Kocha Djibouti alia na safu ya ulinzi
Muktasari:
- Timu hiyo ilianza kampeni zake za kundi B kwa kichapo kizito cha mabao 4-1 kutoka kwa Uganda.Mashindano yaliyopita timu hiyo ilikuwa imeruhusu mabao 19, na mwaka huu kocha ameanza kuona dalili zilezile.
KOCHA wa timu ya Djibouti U-20, Abdirahman Ali Abubakar, amesema mchezo dhidi ya Uganda umemsaidia kubaini maeneo ambayo kikosi chake kinahitaji kufanyiwa maboresho kabla ya kuendelea na michuano ya CECAFA.
Timu hiyo ilianza kampeni zake za kundi B kwa kichapo kizito cha mabao 4-1 kutoka kwa Uganda.Mashindano yaliyopita timu hiyo ilikuwa imeruhusu mabao 19, na mwaka huu kocha ameanza kuona dalili zilezile.
Kocha huyo amesema moja ya changamoto kubwa aliyoiona katika kikosi chake ni eneo la ulinzi, akieleza kuwa limeonyesha mapungufu ambayo yanahitaji kurekebishwa haraka ili timu iweze kuwa imara zaidi katika michezo inayofuata.
Kocha huyo amesema kucheza na Uganda kulikuwa na faida kwake na kwa benchi lake la ufundi kwa sababu kuliwapa nafasi ya kuona namna safu yao ya ulinzi inavyokabiliana na timu yenye ushindani.
“Moja ya changamoto tuliyoiona ni kwenye ulinzi. Kuna mapungufu ambayo tumeyabaini na sasa tunatakiwa kuyafanyia kazi Uganda ni timu nzuri sana na iko fiti,” amesema Abubakar. Ameongeza uzoefu walioupata dhidi ya Uganda utawasaidia kufanya marekebisho katika mazoezi na kuhakikisha makosa yaliyojitokeza hayajirudii katika michezo ijayo.
Abubakar amesisitiza kuwa kikosi chake bado kina nafasi ya kuboresha kiwango, akiwataka wachezaji wake kutumia kila mchezo kama somo la kuongeza uzoefu na kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto za michuano.