Prime
Gamondi ajionea bato la mabeki Yanga
KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi ameanzisha vita kwenye eneo la ulinzi wa kati wa timu yake na sasa kuna uwezekano wa mastaa wawili wa kiwango cha timu ya Taifa kukaa nje kila mechi.
Yanga msimu uliopita ilitwaa makombe yote ya ndani lakini ikafika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Gamondi ambaye ni raia wa Argentina, kwa sasa ametengeneza bato kubwa la namba kwenye timu hiyo baada ya kumsajili Gift Fred na sasa atakuwa na mabeki wanne bora wa kati ambao wote wapo kwenye timu zao za taifa.
Timu hiyo itakuwa na Fred, nahodha Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job ambao wanacheza kwenye eneo hilo.
Hii ina maana kuwa kocha huyo atakuwa analazimika kuwaanzisha wachezaji wawili tu hapo, aidha Fred na Mwamnyeto au Job na Bacca au Bacca na Fred au Bacca na Mwamnyeto kwenye timu yake.
Inaonyesha kuwa mastaa wawili wa Yanga kila mechi watakuwa wanaanzia nje, au wanaweza kuwaondoa mabeki wa pembeni kama ambavyo Job alifanya kwenye baadhi ya michezo msimu uliopita, lakini mabeki waliopo kwa sasa, Yao Kouassi na Joyce Lomarisa nao wanaonekana kuweka msingi kwenye nafasi zao.
Endapo ataamua kuwatumia pembeni mabeki hao, ina maana kuwa wakali wawili pia, Yao ambaye anaaminika ni beki bora wa pembeni na Joyce ambaye msimu uliopita alifanya mambo makubwa watakaa nje.
Mchezo wa kwanza wa hadharani wa Kilele cha Wiki ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs alimuanzisha Job na Mwamnyeto ambao walionyesha uwezo mzuri na mapumziko akawatoa na kuwaingiza, Bacca na Fred nao walionyesha kiwango cha hali ya juu kuonyesha kuwa sasa kuna vita.
Mazoezi kocha huyo amekuwa mkali kwa wachezaji wake wa eneo la ulinzi huku akivutiwa na wale ambao wamekuwa wakicheza kwa kasi na pasi ndefu na sasa anapambana kuweka mambo sawa tayari kukiwasha dhidi ya Azam.
Hii ni vita kali kwa mastaa hao na Gamondi anasema kuwa atakayeonyesha kuukubali mfumo wake haraka ndiye atakeyepata nafasi ya kucheza. Amesisitiza kwamba anataka safu ngumu ya ulinzi ambayo itasaidia timu kuwa na uwiano mzuri na kusapoti staili yake ya uchezaji.