Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Simba atoa onyo kali, Doumbia atajwa!

ONYO Pict


KUNA onyo kali amelitoa Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker kwa wachezaji wa kikosi hicho baada ya kufanya nao kikao kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa kadi nyekundu zinazowakabili.


Katika onyo hilo, Barker amesema hivi sasa hatavumilia kuona nyota wake wanaonyeshwa kadi nyekundu katika michezo inayofuatia baada ya kukumbwa na mkasa huo dhidi ya Kagera Sugar na Pamba Jiji.


Baada ya raundi mbili za Ligi Kuu Bara kumalizika huku kukiwa na kadi nyekundu nne, Simba inaongoza kwa wachezaji wake kuonyeshwa mbili ambao ni beki David Kameta katika mchezo wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar na kiungo Ibraheem Jabaar dhidi ya Pamba Jiji, ikiwa ni mechi ya pili. Wengine ni nahodha wa Coastal Union, Geofrey Manyasi na kipa wa Azam, Aishi Manula.

Barker ambaye mbali na kuwakosa nyota hao wanaotumikia adhabu, pia analazimika kuwakosa wengine waliokumbwa na majeraha akiwemo kipa namba moja, Mahamadou Kassali aliyeumia mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Kagera Sugar.

KUJICH 02

Ili kuona hakuna nyota mwingine ambaye atamkosa kutokana na adhabu ya kadi nyekundu, Barker amefanya kikao hicho na wachezaji wa kikosi hicho akitoa msisitizo kwamba hatavumilia tena kuona hilo likitokea.

“Tunatakiwa kuonyesha kuwa sisi ni timu kubwa, hivyo tunapaswa kuonyesha nidhamu kubwa ya mchezo, hatua ya kwanza nimeongea nao ili kuona wepesi wa kufanikisha hili, baada ya hapo tutaona hatua nyingine za kufuata,” amesema kocha huyo.

Barker amesema, licha ya changamoto hiyo, hawezi kutegemea wachezaji wachache pekee, akisisitiza kuwa mafanikio ya Simba kuvuna pointi sita katika mechi hizo yanatokana na nguvu ya kikosi kizima.

“Ni wazi kwamba unapokuwa na wachezaji waliosimamishwa inakuwa ngumu, lakini timu hazipati mafanikio kwa kutegemea wachezaji 11 pekee. Ni kikosi kizima ndicho kinachofanikiwa,”  amesema.

KUJICH 01

Kauli hiyo imekuja wakati Simba ikijiandaa kwa mchezo mwingine muhimu wa ligi dhidi ya Singida Black Stars huku Barker akitarajiwa kufanya mabadiliko kwenye kikosi kutokana na baadhi ya wachezaji kutokuwepo akiwemo Duchu na Jabaar.

Barker pia amewataka wachezaji waliopo kwenye kikosi kutumia nafasi watakazopata kutokana na wenzao kuwa nje, akisema hali hiyo inaweza kuwa fursa kwao kuonyesha uwezo wao.

“Nafasi hii inawapa wachezaji wengine nafasi ya kucheza na kutumia fursa hizo,”  amesema Barker.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amepongeza pia namna wachezaji wake walivyopambana baada ya kubaki pungufu katika mechi hizo mbili na kupata ushindi, akisema walionyesha umoja, mshikamano na kujituma kuhakikisha timu inapata pointi tatu.

Barker amesema jambo kubwa ambalo anataka kuliona kutoka kwa wachezaji wake ni nidhamu na uwezo wa kuvuka nyakati ngumu bila kupoteza mwelekeo wa mchezo.

KUJICH 03

ISHU YA DOUMBIA

Kocha Barker amelazimika kukaa chini na mshambuliaji wa kikosi hicho, Ibrahim Doumbia ambaye ametua Simba msimu huu akimtaka kuboresha uchezaji wake ili kuinufaisha timu.

Mshambuliaji huyo tangu atue, amefanikiwa kufunga bao moja pekee kwenye mechi za Cecafa, huku akishindwa kutikisa nyavu dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii na mechi mbili za Ligi Kuu Bara alizocheza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesema ameshtukia kitu kwa mshambuliaji huyo na kuna vitu anataka viboreshwe kwa Doumbia, likiwemo kukaa sana kwenye boksi la hatari la wapinzani.

Barker amesema, amemtaka Doumbia kuhakikisha hata kama atakuwa anashuka chini kidogo kusaidia wenzake, lakini anatakiwa kuhakikisha wakati Simba ina mpira anawahi kwenye eneo la hatari ili aweze kupata mipira ambayo inahitajika na kufunga.

“Kuna changamoto tumeziona, anafanya vizuri, anashuka kidogo kuja kusaidia timu, hiyo ni nzuri, lakini anatakiwa wakati tuna mpira awahi haraka pale kwenye boksi, kama atakuwa sana hapo mabao yatakuja kwa kuwa ana vitu ambavyo unaona vinaweza kumsaidia kufunga.

Barker amesema kitu cha pili ambacho amekiona kwa Doumbia ni namna anavyokabiliana na mipira ya juu akitaka kuhakikisha anaruka kwa hesabu ili aweze kufunga kwa kuwa ana ubora wa kujua kufunga kwa mipira ya namna hiyo.

“Anaweza kufunga kwa kichwa, hakuna mashaka kwenye hilo, lakini kuna vitu tumemueleza anatakiwa kuruka kwa hesabu nzuri kwa ‘taiming’ yake sio nzuri sana kwenye mipira ya namna hiyo, tunaamini ataimarika na nadhani itamsaidia.”

Ameongeza kuwa, mshambuliaji huyo raia wa Mali, hatakiwi kucheza kwa presha kubwa na hapaswi kusikiliza mashabiki wanaongea nini kuhusu kiwango chake, kwani atakapoanza kufunga watanyamaza tu.

“Nipo kwenye mpira kwa muda mrefu, najua watu wanaongea sana kuhusu yeye, tumemwambia hatakiwi kusikiliza nini watu wanaongea, aivue hiyo presha, akianza kufunga watanyamaza na wataimba jina lake.”

Shambulizi kali ambalo Doumbia amelifanya kwenye mechi zake mbili za Ligi Kuu Bara, ni pale alipogongesha mwamba kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar, akipokea pasi ya kiungo, Anicet Oura. Shambulizi hilo lilishuhudiwa mpira ukirudi uwanjani ambapo ilibaki kidogo afunge kwani alifanya juhudi kubwa kuuinua mpira na kumpita kipa.