Prime
Doumbia apewa siri ya ‘kutoboa’ Simba
SIMBA kesho itakuwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ikicheza mechi yake ya kwanza ya nyumbani msimu huu dhidi ya Coastal Union, akisubiriwa Ibrahim Doumbia kama ataanza kufunga bao lake la kwanza, sasa kocha mmoja wa zamani wa wekundu hao amempa mchongo mshambuliaji huyo.
Doumbia amecheza mechi mbili kati ya tatu mpaka sasa akiendelea kujitafuta, akitumia dakika 113 uwanjani huku akiwa hajafunga bao lolote hadi sasa, akizua mjadala wa kiwango chake kutoka kwa mashabiki.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha wa zamani wa Simba, Dimitar Pantev amesema bado hajaona changamoto ya ubora mdogo kwa Doumbia na kuna kitu kimoja muhimu anatakiwa kukifanya ili aanze kufunga haraka.
Pantev ambaye aliifundisha Simba kwa miezi mitatu tu, amesema ameangalia mechi za wekundu hao na kuona Doumbia ana vitu vinavyomtambulisha kama mshambuliaji mzuri ambapo kwasasa anatakiwa kujipanga kuikataa presha inayotoka nje ya uwanja.
“Nimemwona yule mshambuliaji (Doumbia), nadhani ni mapema kuona hana uwezo, ukimuangalia kwa jicho la kiufundi, unaona ana vitu ambavyo vinaweza kumlinda kuwa ana ubora wa kuwa mshambuliaji mzuri,” amesema Pantev.
“Timu imecheza mechi nne tu na moja hajacheza kapata nafasi kwenye michezo mitatu, nadhani anatakiwa kupewa muda, kitu cha kwanza ambacho ningeweza kushauri, anatakiwa kujisaidia mwenyewe, asifanye kosa la kuivaa presha ya nje ya uwanja itampa shida, atulie uwanjani mabao yatakuja,’’ amesema kocha huyo
Aidha Pantev amesema Doumbia anacheza kwenye timu yenye viungo wazuri na kama wachezaji wenzake watamsaidia kumpa mipira anayotaka basi anaweza kubadilika kwa haraka na kurudi kwenye kufunga.
“Anacheza kwenye timu yenye viungo wazuri, sitaki kuzungumzia sana mambo ya ufundi kwa kuwa hii ni timu ambayo nimetoka na ina kocha mwingine lakini wachezaji wenzake wanaweza kumsaidia pia kama watagundua anahitaji nini ili aweze kufunga.
“Kwenye soka sio kila kitu kinaweza kufanyika au kuonekana kwa haraka, huyu (Doumbia) ni mshambuliaji mpya hapa anahitaji kuzoea namna timu yake inacheza pia ajuane na wenzake vizuri.”
“Ukiliangalia kwa kulipima hilo unaona bado ndio maana kuna wakati Simba inaamua kucheza kama ilivyokuwa inacheza msimu uliopita kwa kumtanguliza winga Ellie Mpanzu kucheza kama mshambuliaji wa mwisho.”