeza.

“Wachezaji wa nje ya nchi, ndio tutasajili kwani kuna hitaji hilo, lakini tuliache kwanza hili muda ukifika nitalieleza kwa upana kwani sasa akili ni kuchukua ubingwa wa ligi pamoja na kombe na Shirikisho (ASFC),” alisema Kocha huyo ambaye amepania kusuka Simba mpya inayocheza soka lake.

Mwanaspoti linafamu Gomes, miongoni mwa wachezaji ambao anavutiwa nao ni Manyama ambaye Simba imemsajili kwa usiri mkataba wa miaka mitatu na Kibu Denis ambaye pia anadili la kwenda TP Mazembe.

Katika hatua nyingine Gomes alisema kwa ambavyo anafuatilia mashindano ya ndani pamoja na uelewa aliokuwa nao katika ligi mbalimbali pamoja na mashindano ya kimataifa Simba watafanya usajili mzuri.

“Nimefundisha nchi mbalimbali nina taarifa nyingi hata mchezaji wa kigeni ambaye atakuja hapa atakuwa mwenye kukidhi mahitaji ya timu ambayo yalikuwa mapungufu yetu msimu huu,” alisema Gomes.

Licha ya kwamba usajili haujafunguliwa rasmi mpaka ligi itakapomalizika Julai 18, lakini tayari timu mbalimbali ikiwemo Yanga, Azam na Simba zimeanza kusainisha wachezaji mikataba ya awali.

Yanga tayari imeshasainisha wakongomani wawili mmoja beki na mwingine kiungo na wazawa wawili mmoja wa Dodoma Jiji na mwingine wa KMC.

Dili ya Yanga na straika Mzambia Lazarous Kambole anayekipiga Kaizer Chiefs imefutika baada ya mchezaji huyo kushinikiza alipwe Sh23milioni ambao ni mshahara wa kufuru kwa timu za Tanzania.