Kalambo aitega IAA SC kiaina
Muktasari:
- Timu ya IAA SC ya Arusha ilifuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, kupitia mechi ya 'Play-Off', baada ya kuitoa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda nyumbani 2-1, kisha ugenini ikatoka sare ya bao 1-1.
KIPA wa IAA SC ya jijini, Arusha, Aaron Kalambo amesema licha ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja, ila bado ana nafasi ya kuondoka katika kikosi hicho, ikiwa atapata timu nyingine inayocheza Ligi Kuu Bara dirisha dogo la Januari 2027.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kalambo amesema katika mkataba wake kuna kipengele kinachomruhusu kujiunga na timu yoyote ya Ligi Kuu Bara kwenye dirisha dogo la Januari 2027, ingawa kwa sasa malengo yake ni kukipigania kikosi hicho cha Arusha.
"Malengo yangu ni kucheza Ligi Kuu ndio maana kabla ya kusaini mkataba niliwaambia viongozi juu ya suala hilo kijumla, nawashukuru walinikubalia na nikawaahidi kuwapigania ili kufanya vizuri katika Ligi ya Championship," amesema Kalambo.
Kipa huyo aliyejiunga na IAA SC akitokea Transit Camp inayoshiriki pia Ligi ya Championship, Coastal Union, Geita Gold na Dodoma Jiji, amesema uzoefu wake ni chachu muhimu ya kukisaidia kikosi hicho, kwa kushirikiana na wachezaji wenzake.
IAA SC inayoshiriki Championship kwa mara ya kwanza msimu wa 2026-2027, kabla ya mechi ya jana Jumapili dhidi ya Rhino Rangers ya mjini, Tabora, imeshinda moja, ikitoka sare mbili na kupoteza pia mbili, ikiwa nafasi ya 11 na pointi tano.
Timu ya IAA SC ya Arusha ilifuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, kupitia mechi ya 'Play-Off', baada ya kuitoa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda nyumbani 2-1, kisha ugenini ikatoka sare ya bao 1-1.