Djibouti yaondoka na mambo mawili Cecafa U-20
Muktasari:
- Djibouti ilianza mashindano kwa kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Uganda, kabla ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Sudan. Matokeo hayo yaliifanya timu hiyo kumaliza safari yake mapema ikiwa haijakusanya pointi katika kundi hilo.
TIMU ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 ya Djibouti imeaga mashindano ya CECAFA baada ya kupoteza michezo yake miwili ya Kundi B, lakini licha ya kuondoka mikono mitupu, kocha wake Abdirahman Ali Abubakar amesema wameondoka na vitu viwili muhimu uzoefu na somo.
Djibouti ilianza mashindano kwa kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Uganda, kabla ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Sudan. Matokeo hayo yaliifanya timu hiyo kumaliza safari yake mapema ikiwa haijakusanya pointi katika kundi hilo.
Akizungumzia hilo, Abubakar amesema kuondolewa kwao hakumaanishi mwisho wa safari, bali amepata nafasi ya kuwapa vijana wake uzoefu wa kushindana dhidi ya timu zenye wachezaji wanaocheza katika kiwango cha juu zaidi.
Kocha huyo amesema moja ya changamoto walizokutana nazo ni tofauti ya umri na uzoefu kati ya kikosi chake na wapinzani wao, akibainisha kuwa sehemu kubwa ya wachezaji wa Djibouti bado ni vijana wanaocheza katika madaraja ya chini.
“Wachezaji wetu wengi ni U-16 na U-17, tofauti na wapinzani wetu ambao wengi wao wanacheza ligi kuu. Hii ilikuwa nafasi nzuri kwa vijana wetu kujifunza na kupata uzoefu wa michezo ya kiwango hiki,” amesema Abubakar.
Alitoa mfano wa Uganda, akisema sehemu kubwa ya kikosi cha timu hiyo ina wachezaji wanaocheza Ligi Kuu, hivyo walikuwa na uzoefu mkubwa zaidi wa mechi zenye ushindani ukilinganisha na vijana wake ambao bado wako katika hatua za kukua kisoka.
Abubakar ameongeza kuwa Djibouti itatumia masomo iliyoyapata CECAFA kuendelea kuwakuza vijana hao na kuwajenga kwa ajili ya mashindano yajayo.