Prime
Pantev atoa siri Simba, Yanga, awashauri Fei Toto, Doumbia
Muktasari:
- Pantev ameonyesha kwamba licha ya kuondoka Simba, soka lipo kwenye damu yake akiibuka viwanjani kutazama mechi mbalimbali. Uwepo wake nchini ukalifanya Mwanaspoti kumtafuta na kufanya naye mahojiano maalumu, akifunguka mambo mbalimbali.
UNAMKUMBUKA Dimitar Pantev? Yule kocha ambaye alijulikana kutokana na tatoo nyingi mwilini? Jamaa yupo hapa nchini kwa majukumu ya kikazi, lakini pia akionekana katika viwanja tofauti.
Pantev ameonyesha kwamba licha ya kuondoka Simba, soka lipo kwenye damu yake akiibuka viwanjani kutazama mechi mbalimbali. Uwepo wake nchini ukalifanya Mwanaspoti kumtafuta na kufanya naye mahojiano maalumu, akifunguka mambo mbalimbali.
Kocha huyo anasema alirejea Tanzania baada ya kupata nafasi ya kushiriki kozi ya CAF Diploma A, akieleza kuwa Shirikisho la Soka Afrika limekuwa likisisitiza makocha wanaofanya kazi barani humu wawe na sifa hizo.
“Katika kipindi hiki ambacho sina timu niliamua kuhudhuria kozi hii ya ukocha. Nina sifa kama hizi kutoka UEFA (Shirikisho la Soka Ulaya) muda mrefu, lakini CAF inapendelea makocha wanaofanya kazi Afrika kutumia diploma ya CAF. Niliwasiliana na baadhi ya watu wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), na walinisaidia mimi pamoja na msaidizi wangu kujiunga na kozi,” anasema Pantev.
Baada ya kumaliza kozi ya kwanza, Pantev anatarajia kurejea tena Tanzania mwezi Novemba kwa ajili ya hatua inayofuata ya kozi hiyo, lakini kurejea kwake hakujamfanya asizungumzie yaliyopita. Anaikumbuka Simba kama sehemu ya safari yake ya ukocha Tanzania, ingawa anakiri kwamba kuondoka kwake haukuwa uamuzi wake.
SIMBA NDIO ILIACHANA NAYE
Pantev anasema alikubali uamuzi wa Simba kumalizana naye, pande hizo mbili zikisitisha mkataba wao. Hata hivyo, anaamini uamuzi huo ulifanyika baada ya mchezo mmoja uliopotezwa dhidi ya Petro de Luanda wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Mtazamo wangu ulikuwa tofauti na wao. Nafikiri si jambo la kawaida baada ya matokeo mabaya ya mchezo mmoja tu. Tulipoteza mchezo mmoja dhidi ya Petro, halafu wakaamua kubadilisha benchi la ufundi. Nafikiri walikuwa tayari wamefanya uamuzi huo kabla ya mchezo ule,” anasema Pantev.
Pamoja na tofauti hizo, Pantev anasisitiza kwamba hana ugomvi na Simba. Anasema pande hizo mbili zilimaliza mambo yao kwa amani na kila mmoja akaendelea na maisha yake.
“Hatuna mjadala wowote. Tulishukuru kila mmoja kwa muda tuliokuwa pamoja, wao wananiombea kila la heri, nami nawatakia kila la heri. Kila mmoja anaangalia njia yake na maisha yake ya baadaye,” anasema.
Baada ya kuondoka Simba, Pantev hakukaa muda mrefu bila kazi. Alikwenda Botswana ambako aliongoza Jwaneng Galaxy hadi mwisho wa msimu na kuipa timu hiyo ubingwa wa Kombe.
Anasema alipewa ofa ya kuongeza mkataba, lakini hakukuwa na makubaliano kuhusu matarajio ya pande zote.
“Nilikuwa tayari nimefanikiwa kila kitu nilichokuwa nimekuja kufanya pale. Walitaka kuongeza mkataba, lakini tuliona hakuna sehemu ya kukutana kati ya matakwa yangu na yao. Nikaona ni bora kubadilisha eneo na kutafuta changamoto nyingine.”
