Dimitar Pantev mambo safi Afrika Kusini
Muktasari:
- Pantev anatarajiwa kusaini mkataba utakaomfanya kuwa kocha wa Richards Bay hadi mwisho wa msimu huu, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza muda wa mkataba.
PRETORIA, AFRIKA KUSINI: KOCHA raia wa Bulgaria, Dimitar Pantev amefikia makubaliano ya kuwa kocha mkuu mpya wa Richards Bay inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Pantev anatarajiwa kusaini mkataba utakaomfanya kuwa kocha wa Richards Bay hadi mwisho wa msimu huu, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza muda wa mkataba.
Taarifa zinaeleza kuwa Pantev alikuwa njiani kwenda Afrika Kusini kutoka Botswana akiwa na wakala wake huku taratibu za mwisho za kukamilisha uteuzi wake zikiendelea.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 alijiunga na Simba Oktoba, 2025 akichukua nafasi ya Fadlu Davids, lakini alidumu kwa siku 61 kabla ya uongozi wa klabu hiyo kusitisha mkataba wake Desemba 2, 2025.
Katika kipindi chake Simba, Pantev aliiongoza katika mechi tano, akishinda mbili, sare moja na kupoteza mbili. Timu hiyo ilifunga mabao sita na kuruhusu manne katika kipindi chake.
Pantev alianza kwa kuiongoza Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika, akishinda mabao 3-0 ugenini dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini kisha timu hizo zikatoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa marudiano Dar es Salaam. Matokeo hayo yaliisaidia Simba kufuzu hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0.
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara, mchezo wake pekee ulikuwa dhidi ya JKT Tanzania, ambao Simba ilishinda mabao 2-1.
Hata hivyo, katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilianza kwa kupoteza 1-0 dhidi ya Petro de Luanda ya Angola na baadaye ikafungwa mabao 2-1 na Stade Malien ya Mali, mchezo ambao ulikuwa wa mwisho kwa Pantev kabla ya kusitishiwa mkataba.
Baada ya kuondoka Simba, Pantev aliendelea na safari yake ya ukocha Afrika. Kabla ya Simba aliwahi kuiongoza Gaborone United ya Botswana na kutwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2024/25, huku pia akiwa kocha wa Jwaneng Galaxy msimu uliopita.
Sasa Pantev anakwenda Richards Bay wakati timu hiyo ikiwa haijapata ushindi katika mechi sita za mwanzo za ligi msimu huu, imekusanya pointi tatu, sare tatu na kupoteza michezo mitatu, akiwa hivi karibuni alikuwa hapa nchini akiwa masomoni.