Prime
Fei Toto, Yanga kimeeleweka

KUNA furaha inaendelea Jangwani yalipo Makao Makuu ya Klabu ya Yanga, hiyo ni baada ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya nne mfululizo na ya 31 kihistoria.
Wakati furaha hiyo ikishamiri, kuna jambo lingine limeibuka ambalo linanogesha kile kinachoendelea katika klabu hiyo, hili linahusu usajili.
Taarifa zilizopo ni kwamba, Yanga imefanikiwa kumalizana kwa siri na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto', aliyekubali kupewa mkataba wa kurejea timu yake hiyo ya zamani.
Fei Toto amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Azam, lakini hilo halikumzuia kiungo huyo kukubali mkataba huo wa kurejea Yanga ambayo ilikubali kumuachia kwa lazima miaka miwili iliyopita.
Itakumbukwa kabla ya Fei Toto kusaini mkataba huo, alitangulia kuikacha Yanga akiandika barua ya kuvunja mkataba, huku pia akiilipa klabu hiyo na fidia ya Sh 112 milioni za kuuvunja mkataba huo, japo Yanga iligoma kuzipokea kabla ya kulainika walipoalikwa Ikulu na Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka pande hizo kumalina na kumuuza Azam siku moja baadae.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba kiungo huy,ataitumikia timu hiyo kwa msimu ujao baada ya kukubali kusaini mkataba wa miaka miwili.
Azam ilikuwa inapambana kumbakisha kiungo huyo, ikitaka kumpa mkataba wa kufuru,lakini Fei Toto inaelezwa alizuia mchakato huo mara kadhaa.
KUHUSU SIMBA
Simba nayo ilikuwa ikimuwinda kiungo huyo kwa karibu ikitaka kumpa mkataba ambapo klabu hizo kubwa tatu zote zilikuwa zikipishana kutuma ofa za kufuru kwa Fei Toto.
Ingawa Yanga inaficha ikihofia kubanwa na kanuni, lakini Mwanaspoti limejihakikishia kuwa, kiungo huyo amekubali kusaini mkataba wa miaka miwli kufuatia kufurahishwa na ofa ya klabu yake hiyo ya zamani.
“Tumeshakubaliana kila kitu, hii vita tumeshaimalza imebaki hatua tu ya kijana (Fei Toto) kurejea kule alikotoka ni suala la muda tu,” alivujisha mmoja ya mabosi hao wa Yanga.
Tayari Yanga na wasimamizi wa Fei Toto wameshakubaliana kila kitu juu ya mchakato huo, ikibaki hatua moja tu kwa Yanga kwenda kumalizana na Azam.
Bosi mmoja wa juu ndani ya Yanga alifunguka kuwa, uongozi huo utamalizana na Azam kama ambavyo wao walimalizana nao wakati wanakubali kumuachia kufuatia wito wa Rais Samia.
“Mnakumbuka wakati tunawauzia Fei Toto? Hawakutulipa zaidi ya Sh 300 milioni na wao sasa ni wakati wa kufanya biashara ileile ambayo tuliifanya, tutawafuata na tutamalizana,” alisema bosi huyo wa juu wa Yanga.
“Subirini kumuona kijana anarudi nyumbani kila kitu sasa kipo sawa tutakapokamilisha kila kitu tutawatangazia na mtaona ataichezea timu ipi kwa msimu ujao.
Ndani ya mkataba wa sasa wa Fei Toto unaitaka timu yoyote itakayomtaka kiungo huyo italazimika kulipa kiasi cha Dola 500,000 (sh 1.3 Bilioni) kumuachia.
Fei Toto akiwa na Azam msimu huu alikuwa na moto wa kutengeneza nafasi za mabao akiwa ndio kinara wa kutengeneza asisti akiwa nazo 13 huku akifunga mabao manne pekee.
Kabla ya msimu huu msimu uliopita alikaribia kidogo kuibuka mfungaji bora kabla ya kuachwa hatua ya mwisho na kiungo mwenzake wa zamani wa Yanga Stephanie Aziz KI aliyeibuka mfungaji bora kwa mabao 21 huku Fei akibaki nafasi ya pili na mabao yake 19.