YANGA ANAIPA ALAMA
Akiwa Tanzania kwa sasa, Pantev amekuwa akifuatilia mechi za vigogo mbalimbali, huku akisema Yanga kwa sasa anaiona ikiwa na faida kubwa mbele ya Simba, lakini anaonya kuwa hilo ni kwa karatasi tu.
“Kwa majina na aina ya wachezaji, Yanga wana wachezaji wa kiwango cha juu sana, majina makubwa katika soka la Afrika na wenye uzoefu mkubwa. Simba pia wamefanya usajili,” anasema.
Kwa mtazamo wake, Yanga haikusajili wachezaji wengi kwa idadi, bali ililenga maeneo ambayo ilihitaji kuongeza ubora.
“Wamesajili wachezaji wa ubora katika nafasi ambazo waliona wanahitaji kuongeza nguvu. Hadi sasa inaonekana kwa kiwango kikubwa wamefanikiwa.”
Pantev anaiona Yanga ikiwa na nguvu hasa katikati ya uwanja na uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi. Anakumbuka pia mchezo wa Yanga dhidi ya Simba, akisema Yanga ilianza kwa kusita, lakini baadaye ikachukua udhibiti.
“Katika dakika 15 hadi 20 za kwanza Simba ilikuwa bora, lakini baada ya hapo Yanga iliingia kwenye mchezo. Kipindi cha pili walikuwa bora zaidi, katikati ya uwanja walikuwa na nguvu sana na mbele walitengeneza nafasi nyingi,” anasema.
MAPEMA SANA
Hata hivyo, Pantev anasisitiza kuwa mechi tatu za mwanzo haziwezi kutoa hukumu ya mwisho na kwamba bado muda unatakiwa kupewa nafasi.
“Ni mechi tatu tu zimechezwa. Mtihani mkubwa kwa Simba, Yanga, Azam na Singida utakuwa kwenye mashindano ya CAF. Hapo ndipo tutaona ubora wao halisi na kama wanaweza kushindana katika kiwango cha Afrika,” anasema.
AGOMA KUICHAMBUA SIMBA
Licha ya kuwa kocha wa zamani wa Simba, Pantev amekataa kuingia kwenye uchambuzi wa kina wa kikosi cha sasa cha timu hiyo. Anasema anafuatilia mechi zao, lakini hana sababu ya kuingilia kazi ya benchi jipya la ufundi.
“Ninatazama mechi zao zote, si Simba pekee, pia naangalia Yanga. Lakini si sahihi kutoka upande wangu kuzungumzia Simba na namna wanavyocheza. Ni bora kuzungumza na benchi lao la sasa. Nina uhakika wana watu wazuri na wa kitaalamu na wana mkakati wao. Wakifuata mkakati wao na mashabiki wanafurahia, maana yake kila kitu kiko sawa, kwa sababu mpira ni wa watu.”
DOUMBIA APEWE MUDA
Pantev pia amegusa mjadala unaomzunguka mshambuliaji wa Simba, Doumbia, ambaye amekuwa akikosolewa kutokana na kiwango chake katika michezo ya mwanzo.
Kocha huyo anasema mchezaji yeyote anayefika kwenye timu mpya anahitaji muda wa kuzoea mazingira.
“Kila mchezaji anahitaji muda. Nimemuona yule mshambuliaji (Doumbia), nadhani ni mapema kuona hana uwezo. Ukimuangalia kwa jicho la kiufundi, unaona ana vitu ambavyo vinaweza kukulinda kuwa ana ubora wa kuwa mshambuliaji mzuri,” anasema, akisisitiza kuwa hata mchezaji mwenye jina kubwa anaweza kuhitaji muda kama hajazoea mazingira mapya.
“Timu imecheza mechi tatu tu na moja hajacheza, kapata nafasi kwenye michezo miwili. Nadhani anatakiwa kupewa muda. Kitu cha kwanza ambacho ningeweza kushauri, anatakiwa kujisaidia mwenyewe, asifanye kosa la kuivaa presha ya nje ya uwanja, itampa shida. Atulie uwanjani, mabao yatakuja.
