Geita Gold yatafuta nini chanzo
Muktasari:
- Taarifa za ndani zilizoifikia Mwanaspoti zinaeleza vikao hivyo vilifanyika juzi, ambapo uongozi ulianza kwa kukutana na makocha kabla ya kikao kingine na wachezaji ili kusikiliza maoni ya pande zote kuhusu changamoto zilizopo.
GEITA Gold imeanza kutafuta suluhisho la mwenendo usioridhisha wa timu hiyo baada ya uongozi kufanya vikao viwili tofauti na makocha pamoja na wachezaji, ukitaka kubaini chanzo cha matokeo yasiyoridhisha katika mechi za hivi karibuni.
Taarifa za ndani zilizoifikia Mwanaspoti zinaeleza vikao hivyo vilifanyika juzi, ambapo uongozi ulianza kwa kukutana na makocha kabla ya kikao kingine na wachezaji ili kusikiliza maoni ya pande zote kuhusu changamoto zilizopo.
“Walikaa kwanza na makocha, baadaye wakakutana na wachezaji ili kujua tatizo liko wapi na kwa nini timu imekuwa ikikosa matokeo. Kuna mambo wamekubaliana kuyafanyia kazi ili kurejesha matokeo mazuri, lakini hakuna madai yoyote makubwa yaliyowasilishwa kwa uongozi katika vikao hivyo,” kimesema chanzo.
Katika mechi sita za mwanzo za msimu, Geita Gold imekusanya pointi saba, ikishinda michezo miwili, kutoka sare moja na kupoteza mitatu.
Timu hiyo ilianza kampeni kwa ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Mbeya City, kabla ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Azam FC. Baadaye ilipoteza dhidi ya Namungo FC 0-1, Simba 0-2 na mabingwa watetezi Yanga (0-1).
Hata hivyo, Geita Gold imeweka rekodi ya ushindi mkubwa zaidi wa mabao kwenye ligi msimu huu hadi sasa baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 6-2, matokeo yanayoonyesha uwezo wa timu hiyo inapokuwa katika kiwango chake.
Geita Gold inaongozwa na kocha Zuberi Katwila, aliyeisaidia timu hiyo kurejea Ligi Kuu Bara kutoka Championship baada ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa kukusanya pointi 71. Vikao hivyo vinaonyesha hatua ya uongozi kutafuta njia ya kuimarisha mwenendo wa timu na kurejesha matokeo mazuri katika mechi zijazo.