“Anacheza kwenye timu yenye viungo wazuri. Sitaki kuzungumzia sana mambo ya ufundi kwa kuwa hii ni timu ambayo nimetoka na ina kocha mwingine, lakini wachezaji wenzake wanaweza kumsaidia pia kama watagundua anahitaji nini ili aweze kufunga.
“Kwenye soka si kila kitu kinaweza kufanyika au kuonekana kwa haraka. Huyu (Doumbia) ni mshambuliaji mpya hapa, anahitaji kuzoea namna timu yake inavyocheza, pia ajuane na wenzake vizuri. Simba kama wamemsajili, maana yake waliamua kwa kuona ana ubora unaohitajika na wanaamini anaweza kufanya kazi wanayoitaka.”
SHALULILE ATAFANYA MAKUBWA
Pantev hana wasiwasi kuhusu mshambuliaji Peter Shalulile, licha ya kuanza msimu akiwa hajafunga mabao mengi.
Anasema mshambuliaji huyo tayari amejithibitisha katika timu alizopita na anaamini muda si mrefu ataanza kuonyesha makali yake.
“Shalulile atakuja kuonyesha ubora wake. Amejithibitisha kila alikocheza, ni mfungaji bora na naamini atafunga mabao ya kutosha na kuipa timu pointi. Huyu ni mchezaji mwenye kujiamini na ni hatari sana ndani ya boksi. Kadiri akiendelea kucheza sambamba na wachezaji wazuri wa pembeni, atafunga zaidi.”
UBINGWA AZAM KAZI NGUMU
Kwa Azam, Pantev anaamini changamoto kubwa ni uwepo wa Simba na Yanga ambao wana historia kubwa, mashabiki wengi na nguvu kubwa ya kifedha.
“Ukiwa si Yanga au Simba, ni vigumu kuwa bingwa hapa. Hizi ni timu mbili kubwa, maarufu na zenye mashabiki kila mahali. Mashabiki wao ni kama mchezaji wa ziada,” anasema.
“Azam si timu mbaya. Kila msimu inashiriki mashindano ya CAF, wanasajili wachezaji wazuri, wachezaji bora wa Tanzania na wageni wazuri. Wamejenga miundombinu na mfumo wa kitaalamu, huo ndio mwelekeo sahihi.”
VIWANJA VIKIBORESHWA, SOKA LITAKUA
Tatizo moja kubwa analoliona Pantev kwenye Ligi Kuu Bara ni ubora wa baadhi ya viwanja.
Anasema timu na makocha wanaweza kuwa na mawazo mazuri ya kiufundi, lakini wakashindwa kuyaonyesha kutokana na mazingira ya uwanja.
“Viwanja ni muhimu sana. Kama kila timu itakuwa na uwanja wa nyasi bandia au nyasi nzuri, itakuwa rahisi kwa makocha na wachezaji kuonyesha mawazo yao.
“Kila timu inajaribu kuboresha na kuwa kwenye mbio. Hii itasaidia soka na itamsaidia kila mchezaji kukua,” anasema.
SINGIDA, SIMBA, YANGA NA AZAM MTIHANI NI CAF
Pantev anaamini ubora wa vigogo wa Tanzania hautapimwa kikamilifu na mechi za ndani pekee.
“Mtihani mkubwa kwa timu hizi utakuwa kwenye mashindano ya CAF. Hapo ndipo tutaona kama wana ubora wa kushindana na timu kubwa za Afrika,” anasema.
FEI TOTO NI WAKATI WA KUONDOKA
Miongoni mwa wachezaji anaowakubali, Pantev hakusita kumtaja kiungo wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’, akisema sasa ni wakati kwake kuondoka nchini.
“Kama kuna mchezaji ukipata dakika chache utagundua ubora wake ni Feisal. Hapa Tanzania ameshafanya vya kutosha. Kama anaangalia picha kubwa ya maisha yake ya soka, nafikiri uamuzi mzuri ni kwenda nje. Aondoke kwenye kuridhika na maisha yake ya hapa, aende Ulaya, Afrika Kaskazini au ligi nyingine na ajaribu kupanda kiwango,” anasema.
“Kama akishindwa, wakati wowote anaweza kurudi. Lakini kwa sasa nafikiri ni wakati wa kwenda kujaribu kitu tofauti. Huo ni mtazamo wangu.”
MFUKO ANAMKUBALI SIMBA
“Nimefurahi kuona kwa sasa Mfuko anaanza kupewa nafasi ya kucheza. Naye ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana. Bahati mbaya hapati nafasi ya kuonyesha ubora wake. Akiweza, anaweza kuondoka hapa Tanzania.”
TANZANIA INA VIPAJI
Pantev anasema Tanzania ina vipaji vya kutosha, lakini changamoto kubwa ni namna wachezaji wanavyolitazama soka lao. Akitumia uzoefu wake wa kufanya kazi Cameroon na Sierra Leone, anasema amegundua tofauti kubwa katika kiu ya wachezaji kutafuta maisha nje ya nchi.
“Katika nchi kama Cameroon, Ghana, Nigeria na Congo, wachezaji wana njaa kubwa ya kucheza mpira na kuondoka nchini kwenda Ulaya. Tanzania kuna wachezaji wengi ambao hawataki kuondoka kwenye comfort zone yao,” anasema.
“Si lazima uende tu mazoezini na timu. Unapaswa kufanya mazoezi binafsi, kuongeza kitu kingine na kujijenga. Hapo ndipo tofauti inapoanzia,” anasema.
TATTOO ZAKE ZINA MAANA
Pantev pia amezungumzia jambo lililomfanya awe maarufu kwa mashabiki wengi wa Tanzania hata nje ya kazi yake, tattoo zake. Anasema nyingi alizichora akiwa bado mchezaji, zaidi ya miaka 20 iliyopita, na kila moja ina maana yake, likiwemo jina la mwanaye.
“Mwanangu ni fahari yangu na maisha yangu. Ninapendelea kujulikana kwa kazi yangu, sio kupitia tattoo zangu. Sikuwa nafahamu kama mashabiki hapa wamekuwa wakinitambua kupitia hili.”
MWANAWE HAPENDI KUCHEZA CHINI YAKE
Kama hufahamu, Pantev ana mtoto mmoja ambaye pia ni mchezaji anayecheza eneo la kiungo na pia mchezaji mwenye uzoefu wa kucheza katika nchi mbalimbali ikiwamo Croatia, Ufaransa, Botswana na sasa Saudi Arabia.
Licha ya kuwa baba yake ni kocha, Pantev anasema mwanawe hapendi sana kuwa kwenye timu anayoifundisha.
“Kwa kweli hapendi kuwa kwenye timu yangu. Labda kwa sababu macho yote huwa kwake. Kila mtu anamuangalia.”
Pantev amewahi kumchezesha mwanawe mara moja tu, akisisitiza kuwa mara nyingi akishakuwa kocha wa timu nyingine, humuacha mwanawe chini ya mwalimu wake.
“Kama hayuko kwenye timu yangu, namuangalia kama shabiki. Ana kocha wake na wana mpango wao wa kiufundi.”
TANZANIA INAMVUTIA
Licha ya kuondoka Simba kwa namna isiyotarajiwa, Pantev bado anaipenda Tanzania.
“Ninapenda mazingira ya nchi hii. Mimi nimetokea Bulgaria ambako pia ninaishi karibu na bahari. Hapa hali ya hewa iko vizuri, watu wanapenda mpira na kuna mashabiki wengi. Bado sijafikiria kustaafu, nina nguvu za kutosha. Kama ofa itakuja, kwa nini isiwe?”
UJUMBE KWA MASHABIKI
Pantev anawaomba mashabiki wa Tanzania kuendelea kuzipenda timu zao na kuipa nafasi ligi kukua, akisema pia anaamini Taifa Stars inaweza kufanya vizuri katika AFCON inayokuja Tanzania ikiwa mwenyeji.
“Tanzania ilicheza vizuri kwenye AFCON iliyopita. Sasa inapaswa kuongeza kitu na kupiga hatua moja zaidi. Naweza kuja hapa kuangalia fainali hizo, kwa nini isiwe? Nitafurahi kuja,” anasema Pantev.